Luhende (kulia) akichuana na kiungo wa Yanga Haruna Niyonzima kwenye moja ya mechi ya Wanajangwani dhidi ya Mtibwa Sugar msimu uliopita.
MLINZI wa kushoto wa Mtibwa Sugar, David Charles Luhende amekanusha taarifa za kutafutwa na Yanga kama alivyoripotiwa siku za nyuma na baadhi ya vyombo vya habari.
Ilielezwa kuwa kocha mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm anavutiwa na uwezo wa Luhende na aliomba asajiliwe, lakini beki huyo amedai ni maneno ya watu tu.
Yanga jana ilisajili mlinzi wa kushoto kutoka KMKM ya Zanzibar, Mwinyi Hajji na kufikisha idadi ya walinzi watatu wa kushoto kwasababu tayari ilikuwa nao wawili, Oscar Joshua na Edward Charles.
Usajili wa Mwinyi inaweza kuwa dalili ya Luhende kutohitaji tena Yanga.
Hata hivyo, mlinzi huyo wa kushoto wa zamani wa Yanga na Kagera Sugar ameweka wazi kuwa yeye ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na Mtibwa Sugar.
"Nimeshamaliza mkataba na Mtibwa,wameonesha nia ya kuendelea na mimi, lakini bado sijaongea nao". Luhende ameiambia MPENJA BLOG alasiri hii na kuongeza: "Ikitokea timu nyingine, niko tayari kwenda kusaini kama tukikubaliana. Mpira ni kazi yangu, siwezi kuwasubiri Mtibwa wakati kuna watu wananihitaji".
Kuhusu tetesi za kutakiwa na Yanga, Luhende amesema: "Kwasasa hakuna timu iliyonifuata, nipo tu nyumbani. Tetesi za kuhitajika Yanga ni maneno ya watu tu, bado hakuna timu iliyokuja kwangu. Yanga wakinihitaji naenda, mpira kazi yangu"
0 comments:
Post a Comment