Singano akiwa nyumbani kwao jana
STORI
kubwa ya michezo nchini kwasasa ni sakata la mkataba wa kiungo mshambuliaji,
Ramadhan Singano ‘Messi’ na klabu yake ya Simba.
Kuna
sintofahamu kubwa kwasababu Singano anadai amemaliza mkataba, wakati Simba na
TFF wana mkataba unaoonesha ana mwaka mmoja zaidi katika mkataba wa miaka
mitatu aliosaini mei 1 mwaka 2013.
Singano
yeye anadai alisaini mkataba wa miaka miwili mei 1 mwaka 2013 na unatakiwa
kumalizika Julai 1 mwaka 2015, lakini Simba wao wanadai mkataba wake
utaisha Julai 1 mwaka 2016.
Kuna
sakala la ku-foji mkataba baina ya Singano na klabu yake ya Simba, nani kahusika?,
fuatilia sinema hii.
MAELEZO YA RAMADHANI SINGANO ‘MESSI’
Singano anasema: “Baada
ya kusaini mkataba wa miaka miwili mwaka 2013, wiki mbili baadaye nilichukua
nakala ya mkataba wangu na kwenda nayo
nyumbani.
Baada ya mwaka
kuisha tangu nisaini mkataba, nikaitwa timu ya taifa, lakini mwezi wa saba
(2013), nikapewa taarifa kwamba kuna mkataba wa miaka mitatu TFF, nikafuatilia
na kupata nakala yake na nilipoangalia nikakuta kweli kuna miaka mitatu.
Tukirudi nyuma
kidogo kwenye mkataba wa kwanza wa miaka miwili, kuna vipengele ambavyo zikutimiziwa, ikabidi
niandike barua tarehe 13 mwezi wa pili
2013 kwenda kwa uongozi (utawala wa Aden Rage) kuwaeleza kuwa kuna stahiki
zangu sijapata, lakini sikupewa majibu
yoyote, nikaendelea kufanya kazi bila kuingia
kwenye vyombo vya habari.
Baada ya uongozi
kuondoka, nikakutana na uongozi wa Rais Aveva (Aveva), nikaongea na makamu wa Rais (Geofrey Nyange Kaburu) kuhusu madai yangu,
akaniambia haina shida watalifanyia kazi.
Baada ya ligi kusimama mwezi wa 12 mwaka jana
tulikuwa tupo Gym, nikamwambia Kaburu kuhusu barua niliyoandika kudai stahiki zangu.
Alichonijibu hata mimi nilishangaa, aliniambia mchezaji mzawa huwezi kulipwa
kodi ya nyumba, nikasema hakuna shida, lakini kubwa likawa ni mkataba wa miaka
mitatu, nikamwambia, hili mbona silifahamu? Nipe ufafanuzi kwasababu mimi nina mkataba wa
miaka miwili.
Kikubwa
alichoniambia ni kwamba subiri ligi imalizike tutaongea juu ya hilo. Baada ya
ligi kuanza mzunguko wa pili ikabidi nipeleke vielelezo kwanza na nikaandika
barua kuwapa taarifa.
Niliandika barua ya kwanza mwezi wa tatu
(2015) ambayo niliwaambia kuhusu malalamiko yangu ya mkataba wa miaka mitatu
wakati mimi nina mkataba wa miaka miwili, nilimuandikia Rais Aveva.
Nikajibiwa barua ya
hiyo na katibu mkuu wa klabu (Stephen
Ally) akithibitisha kupokea barua yangu ya malalamiko na akanitaka nimpelekee nakala
ya mkataba ili alinganishe na ile waliyokabidhiwa, baada ya hapo aondoe sintofahamu iliyopo
upande wangu.
Baada ya kupokea
barua hii kutoka kwake nikaisoma na kuandika barua nyingine tarehe 31 mwezi wa
tatu 2015 na kuambatanisha nyuma nakala ya mkataba wangu na kumpekelea kama
alivyonitaka kwenye barua yake ya nyuma ambayo ilisema tutamaliza kwa muda
mfupi sintofahamu yangu, lakini wakakaa kimya mapaka leo hii tunavyoongea (jana).
