Umewahi kuwaona wachezaji wa mataifa mbalimbali duniani wakijifunika bendera za nchi zao baada ya kutwaa ubingwa fulani wakiwa na klabu wanazochezea ugenini? Ndicho anachotaka kufanya Mbwana Samatta baada ya staa huyo wa kimataifa wa TP Mazembe na Taifa Stars juzi Jumapili kumkabili Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Msafiri Mgoyi jijini Blantyre akimuomba awatafutie bendera ya taifa yeye na staa mwenzake, Thomas Ulimwengu kwa ajili ya pambano lao la fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya USM ya Algeria.
TP Mazembe imetinga fainali ya klabu bingwa ya Afrika na itachuana na USM katika mechi mbili za fainali Oktoba 30 huko, Algeria kabla ya kucheza pambano la pili la fainali za marudiano jijini Lubumbashi Novemba 8.
“Bosi tutafutie bendera za Tanzania tukishinda mechi za fainali tujifunike kama wenzetu. Unajua kuwa sisi hatuna bendera kabisa pale Lubumbashi,” alisema Samatta akiungwa mkono na Ulimwengu.
Mgoyi aliahidi kuwatafutia bendera mastaa hao pindi watakaporudi jijini Dar es salaam baada ya pambano la jana Jumapili dhidi ya Malawi la kufuzu hatua za makundi michuano ya Fainali za Kombe la Dunia 2018 lililopigwa katika uwanja wa Kamuzu Banda.
Endapo TP Mazembe itatwaa taji hilo, Samatta na Ulimwengu watakuwa wachezaji wa kwanza katika historia ya Tanzania kufanikiwa kulitwaa taji hilo, hivyo watajijengea heshima kubwa nchini.
Chanzo:Mwanaspoti
Chanzo:Mwanaspoti
0 comments:
Post a Comment