SIMBA SC inaamini mechi ya kesho ya ligi kuu Tanzania bara baina
ya Azam fc na Yanga itayopigwa uwanja wa Taifa, Dar es salaam itakuwa nzuri na itatoa burudani
kwa wapenzi wa soka.
Mkuu wa Idara ya habari na Mawasiliano wa Simba, Hajji
Sunday Manara amesema kuwa kesho watu wawili waliowanyoa wanakutana na hiyo
ndio raha ya Simba mwaka huu.
“Kesho timu ambazo tulishazifunga zinakutana,tunachoamini
mechi itakuwa nzuri, unajua raha ya Simba hivi sasa ni kwamba tumezifunga timu
zote ambazo ziko juu yetu, tumewafunga mabingwa wa mwaka jana, tumewafunga
mabingwa wa mwaka huu, na hao hao tena mmoja anashika nafasi ya kwanza na
mwingine nafasi ya pili, kesho wanakutana, tunaamini mechi itatoa burudani,
wote ni watu wetu, wote tulishawanyoa, wanapambana wenyewe”. Amesema Manara.
Kuhusu Simba kuishangilia Yanga kesho ili iwafunge Azam na
kupata upenyo zaidi wa kuchukua nafasi ya pili, Hajji amekanusha na kusema
hakuna shabiki wa Simba anayeweza kuishangilia Yanga.
“Kama Simba Simba tunapenda kuona tunapata nafasi ya pili na
kucheza mashindano ya kimataifa kutokana na matokeo ya kesho hususani Azam
kufungwa, lakini hakuna shabiki wa Simba anayeweza kuishangilia Yanga, heri ya
lawama kuliko fedheha, sisi tunataka nafasi ya pili kwa udi na uvumba, lakini
narudia heri ya lawama kuliko fedhewa”. Amesema Hajji akimaanisha katu hawawezi
kuishangilia Yanga.
Simba wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 44 baada ya
kucheza mechi 25, pointi moja nyuma ya Azam fc wanashika nafasi ya pili
wakijikusanyia pointi 45 kufuatia kucheza mechi 24.
Ili Simba ichukue nafasi ya pili, inabidi Azam wafungwe
kesho, halafu watoa sare mechi ya mwisho mei 9 mwaka huu dhidi ya Mgambo JKT
uwanja wa Azam Complex, lakini nao Simba watatakiwa kushinda mechi ya mwisho
dhidi ya JKT Ruvu uwanja wa Taifa mei 9.
0 comments:
Post a Comment