
Rais wa TFF, Jamal Malinzi ana changamoto kubwa ya kuinua soka la Bongo
Na
Oswald Ngonyani
PENGINE inaweza
ikawa ni kauli ambayo itaonekana kuwaghadhabisha wengi, lakini acha tu niuweke
wazi ukweli huu, kwani nikikaa kimya nitakuwa miongoni mwa watu wasioitakia
mema nchi hii hasa katika tasnia ya mchezo wa soka.
Soka la bongo ni
la kijanjajanja, kila mdau wa soka analijua hilo kinagaubaga. Viongozi wa soka
la bongo ni wajanjajanja, wachezaji nao ni wajanjajanja pia. Hata mashabiki nao
wana hulka hizo hizo za ujanja ujanja.
Hakuna
ustahimilivu wa soka hapa Tanzania. Ubabe, Vitisho na hata Chuki ni nguzo zilizo
wazi zinazoonekana kuongoza soka la bongo. Hakuna dalili ya kufika
tunakokutarajia, tutafikaje huko tunakokutaka wakati marubani wetu ni wajeuri?
Hakuna ‘seriousness’.
Hakuna uzalendo tena, watendaji wakuu wenye dhamana ya kuiongoza soka yetu wapo
kama hawapo huku wakiwa vibaraka wakubwa wa maswahiba wao wanaoongozwa na hulka
ya ujeuri, kiburi pamoja na fitna, vitu ambavyo havikutakiwa kupewa nafasi
lakini wao wamevipa nafasi.
Nakumbuka Msimu uliopita
(2014) kulijitokeza madudu mengi sana katika soka letu watanzania na hata
kuleta hali ya sintofahamu miongoni mwetu sisi kwa sisi. Ubovu huu wa
kiutendaji unawahusu viongozi wote, yaani viongozi wa juu soka wa letu mpaka wa
chini katika ngazi ya vilabu.
Kuna mambo
makubwa ambayo Viongozi wetu katika ngazi ya juu waliyafanyia kazi kimizaha
sana na hata kutoa majibu marahisi mno, majibu ambayo kwa kiasi kikubwa
yaliwafanya wadau wengi wawaone viongozi hao kama wana nia ya kudidimiza soka
la Tanzania, badala ya kuboresha.

Dkt. Damas Ndumbaro amefungiwa miaka saba
Pengine walikuwa
sahihi lakini kwa bahati mbaya jamii ya wafuasi wa soka la bongo hawakuwaelewa.
Wakati fulani suala la kufungiwa miaka saba kwa daktari wa sheria, Dk. Damas
Ndumbaro lilionekana kuibua mjadala mzito sana ambao mpaka leo upo japo makali
yake yamepungua.
Yaliyotokea
kuhusu sakata hilo ni mengi, na hata kuwafanya mashabiki na wafuasi wa soka la
bongo wabakie katika pande mbili zinazokinzana. Wapo walioiunga mkono TFF kwa
maamuzi yake hayo lakini pia wapo waliokuwa upande wa Ndumbaro ambao unaonekana
kuwa na watu wengi zaidi.
Sarakasi za namna
hii si ngeni katika soka la bongo, ni vitu ambavyo vipo na vinatokea mara kwa
mara tena kwa namna ya pekee sana hutangazwa sana katika Vyombo vyetu vya
Habari na hata kuwafikia watanzania walio wengi.
Yapo mengi sana
ambayo viongozi wetu wanayafanya na hata kuwapa hasira mashabiki wa soka la
bongo. Mbali na viongozi hao wa ngazi ya juu, vilabu vyetu navyo vinafanya
madudu mengi ambayo yanawafanya mashabiki wao wabaki babaikoni.
Hii yote
inachagizwa na ujanja ujanja wa Viongozi lakini pia wachezaji wa timu husika.
Leo hii mchezaji mkongwe katika soka la bongo Shaaban Kisiga ‘Marlon’ ametoweka
katika kambi ya timu yake ya Simba mara baada ya mchezo dhidi ya Mbeya City.
Huo ni utovu wa nidhamu lakini pia ni hulka ile ile ya ujanja ujanja.
Juma Nyosso amefungiwa mechi 8 kwa utovu wa nidhamu
Tangu
alipoondoka, awali viongozi wa timu husika walionekana kudai kuwa mchezaji huyo
alipewa ruhusa maalumu lakini baadaye yeye mwenyewe Kisiga alitanabaisha kuwa
ameondoka bila ruhusa na kamwe hatarudi tena klabuni hapo.
Kuna kitu
nimejifunza hapo kuhusu suala hili. Si mchezaji pekee hata Viongozi wake wote
kwa pamoja wanaangukia katika nadharia hii ya ujanja ujanja, Kiongozi anasema
hili, lakini mchezaji na yeye anakuja na kuzungumza lake, hii ndiyo taswira
halisi ya soka la bongo.
Sahau kuhusu
sakata la Juma Nyosso wa Mbeya City kuhusu kumpapasa makalio mshambuliaji wa
Simba Elias Maguri na baadaye kuamua kuomba msamaha. Sahau kuhusu sakata la
Tambwe na yule beki wa Ruvu Shooting.