Kabla ya ligi
kuisha nikaitwa tena ofsini tarehe 13 mwezi wa tano mwaka huu (jumatano),
nikaonana na makamu wa Rais Nyange Kaburu. kwanza kabla ya yote tukaongelea
mkataba, alikiri na mwenyezi mungu ni shahidi, akasema mkataba wao wa kwanza
una makosa. Alivyodai ni kwamba karatasi yao ya kwanza inaonesha ni 2015 na ya
pili 2016. Nikamwambia hilo la 2016 silifahamu, nimekuja hapa kuongelea mkataba
mpya kwasababu nimeshamaliza mkataba wangu.
Wakaleta mkataba mpya bila hata ya kujibu
barua yangu. kubwa sio kama watu wanavyofikirIa, watu wanadanganywa kwamba mimi
nina tamaa ya hela, kwanza ni kumalizana
kuhusu mkataba huu wa miaka mitatu, wakati mimi ninaujua wa miaka miwili”.
MAPUNGUFU YA MKATABA MPYA KWA MUJIBU WA MENEJA NA KAKA YAKE RAMADHANI
SINGANO, HAMIS RAMADHANI
Hamis Ramadhani
ambaye pia ni kaka yake wa damu wa Singano
(Mama mmoja, baba tofauti), anafunguka:
“Kitu anacholalamikia
Ramadhani, bila kujali kama Simba watamsajili au hapana, wala hafungi milango kwa Simba ni mkataba. Simba
wanatakiwa watambue kwamba, mkataba mpya walioleta una mapungufu mengi.
Kwa mfano Simba wanasema
Ramadhani ana miaka mitatu, lakini mkataba huu mpya unasema utaanza tarehe 1
mwezi wa sita 2015. Kama kweli Ramadhani
ana mkataba wa miaka mitatu basi unatakiwa kuisha mwakani (2016). Sasa inakuwaje kama mkataba wa kwanza unaisha
mwakani (2016), mkataba mpya uanze tena mwezi wa sita mwaka huu (2016) na
kumalizika 2017?
Mkataba huu mpya
unaonesha ni wa miaka miwili na utaisha mwaka 2017. kama kweli Ramadhani ana mkataba wa mwaka
mmoja zaidi na Simba, mkataba mpya wa miaka miwili utaishaje mwaka 2017 badala
ya 2018?
Yaani kama bado ana
mkataba wa mwaka mmoja na Simba, sahizi
akaongeza mkataba wa miaka miwili, basi mkataba wake wote utaisha mwaka 2018 na
si 2017.
Chapili ; kuna kipengele
ambacho kinaonesha jinsi gani mchezaji atakavyokuwa katika timu na kocha
atavyokuwa na mapendekezo juu maslahi yake. Hili pia tumeona ni tatizo kwa Ramadhani.
Yeye kama mchezaji anatakiwa kujua kwamba Simba watakapokuja kukatisha mkataba
wake, maslahi yake yako vipi?.
Simba wanasema
mchezaji atakapokatishwa mkataba atalipwa kwa kipindi cha mwezi mmoja, swali
linakuja, mwezi mmoja atalipwa kiasi gani cha fedha?. Ukishaisha msimu wa kwanza, anabakisha mwaka mzima, eti unakuja kumlipa
mshahara wa mwezi mmoja mtu aliyebakiza miezi 12, inakuwaje hapo?
Pia kuna kipengele
kingine ambacho kinaonesha kwamba kina mapungufu katika mkataba huu, hasa
sehemu ya kuvunja mkataba.
Wakati mchezaji
atalipwa mshahara wa mwezi mmoja tu akivunjiwa mkataba na klabu, yeye akivunja
mkataba na klabu anatakiwa kulipa dola laki sita. Yaani klabu ikivunja mkataba
wa mchezaji, analipwa mshahara wa mwezi mmoja, lakini mchezaji akivunja mkataba
na klabu, yeye anatakiwa kulipa dola laki sita. Kipengele hiki tumeona ni kigumu kwa Ramadhani
kusaini mkataba huu mpya.
