![]() |
Zacharia Hans Poppe amesema wanachama wasipomchagua Aveva na Kaburu anaacha kupoteza muda na fedha zake |
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Tel: 0712461976
Imechapishwa Mei 26, 2014, saa 4:57 asubuhi
WAKATI Wekundu wa Msimbazi Simba sc wakiwa mbioni
kufanya uchaguzi wa viongozi juni 29 mwaka huu, kumekuwa na mambo ya hapa na
pale. Kwasasa kamati ya uchaguzi inasikiliza mapingamizi yaliyowekwa kwa
wagombea wa nafasi tofauti.
Simba iliyododa kwa misimu miwili sasa, mwishoni
mwa mwezi ujao inatarajia kumpata rais mpya, makamu wa rais na wajumbe wa
kamati ya utendaji kwa mujibu wa katiba yao mpya.
Kitu kinachovutia zaidi katika uchaguzi huo ni
aina ya wagombea walioomba nafasi za kuiongoza Simba katika kipindi cha miaka
minne ijayo. Wengi wao walishawahi kuwa viongozi katika uongozi unaomaliza muda
wake na wengine miaka ya nyuma.
Nafasi zinazovuta hisia kubwa ni Urais na makamu
wa Rais. Hapa kuna upinzani mkubwa ulioanza kuonekana tangu zoezi la kuchukua
na kurudisha fomu lilipoanza.
Japokuwa kampeni za uchaguzi hazijaanza kwa mujibu
wa ratiba, baadhi ya wagombea walimwaga sera zao siku ya kuchukua na kurejesha
fomu na kuibua minong`ono miongoni mwa wanachama wa Simba.
Baadhi ya wanachama wa Simba wanaeleza wazi kuwa kuna
baadhi ya wagombea walipiga kampeni kabla ya muda na kumtaka mwenyekiti wa
kamati ya uchaguzi wa klabu hiyo, Wakili na wakala wa wachezaji wa FIFA, Dkt. Damas
Daniel Ndumbaro kuyaengua majina ya wagombea hao.
Ndumbaro amekuwa akikaririwa kuwa kama mgombea
anavunja kanuni za uchaguzi ikiwa ni pamoja na kupiga kampeni kabla ya muda
basi sheria itafuata mkondo wake. Kama amepata ushahidi wa matukio hayo, basi
tusubiri kusikia atalipukaje baada ya mapingamizi kusikilizwa.
Michael Richard Wambura na Evance Aveva ni
wagombea wawili kati ya watatu wa nafasi ya Urais. Watu hawa wawili wanavuma
kama wako peke yao. Inawezekana umaarufu wao na ushawishi mkubwa walionao ndio
sababu ya kuteka Msimbazi.
![]() |
Zacharia Hans Poppe amesema Simba wasipomchagua Evans Aveva nafasi ya urais anaacha kupoteza fedha zake |
Vita ya urais inaonekana kuwa baina yao, ingawa
Wambura alishawekewa pingamizi. Aveva yuko mikono salama. Wambura anasubiri
hukumu yake siku chache zijazo baada ya pingamizi juu yake kusikilizwa.
Nafasi ya umakamu wa rais wapo wagombea wengi,
lakini Jamhuri Musa Kiwhelo `Julio` na Geofrey Nyange Kaburu wamekuwa kivutio.
Hawa wanaonekana kuchuana vikali hata kabla ya mambo kufikia patamu.
Wengi tulimsikia Julio akisema mambo mengi
yaliyomsukuma kugombea na akafika mbali kwa kuwawekea pingamizi viongozi wote waliokuwepo
katika uongozi unaomaliza muda wake chini ya mwenyekiti Ismail Aden Rage na
wameomba tena nafasi za uongozi.
Tuyaweke pembeni hayo kwanza. Makala hii inajaribu
kuakisi maneno ya Kaptein wa zamani wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
Zacharia Hans Poppe.
Poppe ni mwanasimba wa siku nyingi. Anaipenda
Simba kutoka moyoni. Ameisaidia Simba kwa kila namna. Ametumia kiasi kikubwa
cha fedha zake kuisaidia Simba. Ametoa fedha zake sana kuwalipa mishahara
wachezaji na kusajili wachezaji. Ni kipenzi cha wanasimba wengi kwasababu
amekuwa na ushawishi mkubwa mno katika klabu. Ni mtu wa kutuliza shari za ukata
katika klabu hii kubwa nchini.
Ni moja ya watu wanaounda kundi la Marafiki wa
Simba `Friends of Simba`. Hili ni kundi ambalo kwasasa limepunguza kasi yake
kutokana na kushindwa kuelewana na Rage. Wamekaa pembeni kidogo, lakini baadhi
yao wanaendelea kuipenda Simba kama kawaida akiwemo yeye.
