Dk Sengondo Mvungi.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam.Mjumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi (61) amefariki dunia katika
Hospitali ya Millpark Netcare, Johanesburg, Afrika Kusini.
Habari zilizolifikia gazeti hili
jana kutoka Afrika Kusini na kuthibitishwa na Msemaji wa Hospitali ya
Millpark, Tebogo Nyembezi zinasema Dk Mvungi alifariki dunia jana
mchana. “Ni kweli tulimpokea mgonjwa huyo kutoka Tanzania na alifariki
6:00 mchana (saa 7:00 kwa saa za Afrika Mashariki),”alisema Nyembezi.
Nyembezi alisema kwamba
walimpokea mgonjwa huyo akiwa na majeraha ya kichwa, lakini aliahidi
kueleza sababu ya kifo chake leo baada ya kuzungumza na madaktari
waliokuwa wakimtibu.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Jaji Joseph Warioba pia alithibitisha kupokea taarifa za
kifo hicho na kwamba walikuwa wakiendelea kuandaa taratibu za kuleta
mwili wake nchini.
“Ni pigo kubwa kwetu,
tunaangalia namna ya kuusafirisha kuja nchini na baadaye tutatoa taarifa
rasmi,”alisema Jaji Warioba na kuongeza:
“Kwa kweli ni pigo kubwa siyo
kwetu tu, lakini pigo kubwa kwa nchi yetu, tumepoteza mtu muhimu na
kiungo muhimu sana. Dk Mvungi, wengine tulimfahamu tangu alipokuwa
mwanafunzi, alikuwa mtu aliyesema kile alichokiamini, akikwambia kitu
kilikuwa ni kile kilichopo moyoni mwake”.
Jaji Warioba alisema Dk Mvungi
alikuwa msomi aliyebobea katika masuala ya sheria na kwamba alikuwa na
mchango mkubwa katika tume. Pia alisema marehemu atakumbukwa kwa
ushiriki wake wa dhati katika kupigania haki za binadamu, kazi
aliyoifanya kwa moyo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa tume
hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani alisema: “Dk Mvungi alikuwa
mfanyakazi hodari, alikuwa hachoki na hata ulipotokea ubishi mkubwa
katika majadiliano kiasi cha watu wengine ku-loose temper (kupandwa na
jazba), yeye alibaki vilevile na alizungumza vilevile bila kubadilika.
Kweli tumempoteza mtu muhimu sana maana alikuwa akifahamu vizuri sana
sheria, hatuna jinsi maana tumempoteza, kwahiyo itabidi tuendelee na
kazi hii. Hatuna namna nyingine ya kufanya,”alisema Jaji Ramadhani.
Jaji Ramadhani alisema taratibu
nyingine zitatangazwa baadaye kwani lazima washirikiane na chama chake,
NCCR- Mageuzi alikokuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji, familia yake na
Chuo Kikuu cha Bagamoyo ambako alikuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi,
James Mbatia aliliambia gazeti hili kwamba walipokea taarifa ya kifo cha
Dk Mvungi saa 9.30 alasiri jana. “Tumepokea taarifa hizo alasiri kwamba
amefariki. Ni kweli na sasa ninaelekea nyumbani kwake ili kuitaarifu
familia,”alisema Mbatia.
Taarifa ya Tume
Jana
jioni, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa taarifa rasmi kuhusu kifo cha
Dk Mvungi ikisema: “Kwa masikitiko makubwa, Tume ya Mabadiliko ya
Katiba inawafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake Dk Sengondo Mvungi
aliyekuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Millpark iliyopo jijini
Johannesburg, Afrika Kusini amefariki dunia.”
Taarifa iliyotolewa Katibu wa
tume hiyo, Assaa Rashid ilisema Dk Mvungi alifariki dunia saa 8:30
mchana kwa saa za Afrika ya Kusini.
Iliendelea kusema taarifa hiyo
kuwa taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka Afrika Kusini
kuja nchini kwa maziko zinaendelea na taarifa zaidi zitatolewa baadaye.
Dk Mvungi, alikuwa akitibiwa
Afrika Kusini baada ya kujeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana
walipovamiwa nyumbani kwake Kibamba, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es
Salaam, Novemba 3 mwaka huu.
Alipelekwa nchini Afrika Kusini,
Novemba 7, 2013 kwa matibabu zaidi baada ya kulazwa kwa siku tano
kwenye Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (Moi)
jijini Dar es Salaam.
