
Na Richard Bakana, Dar es salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mh. Said Meck Sadick ameipongeza klabu ya Azam FC kwa ushindi waliopata jana dhidi ya Al Merreickh kutoka Sudan katika mchezo wa klabu bingwa huku akiwataka wachezaji wasibweteke zaidi na kuona wamevuka kigingi hicho zaidi, wajiandae kwa mchezo wa marudiano.
Akizungumza jana Mh. Meck Sadick ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mchezo huo, amesema kuwa Al Merreikh ni timu kubwa Afrika Mashariki na kati lakini kujituma kwa wawakilishi hao wa Tanzania watakapokuwa ugenini ndio itakuwa silaha ya ushindi.
“Nawapongeza Azam FC wamecheza vizuri sana, wapinzani wao ni wazoefu na ni timu kubwa tu, lakini vijana wamecheza vizuri na kupata ushindi, Kikubwa wasibweteke na kujiona kama tayari wamemaliza mchezo, Hivyo hivyo kwa Yanga nao walicheza vizuri lakini kwenye mechi za ugenini wajitume zaidi” Amesema Sadick.
Zikiwa ni kampeni zake za kwanza katika michuano ya klabu bingwa Afrika toka ianzishwe, Klabu ya Azam FC ilifanikiwa kuwafunga Al Merreickh kwa jumla ya mabao 2-0 yakipachikwa kambani na Didier Kavumbagu dakika ya 9 kipindi cha kwanza na John Bocco katika kipindi cha pili ikiwa ni mpira wake wa kwanza kugusa akitokea benchi baada ya kuchukua nafasi ya Kipre Tchetche aliyepumzishwa na Kocha Joseph Omog.
Kwa upande wa mashabiki walioshuhudia mtanange huo wameonyesha kufurahishwa na kiwango cha Azam huku wakisema kuwa wangekuwa makini wangeibuka na ushindi wa mabao mengi zaid ya waliyopata.
“Kwenye mchezo huu Azam wamebadilika sana, wanakaba vizuri kwa nidhamu, wanaenda mbele kushambulia na kurudi nyuma kwa heshima zote za mchezo, Leo (jana) walitakiwa wapate zaidi ya magoli matatu lakini umakini tu wa wachezaji wetu Sure Boy amekosa mabao mawili ya wazi” Amesema Shabiki wa Soka Abdul Juma.
“Wameonyesha kuwa wamejiandaa kupambana klabu bingwa, kwa leo sina cha kuwakosoa Azam, wamecheza vizuri sana yale matatizo pale nyuma kwa mabeki leo (jana) Wawa kasawazisha kabisa akisaidiana na Aggrey” Amesema Hawadhi Rashid Shabiki wa Simba.

0 comments:
Post a Comment