Na Oswald Ngonyani.
Baada ya timu zote za England zilizokuwa zinashiriki michuano
ya Klabu bingwa Ulaya (UEFA) kufungashiwa virago, vita ya vilabu hivyo kwa sasa
imehamia katika Ligi kuu ya nchini humo EPL 2014/2015 huku nafasi ya timu nne
bora ikionekana kuwa na changamoto kubwa zaidi.
Vijana wa Jose Mourinho wao wangali kileleni baada ya kucheza
mechi 31 huku wakiwa na hazina ya pointi 73 kibindoni pointi saba zaidi ya
Arsenal wanaoshika nafasi ya pili huku ‘The Blues’ wakiwa na faida ya mchezo
mmoja zaidi.
Aina ya michezo yote iliyobaki kwa vijana hao wa darajani
inawafanya mashabiki wengi wa kikosi hicho kuamini kuwa, kuna uwezekano mkubwa
wa kikosi chao hicho kuitwaa ndoo hiyo inayoshikiliwa na Man City kwa sasa.
Kimahesabu ya mpira timu zote hizo yaani Man City, Arsenal,
Man United na hata Liverpool zinaweza zikautwaa ubingwa huo lakini ngekewa hii
kwa kiasi kikubwa itategemea na mantiki ya kuiombea njaa klabu ya Chelsea
maarufu kwa jina la ‘The Blues’.
Utofauti wa pointi saba zaidi ya timu inayofuatia katika EPL
kwa sasa, ni hazina ya pekee kwa klabu ya Chelsea kuwa na asilimia kubwa ya
kuweza kuibuka bingwa katika mbio hizo. Kwa namna kikosi hicho kilivyopambana
msimu huu, ni haki yake Jose Mourinho kuwa kileleni kwa sasa.
Juhudi za akina Diego Costa, Cecs Fabregas, Didier Drogba na
wachezaji wengineo wengi ndizo haswa zilizoifikisha Chelsea mahali ilipo sasa.
Ni wazi kuwa Mourinho amedhamiria kuitwaa ndoo hiyo, uchezaji wa kikosi chake
ndani ya dimba ni ushahidi tosha.
Mwenendo wa doro wa klabu ya Man City nao unaweza ukawa
sababu ya kuifanya vita ya nne bora kuwa tamu zaidi kutokana na idadi ya pointi
ambazo vilabu hivyo vinatofautiana mpaka sasa.
Awali vita ya kuutwaa ubingwa wa EPL kwa msimu huu 2014/2015
ilionekana kuwa ya vilabu viwili pekee, Chelsea na Man City lakini matokeo ya
siku za karibuni ya Vijana wa Manuel Pellegrin yameifanya vita hiyo iwe kubwa,
kwani akina Arsene Wenger na Van Gaal wanaonekana kuja kwa kasi ya ajabu.
Kwa sasa vita ya EPL
imebaki kuwa ya wengi. Pamoja na Chelsea kuwa na faida ya kuwa na pointi
nyingi zaidi ya wale wanaomfuatia, ni wakati wa Mourinho kuelewa kuwa endapo
atasuasua katika michezo iliyobaki huenda akawa katika wakati mgumu kama
ilivyotokea kwa Liverpool msimu uliopita.
Siku zote mchezo wa soka ni mchezo wa mipango. Ni wazi kuwa
makocha wa vilabu hivyo wapo katika hesabu za hali ya juu, hesabu za
kuhakikisha kuwa malengo lengwa yanafikiwa kwa ukamilifu wake.
Tazama, wakati The Blues wenyewe wakiwa kileleni kwa tofauti
ya pointi 7 zaidi dhidi ya Arsenal, ‘The Gunners’ wenyewe wapo juu ya Manchester
United kwa utofauti wa pointi moja pekee huku Man United ikiizidi Man City
pointi nne.
Utofauti huu wa pointi huenda ukaamua chochote mbele ya
safari. Kuna uwezekano mkubwa wa hali yoyote kutokea na hata mkubwa mmoja
akaporomoshwa katika mpambano huo wa nne bora, hii itategemeana na umaridadi wa
vikosi vya Liverpool, Southampton, na Spurs.
Wakati mwenendo ulio bora wa Majogoo wa Jiji, Klabu ya
Liverpool ukipunguzwa kasi pale wiki
jana na Arsenal, Klabu ya Spurs yenyewe tayari imekwishajikusanyia pointi 56,
pointi 1 nyuma ya Liverpool.
Ni kama kusema utofauti wa pointi nne uliopo baina ya Man City
dhidi ya Liverpool unaweza ukasababisha chochote mbele ya safari, kwani hesabu
za soka zinaweza zikabadilika muda wowote na hata kuwafanya wadau wengi wa soka
kubaki na labda.
Mpambano huo wa kugombea namba nne za juu ni mpambano unaoonekana
kuwapa shauku kubwa zaidi wanazi wa mchezo wa soka duniani kote ambao siku zote
wameonekana kumakinika mno na EPL.

Hii ndiyo maana michezo iliyobaki imeonekana kusubirishiwa
kwa marefu na mapana yake huku mchezo wa kesho baina ya Chelsea watakaowaalika
Manchester United ukionekana kupewa uzito zaidi na hata wadau wengi
kuisubirishia tamati ya mchezo huo ili kuona kama ‘Mashetani wekundu’ wataweza
kuibuka kidedea au Vijana wa Chelsea wataendeleza rekodi ya ubora wao katika
siku za karibuni.
Ni imani yangu vita hii ya kuwania nafasi nne za juu katika
EPL msimu huu itatimilika kwa mapana yake na hata kutoa nafasi kwa Makocha
ambao walikuwa na mipango ya muda mrefu, mipango yenye tija yenye kuendana na matumaini chanya ya
mashabiki wa vilabu hivyo.
Bila shaka kocha mbwatukaji Jose Mourinho hatakuwa tayari
kuona timu yake ikiukosa ubingwa huo kizembe. Hapana shaka Manuel Pellegrin wa
Man City atakuwa na furaha zaidi iwapo jeshi lake litafanikiwa kuutetea ubingwa
huo.
Vivyo hivyo kwa Arsene Wenger na Van Gaal, ni wazi kuwa wana
hamu kubwa ya kuitwaa ndoo hiyo ili kujenga imani kwa mashabiki wao ambao
wanaonekana kuwa na imani hasi kwa makocha wao hao. Brendan Rodgers na
Liverpool yake naye pia ana kazi ya ziada kuwaaminisha mashabiki wake kuwa
hakubahatisha katika msimu uliopita.
Ni vita ya ndani ya dimba itakayoamriwa na dakika tisini za
waamuzi wa kila mechi.
Mimi yangu Macho…….
(Mwandishi wa Makala
haya ni msomaji wa blog hii, lakini pia ni Mwandishi wa Makala za uchambuzi
katika Gazeti la Dimba anapatikana kwa simu namba 0767 57 32 87 au kwa barua
pepe [email protected])


0 comments:
Post a Comment