Lakini kwanza tunataka kujua mkataba wa kwanza wa
miaka miwili una mapungufu gani ili tuyaweke
sawa, tuangalie stahiki zake zipoje na amelipwa au hajalipwa?
JICHO LA TATU LA MTANDAO HUU
Ukisoma maelezo ya Ramadhani Singano na
Meneja wake Hamis Said kuna mkanganyiko wa wazi unaonekana na kuna mtu ame-foji
mkataba.
Uchunguzi uliofanywa na mtandao huu umebaini
kuwa mkataba wa miaka miwili aliosaini Singano ulianza mei 1 mwaka 2013 na
unatakiwa kumalizika Julai 1, 2015,
lakini ukiwa na kipengele cha kuongeza kutegemeana na namna Simba watavyomuona
mchezaji.
Katika mkataba huo wa miaka miwili, kuna
stahiki ambazo Singano hajapata mpaka umemalizika kisheria. Kwa mfano kipengele
kimoja cha mkataba kinasema mchezaji atapewa shilingi laki sita (600,000) ikiwa
pango la nyumba ‘House Allowance’ , lakini haijaelezwa kama itatolewa kwa mwezi
au mwaka.
Hata
hivyo Singano hajawahi kupewa pesa hiyo mpaka mkataba wake unaisha. Kumbuka
katika maelezo yake alisema kwamba alimwambia Kaburu kuhusu hilo, lakini
alimjibu kuwa mchezaji mzawa hawezi kupewa kodi ya nyumbani. Kama ni hivyo kwanini kipengele hicho kiwepo
kwenye mkataba?
Ukiachana na hilo, mkataba wa miaka miwili wa
Singano unaeleza kuwa; kama mchezaji
ataitwa mara nyingi timu ya Taifa ataongezewa 25% ya mshahara na imefafanuliwa
kuwa klabu itaanza kumtathimini mchezaji miezi sita tokeo asaini mkataba.
Ukiangalia toka Singano asaini mkataba 1/5/2013
ameitwa mara nyingi timu ya Taifa, lakini anasema mashahara wake haujawahi
kupanda kwa 25%. Kiufupi kuna mapungufu mengi katika mkataba huo na mchezaji
hajapata baadhi ya stahiki zake muhimu.
TURUDI KWENYE UTATA WA
MKATABA WA MIAKA MIWILI NA MKATABA WA MIAKA MITATU
Singano baada ya kusaini mkataba wa miaka
miwili 2015, inatakiwa tarehe 1/7/2015 umalizike, lakini kikanuni mpaka sasa ni
mchezaji huru kwasababu FIFA wanasema mchezaji akibakiza miezi sita kwenye
mkataba wake anaruhusiwa kuongea na timu nyingine.
Utata mkubwa unaonekana katika mkataba wa miaka mitatu
uliopo Simba na TFF. Singano amefafanua vizuri kwamba alienda TFF kufuatilia
baada ya kuambiwa kuna mkataba wa miaka mitatu. Kweli akapewa nakala yake na
uchunguzi wetu umebaini kuwa mkataba huo wa miaka mitatu unaonesha ulisainiwa
siku moja na mkataba wa miaka miwili alionao Singano.
Nimesema hapo juu, mkataba wa miaka miwili
ambao Singano anadai ni sahihi ulisainiwa 1/5/2013 na unaisha 1/7/2015. Mkataba
wa miaka mitatu walionao Simba na TFF ulisainiwa 1/5/2013 na utaisha 1/7/2016.
Mikataba yote miwili inaonesha sahihi ya Singano na
kiongozi mmoja wa Simba. Vipengele vya mikataba hiyo miwili vinafanana kabisa,
utofauti ni idadi ya miaka? Swali ni je, huu mkataba wa miaka mitatu uliopo
Simba na TFF umeandikwa na nani? Je, Simba wamefoji? Au Singano amefoji? Hapo ndipo
utata upo na lazima upatikane kwenye vyombo vya sheria.
