
Msuva amefikisha magoli 6 mawili nyuma ya Didier Kavumbagu wa Azam fc
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
YANGA SC imeitungua Tanzania Prisons mabao 3-0
katika mechi ya ligi kuu soka Tanzania bara iliyomalizika jioni hii uwanja wa
CCM Sokoine, Mbeya.
Mabao ya Yanga yamefungwa na Saimon Msuva (dakika
ya 3, 62’ na Andrey Coutinho 11’).
Kwa matokeo hayo, Yanga wameishusha Azam kileleni
baada ya kufikisha pointi 28 katika mechi 14 walizocheza na wanawaacha Azam
nafasi ya pili wakiwa na pointi 26 kwa mechi 14 walizocheza baada ya jioni hii kutoka suluhu (0-0) na Ruvu
Shootings uwanja wa mabatini, Pwani.
Licha ya kuwazidi Azam kwa pointi, Yanga pia
wamewazidi wanalambalamba wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Azam wamefunga magoli 22 na kufungwa 12, tofauti
ya magoli ya kufunga na kufungwa ni 10, wakati Yanga wao wamefunga magoli 18 na
kufungwa 7, tofauti ni 11.
Ushindi wa leo ni salamu tosha kwa Mbeya City fc
ambao watachuana na Yanga katika uwanja wa Sokoine, jumapili ya wiki hii.
Tanzania Prisons wameendelea kuburuza mkia
wakijikusanyia pointi 11 tu katika mechi 14 walizoshuka dimbani.

Andrey Coutinho

Andrey Coutinho
REPOTI YA MECHI
Mapema dakika ya 3’ Saimon Happygod Msuva
aliifungia Yanga bao la kuongoza akimalizia mpira wa kona uliochongwa na kiungo
mshambuliaji raia wa Brazil, Andrey Coutinho.
Msuva aliruka juu sambamba na kipa na mpira
ulipotua aliugusa kwa mbali na ukamponyoka mlinda mlango na kuzama goli.
Wachezaji wa Prisons walihamaki wakiamini Msuva
amemsukuma kipa, lakini mwamuzi akahesabu bao.
Bao la pili lilifungwa dakika ya 11’ ya kipindi
cha kwanza ambapo Coutinho alipiga shuti la kawaida, beki wa Prisons akiwa
katika harakati za kuokoa alijifunga mwenyewe.
Yanga waliendelea kucheza vizuri, wakigongeana
pasi na kufika eneo la hatari la Prisons, lakini safu ya Prisons ilifanya
vizuri licha ya kupata misukosuko.
Katika kipindi hicho, Prisons walitulia baada ya
kufungwa na kupata nafasi kadhaa, lakini walishindwa kuzitumia.
Mpaka dakika 45’ za kipindi cha kwanza
zinamalizika, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili, Prisons walianza kutafuta mabao
ya kuzawazisha, lakini Yanga waliendelea kuonesha uzoefu wao wakiwatuliza
vizuri.
Katika dakika ya 62’ Andrey Coutinho aliingiza
kona maridadi na Msuva akapiga kichwa ‘ndosi’
na kuzamisha goli la tatu.
Msuva alipata upenyo huo kutokana na uzembe wa
beki wa Prisons, Salum Kimenya aliyekuwa anamuangalia tu wakati akimtoka kupiga
kichwa.
Coutinho leo hii amefunga goli na kusababisha
magoli mawili ya Msuva kutokana na mipira yake ya kona.
Msuva amefikisha mabao 6 msimu huu, magoli mawili
nyuma ya kinara wa kupachika mabao, mshambuliaji wa Azam fc, Didier Fortune
Kavumbagu.
0 comments:
Post a Comment