Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe
UTANI wa jadi una raha yake! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema!
Ile ishu ya Simba kuishangilia Yanga katika mechi ya kesho dhidi ya Azam fc imekuwa tamu ambapo kila upande unasema
yake.
Kama Yanga wataifunga Azam fc kesho itakuwa nafuu kwa Simba
wanaoiwania nafasi ya pili kwa udi na uvumba.
Azam akipoteza mchezo wa kesho na kutoka sare mechi ya mwisho mei 9 mwaka huu dhidi ya Mgambo
JKT, halafu Simba ikashinda mechi yake ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu, basi Mnyama
atachukua nafasi ya pili.
Katika msimamo Azam wanashika nafasi ya pili kwa pointi 45
baada ya kucheza mechi 24, wakati Simba wanashika nafasi ya tatu wakijikusanyia
pointi 44 kwa kucheza mechi 25.
Turudi kwenye utani wa jadi! Leo mkuu wa Idara ya habari na
mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro amesema: “Kama wao (Simba) wataona kuna haja
ya kuishabikia Yanga waje, wavae jezi za Yanga wakiongozwa na viongozi wao,
wachezaji watapata morali, wataweza
kushinda. Wao waite matawi yao, wavae jezi za Yanga, wachezaji wapate morali. Akina
Msuva wakiona makofi yamekuwa mengi wataongeza mbwembwe na kufunga, niwaombe
viongozi wa Simba wavae jezi za Yanga waje kuishangilia Yanga, vijana wa Yanga
watahamasika wakimuona Hans Poppe amevaa jezi ya Yanga, yuko mbele na kitambi
anashangilia Yanga au Aveva (Evans-Rais wa Simba) anashangilia Msuva
funga..funga.. wanaweza kushinda”.
Baada ya maneno hayo ya Muro, mwenyekiti wa kamati ya
usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amejibu mapigo kwa kusema: “Sijui nani
anaweza kuwapigia magoti hao Yanga, mimi ninachoweza kusema uwezo wetu ndio
umetufikisha hapa, watu wengine wasiwe na cha kutafuta, kama yatatokea matokeo
yoyote wakawafunga basi yatokee hivyo lakini sio kwa kuwabeba. Kama mechi zetu
za nyuma hatukucheza vizuri, basi ni matatizo yetu, tumeyakoroga wenyewe, msimu
ujao unakuja, tutafanya vizuri na tutachukua nafasi nzuri, lakini hatuwezi
kuwaomba Yanga, mimi binafsi sitaweza kwenda kuwaomba, wala sina haja ya
kufanya hivyo, sisi tutaingia kwenye mashindano, tutashinda kwa uwezo wetu na
tukifungwa tutafungwa kwa uwezo wetu”.
0 comments:
Post a Comment