YANGA SC wameshangazwa na kitendo cha mahasimu wao Simba
kuwabeza kwa matokeo waliyopata katika mechi mbili za hatua ya 16 ya kombe la
Shirikisho dhidi ya Etoile du Sahel.
Mabingwa hao wapya wa Tanzania bara walitoka sare ya 1-1
uwanja wa Taifa majuma mawili yaliyopita na juzi walifungwa 1-0 na Etoile,
hivyo kutolewa kwa ushindi wa jumla ya magoli 2-1.
Mkuu wa Idara ya mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro amesema: “Wenzetu
wa upande wa pili (Simba) wanatubeza kwa matokeo tuliyopata, sisi hatuna
kinyongo na matokeo hayo, timu ilicheza kwa kiwango cha juu. Angalia kipindi
cha pili hali ya umiliki wa mpira sisi tulikuwa na asilimia 51 kwa 49 za Etoile
du Sahel, sasa anaanzaje kubeza kiwango chetu”
“Wao waache watubeze tu, lakini sisi ni wa kimataifa zaidi,
tunakuja nyumbani kumalizia mechi zetu mbili za ligi kuu kwa ubora uleule,
tukimaliza tutawapumzisha vijana wetu mahiri na mwakani wakimataifa watarudi
tena kwenye ligi ya mabingwa”.
Yanga itacheza mechi ya ligi kuu kesho kutwa dhidi ya Azam
fc kabla ya kusafiri kwenda Mtwara kuchuana na Ndanda fc mei 9 mwaka huu.
Msafara wa Yanga unatarajia kutoa leo uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es salaam majira ya saa 8:00 mchana.
0 comments:
Post a Comment