KIFAA kipya cha Simba, kiungo Peter Mwalyanzi ambaye mwezi uliopita alisaini mkataba wa miaka miwili kukipiga Msimbazi, amefanya mambo makubwa wakati wa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Abbas Mtemvu kwenye Uwanja wa Mwembe Yanga, Temeke, jijini Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na kufunga bao.
Katika mchezo huo uliovuta hisia za mashabiki wengi wa soka wa Temeke na kwingineko, Mwalyanzi alikuwa akiichezea timu ya Kata ya 14 ya Temeke iliyokuwa ikichuana na Kata ya Mtoni za wilayani humo.
Katika mchezo huo, Mwalyanzi akionekana kwa mara ya kwanza kwenye viwanja vya Dar es Salaam tangu aliposaini mkataba wa kuichezea Simba, alionyesha uwezo wa hali ya juu katika kumiliki mpira, akiwa na kasi, chenga, mporaji mzuri wa mpira na mwenye mashuti makali hali iliyomfanya kushangiliwa mno na umati wa mashabiki wa soka waliojitokeza kwenye uwanja huo, hasa wale wa Simba wakiamini wamepata kifaa cha nguvu.
Source: Bingwa
0 comments:
Post a Comment