KOCHA Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Johannes Hans vand der Pluijm amesema tuzo ambazo wachezaji wake wamepewa na uongozi wa Yanga FaceBook Family ni sehemu kubwa ya kuinua morali ya timu wakati huu wanausaka ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara.
Yanga inaongoza msimamo ikiwa na pointi 43 baada ya mechi 20 ikifuatiwa na Azam fc wenye pointi 38 kufuatia kucheza mechi 20 na wana mchezo mmoja wa kiporo watakaocheza jumatano dhidi ya Mgambo JKT CCM Mkwakwani.
Kundi hilo liliwatuza tuzo wachezaji wa Yanga jana wakiwa mazoezini uwanja wa Karume jijini Dar es salaam likionyesha kuthamini mchango wao.
Pluijm amesema tuzo hizo zinawasaidia wachezaji kujua wanafanya kazi kwa ajili yao lakini kuna watu nyuma yao.
“Jambo zuri, kitu kizuri mambo yafuate utaratibu na inasaidia kwa timu. Hivyo wachezaji wajitambue zaidi ya hapo kuwa kuna watu nyuma yao,” alisema.
Pluijm ni kati ya waliopewa tuzo hiyo kutokana na mchango wake katika kikosi hicho ambacho sasa kinaelekea kubeba ubingwa.
Wengine waliopewa tuzo jana ni Mrisho Ngassa, mchezaji bora wa klabu, mfungaji bora wa klabu na kinara wa ufungaji ligi kuu, Simon Msuva na mchezaji bora wa kigeni, Haruna Niyonzima.
Leo jioni Yanga inashuka dimbani kuikabili Mbeya City katika mchezo mgumu wa ligi kuu.


0 comments:
Post a Comment