
Al-Merreikh walizomewa baada ya kutoka suluhu
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Mei 26, 2014, saa 3:08 asubuhi
WENYEJI wa michuano ya CECAFA Nile Basin Cup,
Al-Merreikh ya Sudan jana wamelazimisha suluhu pacha ya bila kufungana katika
mechi ya kundi A dhidi ya Victoria University kutoka Uganda.
Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa habari wa CECAFA,
Rodgers Mulindwa, mashabiki wa Al-Merreikh waliwazomea wachezaji wao baada ya
kipyenga cha mwisho kupigwa kuonesha kuwa hawajaridhishwa na suluhu hiyo.
Kocha wa klabu Al-Merreikh, Mjerumani, Martin Otto
Pfister alikiri kubanwa zaidi na wapinzani wao na kusema kuwa kwa muda wote wapinzani
wao waliharibu mipango yao.
“Kiufundi wako vizuri sana (Victoria University).
Walicheza kwa jitihada kutunyima nafasi za kushinda. Waliharibu mipango yetu na
kutupa nafasi kidogo ya kucheza mpira”. Alisema kocha huyo Mjerumani aliyefanya
kazi Afrika tangu miaka ya 90.
Suluhu ya jana imeifanya Victoria University kuwa
mshindani wa kombe kwasababu timu zote zimefuzu hatua ya mtoano, huku zote zikiwa na mechi moja mkononi.
Mechi nyingine ilizikutanisha timu za Malakia FC
kutoka Sudan kusini dhidi ya Polisi ya Zanzibar.
Kwa mara nyingine tena Maafande hao wa Polisi
kutoka kwa ndugu zetu Wazanzibar waliangukia pua baada ya kuburuzwa mabao 3-0.
Mabao ya Makakia FC yalitiwa kambani na Thomas
Jacob katika dakika ya 68’, 88’ na la
tatu lilifungwa na Richard Justin katika
dakika ya 74’.
Kwa matokeo hayo, Malakia wameonesha kuwa bado
watakuwepo hatua ya robo fainali, lakini Polisi hawana jinsi zaidi ya kurejea
nyumbani baada ya kumaliza mechi yao ya mwisho kesho jumanne.
Mechi nyingine ilipigwa mjini Shandi ambapo Dkhill
ya Djibouti ilipoteza mechi ya pili mfululizo baada ya kukubali kipigo cha
mabao 2-1 kutoka kwa Defence ya Ethiopia.
Matokeo hayo yanawaondoa Dkhill mashindanoni
kwasababu kundi moja linatakiwa kutoa timu mbili za kwanza kuelekea katika
hatua ya mtoano.
Leo jumatatu na kesho jumanne ni mapumziko mjini
Shandi kabla ya wenyeji Al-Shandi kuvaana na Defence siku ya jumatano.

Kocha Juma Mwambusi ataweza kutafuna mfupa wa AFC Leopard?
Michuano hiyo itaendelea leo mjini Khartoum ambapo
wawakilishi wa Tanzania katika michuano hiyo, Mbeya City fc watakabiliana na
AFC Leopard kutoka nchini Kenya majira ya saa 2:00 usiku.
Hii itakuwa mechi nyingine ngumu kwa kocha Juma
Mwambusi kwasababu Leopard ni timu kubwa na yenye uzoefu wa kutosha katika
mashindano makubwa ukanda wa Afrika mashariki na kati.

Pia hata
kihistoria , klabu hii ya Kenya ina muda mrefu zaidi kuliko timu hii changa ya
Tanzania.
Hata hivyo, kocha Juma Mwambusi wa Mbeya City fc
amesema hakuna haja ya kuwaogopa Leopard kwasababu wao wamejiandaa kupambana
kwa mechi zote.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa siku ya
jumamosi, Mbeya City fc walishinda mabao 3-2 dhidi ya Academie Tchite ya
Burundi.
Mbali na Mechi hiyo ya usiku, mapema saa 11:30 kwa
saa za Sudan, Academie watakuwa uwanjani kuoneshana kazi na Etincelles.
0 comments:
Post a Comment