
Na Oswald Ngonyani
UPEKEE WA MCHEZO WA SOKA
Mpira wa miguu maarufu zaidi kwa jina la soka au
kandanda ni mchezo unaochezwa na jumla ya wachezaji ishirini na wawili katika timu mbili husika, kila timu ikiwa na
wachezaji kumi na mmoja.
Lengo hasa la mchezo huu ni wachezaji kuumiliki
mpira kwa kutumia miguu na kuuingiza mpira katika wavu wa wapinzani kadiri inavyowezekana,
ni mchezo wenye idadi kubwa ya mashabiki kuliko michezo mingine yote
inayochezwa katika pande zote za dunia.
Tofauti na michezo mingine yote, katika mchezo huu
matumizi ya mikono ni marufuku isipokuwa kwa mlinda mlango tena katika eneo
maalumu la ndani ya kiboksi chenye vipimo vya mita 18 lakini pia wakati wa
kurudisha mpira baada ya kutoka nje ya uwanja.
NAFASI YA WALINDA MLANGO KATIKA UCHAMBUZI WA
MCHEZO WA SOKA
Mara kwa mara wachambuzi wengi wa mchezo wa soka
tumekuwa tukiwasahau sana walinda mlango katika makala zetu za uchambuzi
tunazoziandika katika magazeti yetu ama mitandao mbalimbali ya kijamii.
Tumekuwa tukiwapa sana kisogo wachezaji hawa ambao
pengine ndio wachezaji muhimu zaidi kutokana na majukumu yao makubwa ya kuzuia
magoli tangu dakika ya kwanza mpaka kutimilika kwa mchezo husika.

UMARIDADI WA OLIVER KHAN
Kunako nafasi hii ya ulinzi wa goli, kuna mtu
anaitwa Oliver Khan. Jina hili si geni hata kidogo kwa mtu aliye mfuasi mzuri wa
mchezo wa soka. Mjerumani huyu ana sifa iliyotukuka katika mawanda ya soka la
kimataifa na hata kujikuta akiweka alama isiyofutika katika vichwa vya wapenzi
wengi wa soka duniani kote.
Mwanamume huyu kwa sasa ni mtu wa kukaa
jukwaani na kuuangalia mchezo wa soka na siyo mtu wa kucheza tena kandanda kama
ilivyokuwa awali. Hapana shaka nyakati na enzi zake zimekwishataradadi, lakini angali
akikumbukwa kwa kile alichokionyesha wakati ule akicheza kama mlinda mlango.
UBABE WAKE LANGONI
Kahn alikuwa ni aina ya wachezaji
wasiotaka masihara anapokuwa uwanjani. Nakumbuka aliwahi kuwakoromea
wachezaji wenzake na kutaka kuwapiga kwenye michuano ya fainali za Kombe la
Dunia mwaka 2006 zilizochezwa kwenye ardhi ya kwao Ujerumani na Italia kuibuka
bingwa.
![[OK.jpg]](https://1.bp.blogspot.com/_CU9TTeMjmLs/SEO3HezufgI/AAAAAAAAABE/g5IxFuMZ5mQ/s640/OK.jpg)
Kitendo cha wachezaji wenzake
kucheza ‘show game’ kwa lengo la kutia
nakshi ufundi wao wa kuuchezea mpira kilionekana kumuudhi sana golikipa huyu
aliyewapasha ‘live’ kuwa wachezaji
hao hawakujitoa kwa ajili ya timu ya ya Taifa, walionekana kukosa moyo wa
uzalendo.
Sifa yake kubwa ilikuwa ni uwezo
wake mkubwa wa kupanga safu yake ya ulinzi wakati timu yake ilipokuwa kwenye
hali ya kushambuliwa na timu pinzani. Hakuwa mwoga wa kuwaonya wenzake
pale walipokosea alikuwa tayari akosane nao kwa lengo la kuipigania timu yake.
Alikuwa hodari sana kwenye suala la
uokoaji wa mipira ya penalti, alikuwa mahiri katika matumizi ya viungo vyake
vya mwilini kama vile kichwa, miguu katika namna ambayo haikuweza kuelezeka.
Ilifikia wakati familia ya wapenda
soka wengi ulimwenguni ilimbatiza jina la ‘Mikono
elfu moja’ kutokana na umaridadi wake wa kuzuia michomo langoni katika kila upande
wa lango alilokuwa analilinda.
Haikuwa rahisi kumfunga magoli ya
kizembe. Ilikuwa ni lazima mfungaji atumie mbinu ya ziada zaidi kuliko ilivyo
kwa magolikipa wetu wa kizazi cha sasa. Kwa sasa hayo yote yamebaki kuwa
historia, ni wazi kuwa ataendelea kukumbukwa na kuheshimika duniani kwa yale
aliyoyafanya katika enzi na nyakati zake.