MALALAMIKO YA SINGANO KUTOTIMIZIWA STAHIKI ZAKE KATIKA MKATABA WA
MIAKA MIWILI
Mtandao huu umebaini kuwa mkataba wa miaka
miwili aliosaini Singano una mapungufu
mengi na ni dhahiri mchezaji hajatimiziwa stahiki zake kwa mujibu wa
mkataba huo.
Mchezaji hakukaa kimya kudai haki zake kwani februari 13, 2014
aliandika barua kwenda kwa katibu mkuu wa Simba, akieleza kwamba ni zaidi ya
nusu mwaka tangu aingie mkataba na klabu hiyo, lakini hajatimiziwa haki zake za
kimsingi zilizoainishwa kwenye mkataba. Kuna
mambo ya msingi alieleza mfano kadi ya Bima ambayo aliahidiwa kupewa kabla ya
kuanza kazi. Pia kodi ya nyumba ambayo hakupatiwa tangu wakubaliane , lakini cha
kushangaza hakujibiwa barua hiyo.
Lilipofika suala la mkataba wa miaka mitatu ambao
Singano hautambui, alichukua hatua za haraka kufuatilia na akapewa nakala ya
mkataba huo na TFF.
Machi 10 mwaka 2015 mtandao huu umegundua
kuwa Singano aliandika barua kwenda kwa Rais Evans Aveva akitaka ufafanuzi juu
ya mkataba wa miaka mitatu uliowasilishwa TFF. Singano alifafanua katika barua
yake kuwa mkakaba huo wa miaka mitatu hajausaini na ameshindwa kujua tafsiri
halisi ya kitendo hicho.
Katibu
mkuu wa Simba, Stephen Ally alimjibu Singano kwa barua ya Tarehe
13-3-2015, KUM: SSC/12/03/2015/KM . Kikubwa katibu mkuu huyo alithibitisha
kupokea barua yake ya malalamiko kwa Rais Aveva kuhusu ualakini kwenye mkataba
uliopelekwa TFF na ule ambao alisaini.
Ally alimwambia Singano kwamba suala hilo
lilipelekwa kwake kwa ajili ya utekelezaji na akamfahamisha kuwa wakati uongozi
mpya unaingia madarakani ulikabidhiwa nyaraka zote za klabu ikiwemo mkataba wa
Singano.
Katibu mkuu akasema kinyume na madai ya
Singano, mkataba wake waliokabidhiwa ni ule unaoonesha amesaini kuitumikia Simba
kwa muda wa miaka mitatu, lakini Singano alikuwa na mkataba wa miaka miwili, Ally akamtaka kuwasilisha nakala ya mkataba
huo ili wamalize mapema tatizo lake.
Haraka sana Singano alikaa chini na
kuandika barua machi 31, 2014 akijibu barua ya katibu mkuu, Stephen Ally ya
tarehe 13/3/2015 yenye KUM: SSC/12/02/2015/KM ambayo ilimtaka kuwasilisha
nakala ya mkataba wake na klabu ya Simba.
Katika
barua yake Singano aliambatanisha mkataba wa miaka miwili anaoutambua
akitarajia kupata ufumbuzi, lakini tofauti na matarajio yake, hakupata majibu
mpaka jana alipokuwa anaongea na mtandao huu.
Cha kushangaza jana hiyo hiyo amepokea
barua kutoka Simba yenye KUM 18/05/2015/RL/05 iliyoandikwa na Rais Aveva tarehe
18/05/2015. Barua hiyo ambayo Singano amepokea ni majibu ya barua yake ya
31/03/2015 aliyotuma pamoja na nakala ya mkataba wake wa miaka miwili.
