Saturday, July 4, 2015

JICHO LA TATU   [email protected]

Na Simon Chimbo;

Timu ya taifa ya wanawake Tanzania, maarufu Twiga Stars inatarajia kuanza michuano ya All African games mwezi Septemba mwaka huu.

Twiga Stars inatarajia kuanza michuano hiyo dhidi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo mwezi huo wa septemba.

Timu hiyo ya Twiga Stars iliyopo chini ya kocha Logatian Kaijage ni miongoni mwa timu kumi bora barani Afrika kutokana na viwango vya soka vya siku kadhaa zilizopita vya FIFA ya soka la wanawake.

Lakini kuelekea katika mashindano haya ya All African games, napata wasiwasi hasa wa jitihada za shirikisho la soka Tanzania, TFF kuiwezesha Twiga Stars.

Taarifa zilizopo ni kwamba Twiga Stars itaanza kambi ya kujiandaa na michuano hii mwanzoni mwa mwezi huu wa Julai, ni sawa lakini ushindi wa timu ni zaidi ya kuweka kambi miezi miwili. Nimesema nina tia shaka jitihada zinazooneshwa na chombo chenye dhamana ya kuiwezesha timu hii yaani TFF kwa kua hadi sasa sijasikia lolote toka kwa shirikisho hilo kama tulivyozoea kwa timu ya wanaume, na hilo linapunguza morali kwa wanadada hawa ambao wamewahi kutuwakilisha vizuri kuliko hata wanaume katika michuano ya kimataifa.

Naunga mkono muda wa kambi uliowekwa kimsingi unatosheleza, lakini shida hapa inakuja kwamba tulihitaji mechi nyingi za kirafiki ili kuwapa uzoefu na umakini dada zetu hasa katika hatua kubwa kama hii.

Timu nyingi zinazoenda shiriki michuano hii zilikuwepo katika michuano ya kombe la dunia la FIFA la wanawake na hapa ndio napata shida kuamini, tunaweza kupata chochote katika michuano hii ya All African games.

Timu hizi zilizotoka katika fainali za kombe la dunia hivi karibuni, kiufundi ziko vizuri zaidi ya timu yetu ambayo husahaulika hadi tunapopata mashindano.

Maandalizi ya ‘zima moto’ ambayo tumeyazoea kuona mara kadhaa timu hii inaenda katika mashindano yanakatisha tamaa hasa kwa watanzania wanaoipenda timu yao lakini pia kwa wachezaji wetu.

Wito wangu kwa wahusika ni kwamba, kama tunahitaji kushindana na sio kushiriki, miezi miwili inatosha kwa kambi ya mwezi mmoja na mwezi wa mwisho tunaweza pata mechi angalau tatu ngumu za kutupa uzoefu na kujiamini kwa wachezaji wanapoanza kuipeperusha bendera ya nchi.

Lakini pia TFF wanatakiwa kuwa na ligi thabiti za akina dada ili kuzidi kupata vipaji zaidi na kuwaimarisha waliopo na sio kutegemea juhudi binafsi na kuibuka tu kwa wachezaji kutoka tusikokujua. Ligi bora ya wanawake nchi nzima itazaa timu bora ya taifa la Tanzania.

Mwisho nitoe wito kwa wadau wote wa michezo nchini kutoegemea tu kwa timu za taifa za wanaume pekee bali kuiangalia pia timu yetu ya Twiga Stars ili kuwatia nguvu wafanye vizuri katika mashindano wanayoiwakilisha nchi yetu.

0 comments:

 
https://www.sexmutant.com/ https://www.sexindrag.com/ porn movies sex videos hd porno video