Kessy (kushoto) atawakosa JKT Ruvu
MLINZI wa kulia wa Simba, Hassan Ramadhan Kessy ni nguzo muhimu ya Wanasimbazi kutokana na aina ya uchezaji wake.
Kessy ana kasi, anapiga pasi, anapandisha mashambulizi, anapiga krosi na kurudi kukaba kwa haraka.
Beki huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar anashirikiana vizuri na Ramadhani Singano 'Messi' ambaye kocha mkuu wa Simba, Goran Kopunovic hupenda kumpanga winga ya kulia.
Licha ya kuwa na huduma muhimu, Simba itamkosa Kessy katika mechi ya mwisho ya ligi kuu msimu huu dhidi ya JKT Ruvu itayopigwa uwanja wa Taifa Dar es salaam mwishoni mwa juma hili.
Sababu ya Kessy kuikosa mechi hiyo ni kadi tatu za njano ambazo zinamlazimu kukosa mchezo mmoja kwa mujibu wa kanuni.
"Sitacheza mechi ya jumamosi kwasababu nina kadi tatu za njano, nilipata dhidi ya Ruvu Shooting, Mgambo na juzi dhidi ya Azam fc. Lakini leo nitahudhuria mazoezi yanayofanyika chuo kikuu cha Dar es salaam". Kessy ameiambia MPENJA BLOG.
Katika mechi hizo ambazo Kessy alipata kadi tatu za njano Simba ilishinda 3-0 dhidi ya Ruvu Shooting, ikashinda 4-0 na Mgambo na juzi 2-1 dhidi ya Azam fc.
Kopunovic atalazimika kumtua mlinzi wa kulia mkongwe na nahodha wa zamani wa timu hiyo, Masoud Nassor Cholo.
Tangu asajiliwe dirisha dogo mwezi desemba mwaka jana kutoka Mtibwa Sugar, Kessy amekosa mechi tatu tu.
Alikosa mechi dhidi ya Mbeya City januari 28 mwaka huu uwanja wa Taifa kwasababu ya kadi tatu za njano, akakosa mechi mbili dhidi ya Kagera Sugar uwanja wa Kambarage, Shinyanga na Mbeya City uwanja wa Sokoine kwasababu alijiondoka kikosini akidai maslahi yake kwa uongozi wa Simba.
Simba wanahitaji ushindi jumamosi huku wakiwaombea Azam fc wafungwe kesho na Yanga halafu watoe sare mechi ya mwisho dhidi ya Mgambo ili wachukue nafasi ya pili na kuwakilisha nchi katika michuano ya kombe la Shirikisho.
Azam wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 45 baada ya kucheza mechi 24 na Simba wapo nafasi ya tatu kwa pointi 44 kufuatia kushuka dimbani mara 25.
0 comments:
Post a Comment