Dk Mvungi, ambaye aligombea
urais mwaka 2010 kwa tiketi ya NCCR- Mageuzi, alijeruhiwa vibaya
kichwani na sehemu nyingine za mwili wake baada ya kukatwa mapanga na
wavamizi hao.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Bagamoyo, Profesa Costa Mahalu alisema chuo hicho kimepoteza mtu muhimu
sana, kwani ni mmoja wa waanzilishi waliokuwa wakifahamu vyema malengo
na dira yake.
“Tumepata pigo kubwa sana kwani
tumempoteza mtu ambaye tulishirikiana naye katika kuanzisha chuo hiki na
aliyafahamu vyema malengo na dira yake, alikuwa ni mwalimu mzuri
aliyebobea katika constitutional laws (sheria za Katiba) na wanafunzi
walimpenda sana,”alisema Profesa Mahalu.
Profesa Mahalu alisema Dk Mvungi
ambaye alikuwa naibu wake kabla ya kujiunga na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, walifahamiana naye siku nyingi na kwamba wakati marehemu
alipokwenda kusoma Shahada ya Uzamivu nchini Ujerumani alifikia nyumbani
kwake (kwa Mahalu).
“Wakati huo nilikuwa
nikifundisha Ujerumani, alikuja kusoma PhD yake ya masuala ya sheria na
alifikia nyumbani kwangu, tutamkumbuka kwa uhodari wake katika kuchapa
kazi, kweli tumempoteza mtu mahiri sana,”alisema.
Chadema, CCM wamlilia
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe alisema amesikitishwa na taarifa za kifo cha Dk Mvungi na kwamba
taifa limempoteza mwanzilishi wa mageuzi ambaye alikuwa mstari wa mbele
katika kudai Katiba Mpya.
“Tumepokea
taarifa za kifo hiki kwa mshtuko mkubwa, tunamwomba Mwenyezi Mungu aipe
nguvu familia ya Dk Mvungi, tunatoa pole kwa Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na uongozi wa NCCR-Mageuzi,”
alisema Mbowe.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa (CCM),
Mwigulu Nchemba alisema amepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa na
kutoa pole kwa Watanzania wote kwa sababu Dk Mvungi alikuwa anafanya
kazi muhimu ya kuwezesha kupatikana kwa Katiba Mpya.
Alisema amekufa wakati mchango
na mawazo yake yakiwa yanahitajika kwa kiasi kikubwa katika Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na kwamba CCM kinaendelea kuisisitizia Serikali
iwasake wahalifu hao ili wafikishwe kwenye vyombo vya dola.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willbrod Slaa alisema ameshtushwa na taarifa za kifo hicho ambacho
kimetokea wakati Dk Mvungi akifanya kazi muhimu ya kuitafuta Katiba
Mpya. “Naomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi,
amina,” alisema.
Mwenyekiti wa Democratic Party
(DP), Mchungaji Christopher Mtikila alisema taifa limepoteza mtu muhimu
na kwamba hali ya ulinzi ni suala linalohitaji mjadala wa
kitaifa.“Tunahitaji kuangalia kiini cha uhalifu hapa nchini, watu
wanateswa na kujeruhiwa ovyo ni lazima tuchukue hatua,” alisema.
Mitandao ya kijamii
Muda mfupi baada ya taarifa za
kifo chake, mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter na Jamii
Forum ilikuwa ilitawaliwa na salamu za pole kutoka kwa watu mbalimbali.
Hussein Bashe kwenye ukurasa
wake wa Facebook aliandika kuwa, “Dr Sengondo Mvungi Is No More
(hatunaye tena), taarifa zilizonifikia kutoka Hospitali ya Millpark,
ndugu yetu Mvungi amefariki, mnamo saa tisa na nusu.
Mungu ailaze roho ya marehemu
mahali pema peponi. Wahalifu wamekatisha uhai wake wakati akifanya
jukumu zito kwa ajili ya taifa letu. Jambo hili linaumiza sana Mungu
atalipia uhalifu huu, poleni Tume ya Katiba, Poleni Familia, poleni
NCCR-Mageuzi.”
Mtu
mwingine aliyechangia suala hilo kwenye mtandao wa Jamiiforum ni yule
aliyejitambulisha kwa jina la Ta Muganyizi aliyeandika kuwa, RIP Dr.
Mvungi… Mungu akulaze mahala pema peponi. Japo umeondoka kivuli chako
kitaishi… Naipa pole familia yako, maisha yetu kwa sasa nchini ni kudra
za Mwenyezi Mungu. Ni kwamba tupigwe… wengine wamepona lakini wewe
umeondoka.”
CHANZO: MWANANCHI


0 comments:
Post a Comment