Poppe kwasasa ndiye mwenyekiti wa kamati ya
usajili ya Simba. Mwishoni mwa wiki aliongea na matandao huu na kusema tayari
ameshamaliza mazungumzo na wachezaji wawili wa kimataifa, mmoja kutoka Kenya na
mwingine kutoka Uganda.
Poppe alisema kimsingi kila kitu kipo sawa, lakini
hajawapa mikataba kwasababu anasubiri wapatikane viongozi wapya. Pia alisema
wamepata wachezaji wengine 12 wa Kitanzania na kila kitu kipo sawa. Akasema katika
kikosi cha msimu uliopita wamebakiza wachezaji 13 tu.
Wakati Poppe akisubiri viongozi wapya wapatikane
ili aendelee kugawa mikataba kwa wachezaji wapya kwa ajili ya msimu wa
2014/2015, akaibua hoja waziwazi juu ya nani awe rais na makamu wa rais wa
Simba sc.
Poppe alionesha mapenzi ya wazi kwa Aveva katika
nafasi ya urais na Kaburu nafasi ya umakamu wa rais.
Aliweka wazi msimamo wake kuwa kama wanachama wa
Simba hawatawachagua Aveva na Kaburu katika nafasi hizo mbili anabwaga manyanga
katika nafasi yake ya mwenyekiti wa
kamati ya usajili na ataacha kutoa fedha zake.
Mwanajeshi huyo wa zamani anawafagilia wawili hao
kwa madai ya kupata mafanikio wakati wa uongozi wao. Anasema Kaburu alifanya
jitihada kubwa ya kuijenga Simba B iliyozalisha akina Ramadhan Singano `Messi`,
Harun Chanongo, Jonas Mkude, Said Ndemla na wengineo.
Kwa Aveva anampa kura yake kwasababu aliwahi kuwa
mwenyekiti wa kamati ya usajili miaka ya 2000 na katika kipindi chake Simba
ilikuwa kali mno na haijawahi kutokea tena. Aveva ndiye aliyewaibua akina Juma Kaseja,
Suleiman Matola, Boniface Pawasa, Ulimboka Mwakingwe, Emannuel Gabriel Mwakyusa,
na wengineo.
Kama anatumia ukali wa Simba wa miaka ile ya 2000,
2002,2003 kama mafanikio ya Aveva, basi hilo halina upinzani. Ilikuwa timu bora sana na haijawahi kutokea tena.
![]() |
Geofrey Nyange Kaburu amechaguliwa kuwa `makamu wa rais` na Hans Poppe. |
Poppe anasema waziwazi kuwa Richard Wambura
hakuifanyia Simba lolote wakati wa uongozi wake, lakini Kwa Julio ndio kabisa.
Anasema hajafanya lolote kwasababu yeye alikuwa kocha na alikuwa analipwa
mshahara.
Hoja hapa sio Zacharia Hans Poppe kuwa na mapenzi
kwa Aveva na Kaburu. Hoja ya kujiuliza ni kwanini anawaunga mkono na kuona timu
ya uongozi chini ya hawa wawili italeta maendeleo katika klabu ya Simba.
Pia lazima ujiulize na kupata majibu, kwanini
Poppe anatamba kuwa wanachama wasipowachagua Aveva na Kaburu atabwaga
manyanga?.
Nadhani kwa mujibu wa maelezo yake ni kwamba
amechoka kupoteza muda wake na fedha zake katika uongozi unaomaliza muda wake
bila mafanikio yake.
Poppe anatumia fedha zake nyingi kuisaidia Simba.
Nadhani amechoka kumwaga pesa bila
mafanikio. Ndio maana anaona kuna haja ya kumchagulia viongozi watakaoendana
sawa kimawazo na anawapenda Kaburu na Aveva.
Wote wawili, Poppe alifanya nao kazi kwa nyakati
tofauti, yawezekana walikuwa wanaelewana sana.
Aveva ni moja ya watu wa `Friends of Simba`kama
ilivyo kwa Poppe. Kwa pamoja walifanya kazi miaka ya nyuma na kuisaidia Simba
sc kifedha.
Wengi walisema Aveva anagombea urais na nyuma yake
kuna watu wengi wa Friends of Simba akiwemo Kassim Dewji na Poppe. Kwa maneno
ya mwanajeshi huyu wa zamani unaweza kuanza kuamini kuwa Aveva anaungwa na watu
wengi wenye ushawishi ndani ya Simba.
Hata matarumbeta yaliyomsindikiza siku ya kuchukua
na kurudisha fomu, unaweza kusadiki kuwa jamaa huyu ana nguvu sana kuelekea
uchaguzi huo wa juni 29.
Sipingani na mtazamo wa Poppe juu ya viongozi
anaowataka yeye kwasababu ana haki kikatiba akiwa mwanachama wa Simba. Ni
mtazamo wake na maono yake, lakini wanachama ndio watakaochagua watu
wanaowahitaji.
