
Leo watashingilia kama hivi?
MABINGWA mara 24 wa Tanzania, Dar Young Africans
wanashuka dimba la Taifa leo kucheza mechi ya kwanza ya raundi ya awali ya
kombe la Shirikisho dhidi ya klabu ya jeshi ya BDF XI ya Botswana.
Hii ni mechi muhimu kwa Yanga kama wanataka
kusonga mbele hatua inayofuata.
Waswahili husema ‘Mcheza kwao hutunzwa”. Uwanja wa
nyumbani ni sehemu pekee ya kutengeneza matokeo ingawa kwa mpira wa kisayansi
tulionao sasa, Mgeni anaweza kukufunga hata ukiwa nyumbani kwako.
Hata tunaposhuhudia michuano mikubwa kama UEFA,
timu za ulaya zinajitahidi kutumia vizuri nafasi ya nyumbani kupata matokeo,
ingawa nyingine hufungwa nyumbani na ugenini.
Uwanja wenu, mashabiki wenu, wanalala kwenu,
wanakula vyakula vyenu, kwanini BDF wawafunge?
Timu hii ni mahiri sana kule Botswana, lakini kwa
ubora waliokuwa nao Yanga, bila shaka watakalishwa.
Siku za karibuni Yanga wamekuwa na tatizo la
kutumia nafasi wanazopata uwanjani katika mechi za ligi. Timu ina washambuliaji
hatari kama Kpah Sherman, Amissi Tambwe, Simon Msuva, Danny Mrwanda, Mrisho
Ngassa na wengineo.
Lakini ni kawaida kwa Yanga kupata nafasi tano
wakafunga moja au wasifunge kabisa. Hata kocha Hans van der Pluijm amekiri
kuwepo kwa tatizo la umaliziaji.
Michuano ya Shirikisho ni mikubwa barani Afrika, timu
zinazoshiriki ni kubwa pia. Yanga wakumbuke wanaenda kucheza na timu nzuri ya
Botswana. Hawa ni makamu bingwa kama ilivyo kwao Yanga Tanzania.
Cha msingi ni kuhakikisha wanacheza kwa nidhamu ya
hali ya juu na kutumia kila nafasi watakayopata ili kupata ushindi mkubwa.
Ushindi wa kuanzia mabao 3-0 utakuwa na faida
kubwa kwa Yanga kwani itakuwa rahisi kwao kulinda ugenini kwa maana ya
Wapinzani wao watahitaji mabao 4-0 ili kuwatoa Yanga.
Lakini ushindi wa bao 1-0 au 2-0, 2-1, 3-2
utawaweka Yanga mazingira magumu kwani lolote linaweza kutokea ugenini, hata
kama wanaweza kulinda ushindi wa goli
1-0 ugenini.
Mashabiki wa Yanga jitokezeni kwa wingi, wale wa
mikoani iombeeni dua timu yenu hata kama imewanyima haki ya kuuona mchezo huo kupitia
Televisheni.
Kila la kheria Dar Young Africas katika mechi yenu
ya leo!!.
0 comments:
Post a Comment