Na Shaffih Dauda
MABINGWA watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara Azam fc wamejiweka katika mazingira magumu ya kutetea taji lao na hata nafasi ya pili msimu huu baada ya kutoka sare katika mechi tatu mfululizo.
Katikati ya juma lililopita, Azam walitoka sare ya 1-1 dhidi ya Mbeya City uwanja wa Azam Complex, kabla ya kusafiri kwenda Manungu walikotoka sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar na hatimaye hapo jana wakatoka suluhu (0-0) na Mgambo JKT uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga.
Kwa matokeo hayo, Azam wamefikisha pointi 39 baada ya kucheza mechi 21 na sasa wanazidiwa pointi 7 na Yanga wenye alama 46 kileleni kufuatia kucheza mechi 21.
Azam wamebakiza mechi tano ambazo ni dhidi ya Kagera Sugar, Yanga, Simba, Stand United na Mgambo JKT.
Katika mechi mbili za Simba na Yanga watacheza uwanja wa Taifa ambao Azam wanamekuwa wakipata wakati mgumu kupata ushindi.
Vinara Yanga achilia mbali mechi dhidi ya Azam fc, wamebakiza mechi dhidi ya Ndanda fc, hii ni mechi pekee ambayo watacheza nje ya Dar es salaam. Mechi nyingine ni tatu ambazo ni dhidi ya Polisi Moro, Ruvu Shooting na Stand United.
Azam wametoa sare tatu mfululizo na jiulize kama wachezaji wake watatu wangekuwepo, wangepata sare dhidi ya Mbeya City fc?
Namzungumzia Aggrey Morris kwenye safu ya ulinzi, Kipre Tchetche na Didier Kavumbagu safu ya ushambuliaje kwenye sare ya 1-1 dhidi ya ‘Wagonga nyundo wa Mbeya’ Mbeya City.
Baada ya mechi hiyo Azam walitoka 1-1 na Mtibwa Sugar na jana wametoka suluhu na Mgambo JKT kama nilivyosema mwanzoni mwa makala hii.
Pointi ni kwamba wachezaji watatu, Aggrey Morris, Kipre Tchetche na Said Morad walifungiwa mechi nne na uongozi kwasababu walitoka kambini bila kuaga au bila ridhaa ya viongozi.
Huu ni uamuzi ninaoamini walichukua kisu au mkuki wa moto na kujichoma wao wenyewe.
Ikumbukwe kwamba miongoni mwa watu waliofariki kwenye ajali ya wanachama wa Simba wa tawi la Mpira na Maendelea maarufu kwa jina la Simba Ukawa, ni mjomba wake Said Morad.
Kwa mazingira hayo, Morad aliomba ruhusa ya kwenda kwenye msiba, lakini hakurejea mapema na ulikuwa kama mgomo baridi kwasababu mkataba wake unakwisha mwishoni mwa msimu.
Morad amekuwa akiwaambia viongozi wazungumze mstakabli mpya kwa maana ya kuongezewa mkataba, lakini uongozi hautoi ushirikiano.
Kwa maana hiyo Morad akawa kwenye mgomo baridi na kuchelewa kurudi kambini, matokeo yake akaadhibiwa kwa kufungiwa mechi nne sawa na wenzake.
Ukirudi kwenye uhalisia, ukubali ukatae, kwa muda mrefu muanganiko wa safu ya ulinzi wa kati wa Azam fc ni Aggrey Morris na Said Morad. Alipokuja Paschal Wawa ukatengenezwa muunganiko wa Aggrey na Wawa.
Wakati mwingine wanacheza Wawa na Morad, wakati mwingine Morris na Morad, lakini kwa maana ya kutengeneza mabeki wanne wa kati kuna mwingine chaguo la nne, David Mwantika.
Unapopanga safu ya mabeki wa kati wanne wa Azam, wa kwanza ni Wawa, chaguo la pili na Aggrey Morris, chaguo la tatu ni Said Morad na chaguo la nne ni John Mantika.
Baada ya Morris na Morad kufungiwa ikabidi waende kwa Mwantika kwenye mechi ya Mbeya City, alicheza na kumaliza mechi.

Tchetche amesimamishwa
Tchetche amesimamishwa
Lakini kwenye mechi hiyo hiyo ya Mbeya City walikuwa wamemsimamisha Kipre Tchetche, halafu Kavumbagu alikuwa na kadi tatu za njano na hakucheza hiyo mechi, hivyo idara ya ushambuliaji akabaki Gaudence Mwaikimbi na John Bocco.
Kama angekuwepo Tchetche, Azam wasingetoka sare hizo mechi tatu, mimi naamini Kipre pamoja na mapungufu yake, amekuwa na mchango mkubwa kwenye timu.
Kukosekana kwa Aggrey, Tchetche na Kavumbagu dhahiri kuliwafanya watoe sare dhidi ya Mbeya City na mapungufu yalionekana mengi.
Walipoenda kwa Mtibwa Sugar, wachezaji waliofungiwa hawakwenda kabisa Manungu, walibaki kula bata Dar es salaam na ndipo Mwantika akacheza tena na Wawa, halafu akaumia na kukawa hakuna beki mwingine wa kuchukua nafasi yake, wakamuingiza bwana mdogo mmoja ambaye aliumia pia.
Mwantika aliumia kwasababu hayuko fiti kutokana na kutocheza mechi msimu huu, baada ya beki huyu wa zamani wa Tanzania Prisons kutoka wakalazimisha Erasto Nyoni aingie ndani kucheze na Wawa.
