BAADA ya kuwapoteza wachezaji wake nyota, Deus Kaseke na Peter Mwalyanzi, Mbeya City fc wameanza kuangalia uwezekano wa kuinasa saini ya mshambuliaji wa Stand United, Mnigeria, Abasalim Chidiebele.
Mwishoni mwa juma lililopita, Kaseke alisaini mkataba wa miaka miwili Yanga, wakati Mwalyanzi naye alisaini mkataba kama huo katika klabu ya Simba.
Chidiebele ameiambia MPENJA BLOG jioni kuwa amemaliza mkataba na Stand United, hivyo anasubiri ofa kutoka timu nyingine.
Mnigeria huyo amesema kwamba kwasasa hajakaa mezani na timu yoyote, lakini klabu za Mbeya City, Coastal Union na Kagera Sugar zimeshampigia simu kuhitaji ofa yake.
"Mkataba wangu na Stand United umekwisha, mimi ni mchezaji huru. Timu zinanipigia simu, lakini sijapata ofa yoyote. Stand wameniambia nisubiri, ila mimi nasubiri ofa nzuri kutoka timu yoyote". Chidiebele amesema na kuongeza: "Kagera Sugar, Coastal Union na Mbeya City wamenipigia simu ingawa hawajazungumza lolote zaidi ya kuniambia wanahitaji ofa yangu".
Mshambuliaji huyo aliyefunga magoli 11 msimu wa ligi kuu Tanzania bara 2014/2015 uliomalizika mei 9 mwaka huu amesema anahangaikia mambo yake mwenyewe kwasababu meneja wake yuko Dubai.
"Sio weledi kujihangaikia mwenye, lakini mtu anayenisimamia (meneja) ni mwanasheria na amepata dharura, yuko Dubai".
Hata hivyo, mfumania nyavu huyo aliyewafunga Simba Kambarage, Shinyanga, amekiri kuwa hawezi kuendelea kuwasubiri Stand kwasababu wana mambo ya 'kiswahili'.
"Unajua Stand ni timu ya kiswahili, siwezi kuwasubiri, wanafanya mambo yao pole pole sana. Mimi nikipata ofa sasa hivi naondoka zangu haraka". Amefafanua na kusisitiza: Niliichezea Stand United toka ligi daraja la kwanza, hawajui namna ya kuishi na mchezaji wa kimataifa, hawajajipanga".
"Najua namna timu kubwa zinavyoishi na wachezaji wa kimataifa, Stand United hawajafikia hatua nzuri, sina furaha. Kwasasa sitaki kucheza timu yenye uswahili, nahitaji timu nzuri itayonilipa kwa muda mshahara, posho, nauli ya kurudi nyumbani Nigeria na kurudi Tanzania pamoja na familia yangu".
"Unajua mimi sio Mtanzania, ligi imeisha sasa hivi, natakiwa kurudi Nigeria na familia yangu, lakini nipo hapa Mwanza na familia yangu, Stand hawajui namna ya kuishi na wachezaji wa kimataifa".
0 comments:
Post a Comment