Vijana wakiandaliwa kuwa mastaa wa badaye, lakini mazingira wanayoandaliwa ni bonge la tatizo
Timu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 12 Jinu Star ya
Mtoni Mtongani, Manispaa ya Temeke imeomba kusaidiwa vifaa vya michezo ili
iweze kusonga mbele katika juhudi zake za kuinua soka la vijana nchini ambao
watakuja kucheza kwenye ngazi za vilabu na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ muda
mfupi ujao.
Kocha wa timu hiyo Charles Beka amesema, timu hiyo
ina upungufu wa vifaa vya michezo ikiwemo mipira, viatu pamoja na jezi mbavyo
ndio changamoto kubwa kwenye timu hiyo.
“Mimi unavyoniona hapa ndio kocha wa timu hii, katibu,
mwenyekiti na kila kitu hapa, sina msaidizi na mimi ndiyo nashughulika na
kilakitu kwenye timu hii. Kwenye timu yetu tunashindwa kufanya mambo mengi ili
kufikia malengo kwasababu ya upungufu wa vifaa”, amesema Beka.
“Mipira tuliyonayo ni mitano tu, tena mibovu lakini ndiyo
tunaitumia hiyohiyo kwenye mazoezi kitu ambacho kinatupa wakati mgumu. Wakati
tunajifunza ufundi wa mpira (kuchezea mpira) tunahitaji angalau mpira mmoja
utumiwe na wachezaji wawili japo kiuhalisia inatakiwa kila mchezaji awe na
mpira wake”, ameongeza Beka.
“Changamoto nyingine ni ushirikiano duni toka kwa wazazi
japo sio wote, baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwazuia watoto wao kuja kufanya
mazoezi lakini wakati mwingine tumekuwa tukiwaomba michango kwa ajili ya
kutengenezea mipira inapoharibika au pesa ya nauli tunapohitaji kusafiri kwenda
kucheza mechi za kirafiki, wazazi wengine wamekuwa wagumu kujitolea. Timu haina
mdhamini kwahiyo tunapata changamoto kubwa”, Beka alisisitiza.
Kocha huyo wa kujitolea ametoa wito kwa Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) kuangalia timu za mtaani ambazo zinafundisha soka kwa
vijana ili kushirikiana kwa pamoja katika kutatua changamoto zinazowakabili na
kuwajumuisha wachezaji wenye vipaji kwenye timu za Taifa za vijana.
0 comments:
Post a Comment