Hawa sio vijana wa mitaani, ni timu ya Taifa
TIMU ya Taifa ya masumbwi inayojiandaa
kwa ajili ya michuano ya ‘All African Games’ na michuano mingine ya klabu
bingwa ya Taifa inaendelea na mazoezi yake kwenye viwanja vya nje ya uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam.
Kitu cha kusikitisha ni mazingira
ambayo timu hiyo inajiandaa, wachezaji wanafanya mazoezi chini ya mti eneo
ambalo pia halina sakafu (kwenye mavumbi), pia eneo hilo ni la wazi kitu ambacho ni
hatari kwa afya zao.
Kocha wa timu hiyo Jonas Mwakipesile
amesema anasikitishwa na hali hiyo na kuongeza kuwa inakatisha sana tamaa
kuanzia wachezaji mpaka walimu kwa ujumla.
“Kama unavyoona mwenyewe, hawa ni
vijana wa timu ya Taifa ya masumbwi wanafanya mazoezi nje, kwenye mavumbi,
lakini wakiwa hawana vifaa vya mazoezi kama vile gloves, jezi na viatu. Kuna
gloves chache ambazo hazitoshi wachezaji wote lakini pia sio za timu, tumeazima
kwenye timu ya jeshi (JKT)”, amesema Mwakipesile.
“Timu haina kambi, kila mchezaji
anatoka kwao na hatujui kama wachezaji wanakula vizuri kama inavyotakiwa, hawapati
posho wala kifuta jasho, wanajitolea tu. Maana hawa wanajiandaa kupambana na
mabondia wengine wa Afrika, inasikitisha na inakatisha tamaa. Kwa mwendo huu
unatarajia mchezaji atakuwa na moyo wa kupambana wakati haoni ‘support’
yoyote?”, Mwakipesile alihoji.
“Lakini pale timu inapofanya vibaya
tumekuwa tukinyooshewa vidole na watanzania wote, lakini wao hawajui haya yote
yanayoendelea, laiti kama wangekuwa wanajua wangezuia hata timu isiende kwenye
mashindano”, aliongeza Mwakipesile.
“Chakushangaza timu nyingine za Taifa
zinapewa kila kitu kinachohitajika lakini hazifanyi vizuri, kwa mfano Taifa
Stars inapewa karibu kila kitu lakini bado ina matokeo mabovu. Inasafiri kwa
ndege, inawekwa kambini, inapata vifaa vya michezo lakini hatujaona matokeo
mazuri,” amesema.
Kocha huyo amesema kuwa, wamejaribu
kuomba kutumia eneo la uwanja wa Taifa lenye sakafu lakini wakaambiwa wakaombe
kwenye wizara husika maana ndiyo yenye dhamana ya uwanja huo.
Kocha Jonas Mwakipesile
Mwakipesile kupitia mtandao huu ameiomba serikali, wapenzi na wadau wa
mchezo wa masumbwi kuangalia uwezekano wa kuboresha mazingira ya kikosi hicho
na sio kusubiri kutoa lawama pale timu inapofanya vibaya kwenye mashindano.
Timu hiyo inatarajia kwenda kucheza
michezo ya kirafiki nchini Zambia kwa ajili ya kujipima kabla haijasafiri
kuelekea nchini Congo Brazzaville ambako michuano hiyo itafanyikia.
0 comments:
Post a Comment