Lakini kama wanachama wanamuamini Poppe na
hawataki aondoke katika nafasi yake ya mwenyekiti wa kamati ya usajili , basi
kwa lugha nyepesi hawatachagua wao ila wataenda kukamilisha zoezi kwa kubariki
kura ya Zacharia Hans Poppe kwa Aveva na Kaburu.
Kuondoka kwa Poppe kunaweza kuwa tatizo kubwa kwa
Simba kifedha. Kila siku tunaandika kuwa ifike wakati Simba na Yanga
zijitegemee kifedha. Wengine kutokana na mapenzi ya klabu zao wanatubatiza
majina ya ajabu.
Wengine wanatuita makanjanja, mamluki ,
wababaishaji na mengineyo. Lakini kamwe haifuti ukweli kuwa Yanga na Simba ni
hovyo katika mipango ya kujiendesha bila kutegemea mamilionea wanaamua kila
kitu.
Timu zenye wanachama kila kona ya nchi, rasilimali
za kutosha, mpaka leo hii zinategemea fedha kutoka mifukoni mwa watu wachache,
hii ni aibu upende usipende!.
Angalia hata Yanga, kuna watu kama Abdallah Bin
Kleib, Yusuf Manji, Clement Sanga, David Mosha, Seif Magari na wengineo. Hawa
jamaa wakisusa hata sekundi hii unaposoma makala haya, basi hali itakuwa tete
mno.
Kama klabu inaendeshwa kwa fedha zao. Maan yake
hawa watu wana ushawishi mkubwa mno na hawawezi kupingwa kirahisi.
Leo hii Manji akisema hapapa! Ni hapana. Si
kwasababu yeye ni mwenyekiti. Ni ushawishi mkubwa wa kifedha alionao katika
klabu ya Yanga.
Watu hawa wanatumia fedha nyingi sana kuzisaidia
klabu hizi mbili. Na wenyewe wana mapenzi yao. Wanataka viongozi wanaowapenda
ili watoe fedha kwa faida.
Poppe yeye amechoka na ubabaishaji, sasa ameamua
kuwachagulia wanachama viongozi. Yuko sahihi kwasababu anapoteza pesa zake.
Lakini kimsingi, hapa sio demokrasia. Maana yake Poppe
kawashawishi wote wanamuamini yeye. Watu wanaompenda hawana ubavu wa kukimbia
machaguo ya mwanaumwe huyu katika klabu ya Simba.
Kama wanafikiri ni utani basi wasiwachague waone.
Hakika maneno ya Poppe yamenifikisha mbali sana na kuona ipo haja ya klabu hizi
kujiuliza upya.
Kama ulimsikia Wambura alisema anataka kuiondoa
Simba kutoka mikononi mwa watu wachache ili ijitegemee kiuchumi. Maana yake
Wambura ana maanisha watu kama Zacharia Hans Poppe wasiwe tegemeo kwa asilimia
100.
Binafsi mawazo ya Wambura nayaunga mkono, japokuwa
yapo mdomoni mwake na sijui kama anaweza kutekeleza. Sisemi ndiye achaguliwe. Lakini ukweli unabaki
kuwa mawazo yake ni bora hasa kwa wakati huu Simba inapohitaji kupiga hatua.
Mara nyingi unapotaka kufanya mabadiliko lazima
ukubali athari. Kama Wanachama wanataka kuibadili Simba, wakubali kuwa
wavumilivu. Lakini kama wanataka mabadiliko ya haraka, basi watazingatia
maamuzi ya watu kama Poppe.
Yeye ana jeuri ya fedha. Wakimpuuza sijui nani
atawalipa mishahara na posho wachezaji wanapotaka kwenda Zanzibar kuweka kambi
kujiandaa na mechi ya mtani wake wa jadi, Yanga SC. Daah! Inatia uchungu sana
kuona mtu mmoja ana maamuzi makubwa kiasi hiki. Simpingi Poppe, ni mapendekezo
yake. Lakini hili la kuondoka madarakani kama Kaburu na Aveva hawatachaguliwa,
hapo sasa kuna tatizo.
Narudia tena! Simpingi Poppe hata kidogo kwasababu
kweli anapoteza pesa zake. Lakini kuna haja gani kwa klabu kubwa ya Simba
kuwategemea watu kama hawa?. Kwanini wasiwe katika nafasi ya wadau wa Simba
wanaochangia kwa hiari?. Hata wasipochangia mambo yawe yanakwenda tu.
Nani atakuwa rais na makamu wa rais wa Simba?.
Juni 29, 2014, jibu litapatikana. Poppe yeye amewachagua Aveva na Kaburu.
Wanachama wanasemaje?, tusubiri siku ya uchaguzi.
Nawatakia jumatatu njema wana Simba wote na wadau
wa soka.
0 comments:
Post a Comment