Jumuiya
ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umepokea kwa
masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha mjumbe wa tume ya mabadiliko ya
katiba Dr Sedondo Mvungi ambacho kimetokea katika hospitali ya Millpark
nchini Afrika kusini.
Uongozi
wa UVCCM Taifa unatoa pole kwa familia na ndugu wa marehemu, pia UVCCM
inatoa pole kwa uongozi wa NCCR- Mageuzi na kwa Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba Jaji Warioba pamoja na Vijana nchini kote ambao
wamenufaika na Utaalamu na mafunzo. Kama vijana tulihitaji sana mchango
wa mawazo, hekima na utaalamu kutoka kwake, hakika tumepoteza kiongozi
shupavu, muadilifu na mzalendo ambae ni mfano wa kuigwa kwa Vijana wa
Taifa hili.
Kadhalika,
UVCCM inatoa pongezi za dhati kwa hotuba makini iliyojaa hekima, busara
na ushupavu wa Uongozi iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete.
Hakika
vijana tumeridhishwa na maamuzi ya Mheshimiwa Rais ya Kuendelea kuwa
Mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na tunapongeza maamuzi
hayo yanayolenga kudumisha Umoja na Ushirikiano wa Nchi za kiafrika
katika kujiletea maendeleo. Kwa kutambua nafasi na manufaa
yanayopatikana kwa vijana kutokana na fursa za kiuchumi, kisiasa,
kijamii, ajira nk UVCCM Inamuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake
huo.
Pamoja
na kuunga mkono uamuzi huo, UVCCM inatoa angalizo kuwa ni vyema kwa
nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuendelea
kuheshimu taratibu na kanuni za jumuiya hiyo ili kuifanya endelevu,
imara na mfano kwa nchi nyingine za Afrika na Duniani kwa ujumla. Ni
lazima wazingatie kuwa Umoja na Mshikamano ndio nguzo ya maendeleo ya
kweli ya Afrika.
Pia,
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesikitishwa na tuhuma
ambazo zimeripotiwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari kutoka kwa
Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA) Mheshimiwa Godbless Lema ambazo
amezielekeza kwa baadhi ya Viongozi wa Jumuiya akiwemo Mwenyekiti wa
Taifa wa UVCCM Ndugu Sadifah Juma kuwa amehusika na usambazaji wa Picha
chafu mitandaoni.
Pamoja
na kusikitishwa, UVCCM inazo taarifa juu ya mgogoro unaoendelea katika
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kwamba inamtaka Lema
kutoelekeza tuhuma kwa UVCCM na viongozi wake bali waangalie namna bora
ya kushughulikia na kutatua migogoro yao ya ndani ambayo imesababisha
kuzushiana, kuchafuana na kuvujishiana siri katika mitandao hasa ya
kijamii.
UVCCM
na Viongozi wake inakana kwa namna yeyote ile kuhusika na usambazaji
huo na kwamba Jumuiya hii ni ya Vijana makini na wanaojitambua na
inajielekeza katika kufanikisha malengo ya kuundwa kwake ya kukisaidia
Chama kushika dola mwaka 2015.
Na
kwamba UVCCM inalaani tabia ambayo imeasisiwa na Vijana wa CHADEMA ya
kukashifu, kuzomea na hata kutukana Viongozi wa CCM na Serikali yake na
kwamba yaliyomkuta Mhe Lema ni matunda ya kazi waliyoiasisi wenyewe.
Imetolewa na:
PAUL MAKONDA
KATIBU WA IDARA YA HAMASA NA CHIPUKIZI
UVCCM
13/11/2013


0 comments:
Post a Comment