
WATU wanaicheka Simba kwa kutolewa na Coastal Union kwenye robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), lakini wasichotambua ni kuwa timu hiyo kwa sasa inatega mitego ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Kitendo cha Simba kutolewa kwenye Kombe la FA, kinamaanisha timu hiyo imepoteza tiketi moja ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani kwa sababu bingwa wa michuano hiyo ndiye ataiwakilisha Tanzania Bara katika Kombe la Shirikisho barani Afrika msimu ujao.
Lakini kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya timu hiyo kwa sasa imeelekeza nguvu zake zote kwenye kuhakikisha inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ili kushiriki kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu.
Akizungumza na BINGWA, Rais wa Simba, Evans Aveva, ametamba kuwa timu yake haijakata tamaa ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani na kwamba kwa sasa hivi miamba hiyo ya Msimbazi inajipanga zaidi kuhakikisha inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
“Kiukweli lolote linaweza kutokea msimu huu cha msingi ni kuwa sisi hatujakata tamaa na tunaendelea na mikakati ya kuhakikisha ubingwa wa ligi kuu unarudi Msimbazi msimu huu,” alisema Aveva.
Akionekana kuungana na kauli iliyotolewa na rais wake, kocha wa Simba, Jackson Mayanja, kwa upande wake naye alifunguka na kusema kuwa kwa sasa akili yake yote ipo kwenye ubingwa wa ligi.
Mayanja alisema baada ya kutolewa kwenye Kombe la Shirikisho hawana tena presha ya kushiriki michuano mingi, hivyo nguvu, akili na mkazo wa timu yake wote uko kwenye mbio za ligi ambako wanaongoza kwa tofauti ya pointi moja mbele ya Yanga inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 56 na mchezo mkononi.
“Akili yetu kwa sasa ipo kwenye ligi kwa sababu ndicho kitu tulichobaki nacho, hivyo tunapambana usiku na mchana kuhakikisha tunatimiza malengo yetu,” alisema Mayanja. “Kwenye soka chochote kinaweza kutokea hivyo bado hatujakata tamaa ya kutwaa taji msimu huu.”
Naye mchambuzi mahiri wa soka katika magazeti ya BINGWA na Dimba, Ally Kamwe, alisema kutolewa kwa Simba kwenye Kombe la Shirikisho kuna faida kubwa sana kwa timu hiyo licha ya wenyewe kubezwa na wapinzani wao.
Kamwe alisema kutolewa kwa Simba kunamaanisha timu hiyo kwa sasa imeelekeza nguvu zake zote kwenye mechi sita za ligi kuu zilizobakia wakati wapinzani wao Yanga na Azam wakiwa kwenye michuano mitatu kitu kinachowapa wakati mgumu sana kupumzisha wachezaji wao.
“Unajua Simba imefaidika sana baada ya kutolewa na Coastal kwenye Kombe la Shirikisho,” alisema Kamwe na kuongeza: “Sasa hivi hawana tena presha ya michuano mingine akili yao yote ipo kwenye ligi.
“Lakini Yanga na Azam ona leo (jana) wamecheza ligi wakimaliza wana ratiba ya mechi za kimataifa ugenini, kisha wakirudi wanakutana na nusu fainali ya Kombe la FA kitu ambacho kitasababisha wachezaji wao wachoke sana na kupoteza nguvu ya kuendelea kupambana kwenye ligi na kuipa faida kubwa Simba ambayo itakuwa imetulia tu ikijiandaa na mechi zake za ligi zilizosalia.
“Halafu kitu kingine ambacho watu wanaweza wasikione ni kuwa kama Simba ingevuka robo fainali ingeweza kukutana na Yanga na siku zote inajulikana namna matokeo ya kwenye mechi hii yanavyoweza kuivuruga timu, lakini kwa sasa hawana changamoto hilo ni jukumu la Mayanja tu kukaa chini kuandaa kikosi chake kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu zilizosalia.”
Simba kwa sasa inaongoza ligi ikiwa na pointi 57 baada ya kucheza michezo 24, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 56 katika michezo 23 na nafasi ya tatu inashikiliwa na Azam yenye pointi 55.
0 comments:
Post a Comment