Rais Aveva katika barua hiyo amemueleza
Singano kwamba kwa mujibu wa kumbukumbu za klabu pamoja na nakala ya mkataba
uliowasilishwa TFF, mkataba wake na klabu ya Simba utamalizika tarehe 1 julai
2016. Hii ni tofauti na nakala ya mkataba aliyoambatanisha Singano kwenye barua
yake inayoonesha mkataba wake unaisha Julai mosi, 2015.
BOMU LINGINE KATIKA SAKATA HILO LA MKATABA
Wakati hayo yote yakiendelea,
mtandao huu umegundua kuwa klabu ya Kuhnsdorf-Klopeiner See ya Austria ilituma
mwaliko Simba ikiomba Ramadhani Singano akafanye majaribio. Barua hiyo ya
mwaliko iliandikwa 29.04.2015
Kuhnsdorf katika
mwaliko wao walisema majaribio hayo yataanza mei 15, 2015 mpaka angalau juni 30
mwaka huu. Walifafanua kuwa gharama za usafiri wa ndege na kuishi kule, matibabu
yote watagharamikia wao wenyewe na wakatumaini kwamba mpaka mei 15 mwaka huu
Singano atakuwa amewasili klabuni kwao.
Katibu mkuu wa Simba,
Stephen Ally baada ya kupokea barua hiyo ya mwaliko aliandika barua yenye KUMB:
SSC/22/2015/05/GS kwenda ubalozi wa Austria Tanzania akieleza kupokea maombi ya
klabu ya SK Kuhnsdorf kumtaka Singano akafanye majaribio kwao.
Simba katika barua yao hiyo
walieleza kuwa Ramadhan Singano ana mkataba na amealikwa kwenda kufanya majaribio
katika klabu hiyo iliyopo maeneo ya Viebba, Austria, hivyo wanauomba ubalozi wa nchi hiyo
hapa Tanzania kumruhusu kusafiri kwenda nchini mwao.
UTATA MWINGINE HUU HAPA…….
Simba katika barua
waliyoandika kwenda ubalozi wa Austria inaeleza kwamba Singano ana mkataba
ambao ndio ule wa miaka mitatu unaoisha 2016, lakini ukiangalia kwa jicho
lingine, mei 12 mwaka huu 2015, siku mbili kabla ya mchezaji kwenda Austria kufanya majaribio, walitengeneza mkataba mpya
na kumtaka Singano asaini haraka.
Kwa maana hiyo wakati
anakwenda Austria walitaka awe na mkataba wa miaka miwili. Katika maelezo ya
mkataba huo mpya wa miaka miwili, Simba wameeleza kuwa utaanza rasmi Juni 1
mwaka huu hadi mei 30 mwaka 2017, lakini kuna kipengele cha kuongeza kutegemea
na muelekeo wa klabu.
Swali linalotatiza ni
kwamba, kama kweli Singano bado amebakiza mkataba wa mwaka mmoja, kwanini Simba
walimharakisha kusaini mwingine kabla ya kwenda Austria? Ingawa kisheria unaruhusiwa
kuongeza mkataba wakati wowote.
Hata angeenda bila
kusaini mkataba mpya, bado klabu ya SK
Kuhnsdorf ingelazimika kuzungumza na Simba ili imsajili kwasababu ana mkataba
wa mwaka mmoja zaidi kama wanavyodai.
Kumbuka mkataba wa
miaka miwili anaoujua Singano unatakiwa kuisha kabisa 1/7/2015, lakini kikanuni
umeshaisha na mchezaji yuko huru. Maana yake kama Singano angeenda Austria na
kufuzu majaribio angesajiliwa bure kabisa, Simba wasingepata chochote.
Kwa mazingira haya,
unashawishika kusema Simba walijua Singano amemaliza mkataba, hivyo wakalazimika
kumtengeneza mkataba mpya haraka ili akienda Austria na kufuzu, wafaidike na
biashara hiyo.
Nani aliyefoji mkataba
kati ya Singano na Simba?
Endelea kusoma mtandao
huu…yapo mengi kuhusu sinema hii…kesho tutakuletea majibu ya Simba kuhusu sakata hili.
0 comments:
Post a Comment