Rais Jakaya Kikwete.PICHA|MAKTABA
Geita.Rais Jakaya Kikwete jana
aligoma kupokea zawadi ya dhahabu kutoka Kampuni ya Nyamigogo Grand
Vezir Holdings ya mkoani Geita.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu
jana ilisema viongozi wa kampuni hiyo walitaka kumkabidhi Rais Kikwete
gramu 227 za dhahabu safi wakati alipotembelea mgodi huo.
Rais Kikwete badala yake aliwaelekeza waiuze dhahabu na fedha zitakazopatikana zitumike kuwasaidia watoto yatima.
Alikabidhiwa zawadi hiyo wakati
wa sherehe ya kuzindua mgodi wa uchenjuaji dhahabu wa kampuni hiyo nje
kidogo ya mji mdogo wa Kharuma ambao ni makao makuu ya wilaya mpya ya
Nyang’hwale, Geita.
Gramu hizo 227 zina thamani ya Sh16 milioni kwa bei ya sasa ya soko la dhahabu duniani.
Baada ya kukabidhiwa zawadi
hiyo, Rais Kikwete aliuliza: “Sasa nifanye nini na zawadi hii?
Nawarudishieni hii dhahabu, iuzeni popote mnakotaka na fedha
itakayopatikana tutawapa watoto yatima.”
Akizungumza na wananchi katika
mgodi huo, Rais Kikwete aliupongeza uongozi wa mgodi huo akisema
umeongeza thamani ya dhahabu na maisha ya wananchi katika eneo hilo…
“Mmefanya vizuri na mgodi huu, ni mradi wa maana kwa kuongeza thamani ya
dhahabu na kuboresha maisha ya wananchi katika eneo hili. Ubunifu huu
unastahili pongezi,” alisema Rais Kikwete.
Mgodi wa Nyamigogo ni wa marudio
kwani unazalisha dhahabu kutokana na mchanga ambao awali ulishafuliwa
na kutoa dhahabu. Ulianzishwa mwaka 2011 na mpaka sasa kiasi cha Sh 1.6
bilioni kimewekezwa kuuendeleza.
Uongozi wa mgodi huo ulisema
mgodi huo unaozalisha kiasi cha gramu kati ya 500 na 600 kwa mwezi, na
unaajiri watu 45 kati yao wanawake 10.
Rais Kikwete alizindua mgodi huo
ikiwa sehemu ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika ziara
yake Geita ambao ni moja ya mikoa minne aliyoianzisha mwaka jana. Mikoa
mingine ni Simiyu, Njombe na Katavi.
Amtetea Magufuli
Rais
Kikwete amewataka viongozi wa CCM kuacha kulalamikia utendaji wa
viongozi na badala yake kuelimisha wananchi juu ya utendaji wa Serikali.
Akizungumza wakati wa kikao cha
majumuisho ya ziara yake ya siku tano mkoani Geita, Rais Kikwete alisema
viongozi hao walimpinga Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli wakati akiwa
Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi alipokuwa akipambana na uvuvi
haramu.
“Walimwona mbaya, tena hata
wazee wa CCM walilalamika na kupiga kelele… anatuharibia kura, sasa
hayupo, samaki wamekwisha ziwani. Watu wenu wamebaki kuwa maskini na
hakuna samaki,” alisema.
Aliwahimiza
viongozi wa Mkoa wa Geita kufikiria mpango wa kufuga samaki akitoa
mfano wa Vietnam ambayo sasa inafuga sato na sangara kwa kiasi kikubwa.
CHANZO: MWANANCHI


0 comments:
Post a Comment