Lakini pia fanya
kumbukizi kuhusu ishu ya Emmanuel Okwi aliyepigwa kiwiko na beki wa Azam FC.
Kwa neno rahisi sana, matukio yote haya yaliyofanywa na wahusika yanaendana na
hulka zile zile za ujanja ujanja.
Misimu kadhaa
iliyopita Mshambuliaji machachari wa Yanga alikuwa akiitumikia klabu ya Simba
na hata alipomaliza mkataba wake aliamua kwa dhati ya moyo wake kuchukua
mamilioni ya Simba kwa lengo la kusaini mkataba mpya kwa klabu hiyo, lakini
baadaye akaamua kusaini Yanga. Maisha ya mwanandinga huyo kwa sasa
yanasikitisha sana.
Ujanja ujanja
aliokuwa ameufanya kwa kuchukua pesa katika pande mbili zinazokinzana yaani
Simba na Yanga leo hii zinamjutisha kijana huyu aliyewahi kuwazimia simu
maafisa fulani wa timu kutoka nje ya nchi waliokuja bongo kuisaka saini yake
eti ili wakimpigia wasimpate.
Nakumbuka wakati fulani Uongozi wa Klabu
ya Yanga ulifunguka kuwa hauhusiki na deni la mshambuliaji wao huyo anayedaiwa
fedha na Benki ya CRDB kwa kuwa yeye aliomba udhamini katika timu hiyo na si
kulipiwa kama anavyodai.

Ngassa alinukuliwa akidai kushindwa kuwa
katika kiwango kizuri cha kuitumikia timu yake hiyo kufuatia deni la shilingi
milioni 45 alizokopa CRDB kwa ajili ya kuilipa Simba ili ajiunge na Yanga,
baada ya kusaini timu mbili kwa madai kuwa uongozi wa timu hiyo ungemsaidia
laki tano kila mwezi jambo ambalo Yanga wamelipinga.
Ujanja ujanja wake aliokuwa ameufanya
sasa unamfanya akose amani ya moyo wake. Mbwembwe zote za pale TFF wakati ule
alipoenda kulipa deni la Simba sasa hazipo tena. Wale waliomsindikiza kwa
bashasha nyingi wamejiweka kando pasi kumpa msaada wowote. Ujanja ujanja wake
umemponza.
Kuna mengi sana ya kuandika kuhusu
minajili ya soka la bongo kwa sasa, soka ambalo kwayo limetawaliwa na hulka ya
ujanja ujanja miongoni mwa mioyo ya tuliowapa dhamana ya kutuongoza lakini pia
wachezaji wetu nao wana hulka ile ile, hulka ambayo kamwe haitatufikisha
kokote. Hulka ya ujanja ujanja.
Tubadilike sasa. Naam ni wakati muafaka
sasa kwa viongozi wa soka nchini kubadilika. Mabadiliko haya yaanzie juu lakini
pia yaje mpaka kwenye vilabu ambapo Viongozi wa timu pamoja na wachezaji wao
watatakiwa kuwajibika kwa kadri inavyopasika na siyo kuendekeza hulka ya ujanja
ujanja.
TUKUBALI KUWA TUMEANGUKA, TUINUKE, TUANZE
SAFARI UPYA YENYE KULETA TIJA KWA SOKA LA BONGO.
Unapenda kuwa Mkufunzi wa mchezo wa soka?
Nunua sasa Kitabu cha ‘SIRI YA SOKA’ Uweze kuwa na uelewa zaidi katika mchezo
huo, Wasiliana na Mwandishi wa Makala haya kwa
simu namba 0767 57 32 87 ili kuweza kujipatia nakala ya Kitabu hicho.
0 comments:
Post a Comment