Kule mbele alicheza John Bocco na Kavumbagu, lakini Bocco aliumia na hakukuwa na mtu mwingine. Kama angekuwepo Kipre kwenye mechi hiyo na Mtibwa, Azam walikuwa na nafasi kubwa ya kupata matokeo.
Wakaenda mechi ya tatu Tanga jana, alisimama Mwaikimba kuongoza mashambulizi, kumbe ni kweli kwamba Simba ikizidiwa hula majani. Hata Chelsea kwa mfumo wao wanaosimamisha mshambuliaji mmoja katikati, mshambuliaji chaguo namba moja ni Diego Costa, wa pili Loic Remy na chaguo la tatu ni Didier Drogba. Walilazimika kumtumia Drogba mechi ya juzi dhidi ya Queens Park Rangers kwasababu Costa na Remy walikuwa wanaumwa.
Ni sawasawa na Azam walivyomtumia Mwaikimba dhidi ya Mgambo kwasababu John Bocco anaumwa, Kipre Tchetche wamemfungia.
Kwa kawaida mfumo wa Azam wanachezesha washambuliaji wawili, Kavumbagu ikabidi achezea na Mwaikimba na walichemsha vibaya sana..
Katika mechi zote ambazo Kavumbagu amecheza, mechi ya jana alionekana ‘boya’ na mpaka akatolewa. Lakini ni kwasababu hakuwa na mtu wa kucheza naye, Mwaikimbi yako polepole, hana mwendo, hana kasi, yaani ukweli ni kwamba kazeeka.
Lakini kuna maswali, kwanini Azam wahangaike hivyo wakati Tchetche, Aggrey Morris wote ni wazima? Pamoja na kutoka suluhu na Mgambo, kulikuwa na makosa mengi mno yaliyosababishwa na safu ya ulinzi ya Azam.
Kama uliangalia mpira jana, Mwamuzi aliwasaidia Azam kwasababu mchezaji wa Mgambo alipiga krosi na jamaa akafunga, lakini mwamuzi akapuliza kipyenga kumaliza mechi.
Safu ya ulinzi ilitikisika sana kwa pengo la Aggrey Morris na safu ya ushambuliaji imekuwa dhoofu kwa kukosekana Tchetche.
Unajiuliza kitu, kulikuwa na ulazima gani wa kuwasimamisha wachezaji hao kwa makosa waliyofanya wakati wako fiti kucheza?
Kwanini wasingetafuta njia nyingine mbadala ya adhabu wakati huo huo wanaendelea kucheza kuisaidia timu?
Majukumu yao mama ni kucheza mpira na adhabu za wacheza mpira tunaziju, kuna namna ya kawaadhibu wakifanya makosa na si kuwasimamisha mechi.
Adhabu zinazotumika ni kumkata mshahara, kumnyima malupulupu ‘bonasi’. Hizo ndizo adhabu zinazotumik. Kwa bahati mbaya uongozi wa juu wa Azam uliingilia kutoa adhabu kitu ambacho si sahihi.
Kama mchezaji amekosea, anayewajibika kumpa adhabu ni kocha. Mchezaji anaripoti kwa kocha, kwahiyo George Best Nsimbe na benchi zima la ufundi walitakiwa kusema adhabu waliyotakiwa kupewa.
Lakini kutokana na muundo wa uongozi wa klabu zetu, benchi la ufundi kazi yao ni kufundisha tu na hawana nafasi ya kutoa maamuzi juu ya wachezaji wao. Kwa kawaida makocha ndio wanatakiwa kuamua wanamkata mshahara kiasi gani au wanampa adhabu ya kumnyima bonasi.
Kwa kifupi Azam katika mechi hizi tatu inaonekana wamejitoa katika mbio za kutetea ubingwa kwa wao wenyewe kujimaliza.
Wamejichoma kisu cha moyo, wamejiua, sawa na mtu aliyekunywa sumu mwenywe na kujiua.
Watu wanasema wachezaji wana majeruhi, hapana! Hawana majeruhi, ni wazima na wamesimamishwa na uongozi kwa kosa la kutoroka kambini bila taarifa na kuamua kuwafungia mechi nne na hicho ndicho kinawagharimu wao wenyewe.
Azam wamejiondoa kwenye mbio za kuwania ubingwa, halafu wamejihatarishia nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa kwasababu wanawazidi Simba pointi moja halafu wachezaji wamesimamishwa mechi nne.
Wachezaji waliofungiwa mechi nne sasa watakosa mechi ya nne dhidi ya Kagera Sugar itayopigwa jumamosi uwanja wa Azam Complex, hiyo mechi wanaweza kutoa sare tena au kufungwa na kutengeneza nafasi kwa Simba kuchukua nafasi ya pili ambayo ipo kwenye mikono yao kwasasa.
Nawashauri Azam fc, wawarejeshe wachezaji kundini ili kutetea angalau nafasi ya pili kama si kutetea ubingwa wao.
Hata Coastal Union walipocheza na Yanga na kufungwa 8-0 walifanya boko kama hilo. Waliwasimamisha wachezaji wengi muhimu wakiwemo, Shaban Kado, Joseph Mahundi, Tumba Swed, Kibacha na wengineo, lakini wakaja kujiuliza kwenye mechi iliyofuata na JKT Ruvu, wakawarudisha wachezaji wote na kupata ushindi wa magoli 2-0.
Kutokana na hali iliyopo, si dhambi kwa viongozi kulegeza kamba kwa faida ya timu, wawarejeshe kundini au wawaponye kwasababu wameshatangaza kuwa ni majeruhi, waseme tena wamepona na warudi uwanjani kucheza mechi zilizobaki.


0 comments:
Post a Comment