ALIANZAJE KUCHEZA MPIRA?
Alianza kuitumikia timu ya
taifa, Ujerumani mwaka 1994, kwenye ngazi zote za vijana, hadi kustaafu soka
mwaka 2006. Moja kati ya mechi ambayo mashabiki wa soka hawawezi kumsahau
Khan, ni kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2002.
Mchezo huo ulizikutanisha Brazil na
Ujerumani, lakini uliisha kwa Brazil kutwaa kombe kwa kuwafunga Ujerumani mabao
2-0. Mabao hayo, aliyafunga Ronaldo De Lima, baada ya mkongwe Khan kutema
mipira iliyokuwa imepigwa na Rivaldo Ferreira.
Kitendo hicho cha kutema mipira
miwili iliyosababisha kufungwa kwa Ujerumani, kilimudhi sana mkongwe huyu na
kuanza kulia uwanjani hapo baada ya mchezo huo kumalizika. Ana umri wa
miaka 45 kwa sasa na amekwishastaafu soka kitambo.

Makuzi yake ya soka yalianzia kunako
klabu ya Karlsruher S.C ya nchini Ujerumani. Mwaka 1994 alijiunga na Klabu ya
Bayern Munich na kustaafu soka lake akiwa na klabu hiyo ambayo alikuwa
ameitumikia kwa mafanikio na mahaba makubwa.
MATAJI ALIYOSHINDA
Kahn ameweza kushinda mataji mengi
kwa timu kiujumla na tuzo nyingine nyingi binafsi. Mwaka 2001,
alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi, kwenye mchezo wa fainali ya UEFA,
dhidi ya Valencia na timu yake, Bayern Munich.
Haikuishia hapo, msimu wa 2000-2001,
alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa ligi ya Ujerumani.
Kwenye mwaka 1999, 2001 na mwaka
2002 Khan, alichaguliwa kuwa mlinda mlango bora zaidi kwenye ligi zote barani
Ulaya.
Katika miaka ya 1994, 1997, 1998,
1999, 2000, 2001 na mwaka 2002, Kahn aliweza kuchaguliwa mlinda mlango bora
kwenye ligi Kuu ya Ujerumani ‘Bundesliga’.Kwenye kikosi bora cha michuano ya
Kombe la Dunia, mwaka 2002, Khan alichaguliwa kuwa mlinda mlango bora na kupewa
tuzo iliyozidi kuchagiza ubora wake.
HITIMISHO
Hapana shaka orodha hiyo ya
tuzo na mataji kwa nyanda huyu ni ushahidi tosha kuwa dunia itaendelea
kumkumbuka zaidi kutokana na vile alivyokuwa amekitendea haki kipaji chake
awapo ndani ya milingoti mitatu.
Kwa sasa mlinda mlango huyo amekuwa
hajishughulishi tena na masuala ya soka, japokuwa kwa uchache, bali amekuwa
mshauri mzuri wa kocha wa sasa wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Leow.
Pamoja na kujiweka kando na soka
bado wachambuzi wengi wa masuala ya soka wangali wakiamini kuwa, ipo siku
atarudi kwenye mchezo huu wa soka kama mwalimu kwenye timu yoyote ile ya Taifa
ama klabu.
Hapana shaka wakati utatupa majibu
stahiki.
(Maoni/Ushauri
tuma kwenda namba 0767 57 32 87.)
0 comments:
Post a Comment