Mashabiki wakiwa wamekaa chini katika Uwanja wa Chamazi baada ya sehemu za kukalia kujaaa katika moja ya michezo iliyochezwa katika uwanja huo na kuhusisha watu wengi.
Na Richard Bakana, Dar Es Salaaam
UONGOZI wa klabu ya Azam FC umelitupia mbali ombi la mashabiki na wapenda soka la kuwataka baadhi ya mechi zao kubwa za Kimataifa kuzihamishia katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam ili kutoa fursa kwa mashabiki wengi kutazama mchezo husika.
Hayo yamekuja baada ya jana zaidi ya mashabiki Elfu tatu (3000) kushindwa kuingia Uwanjani kutazama mchezo kati ya Azam FC na Al Merreikh baada ya Uwanja huo kujaa mapema huku watu wengine wakibaki nje wakiwa na tiketi mkononi kitu ambacho kiliwafanya wauombe uongozi wa Klabu hiyo kupeleka baadhi ya michezo kwenye uwanja wa Taifa.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saddy Kawemba amesema kuwa Kama uongozi watakaa kikao na kutoa taarifa kamili, lakini amedai kuwa suala la kuhamishia mechi zao Taifa ni kitu ambacho hakiwezekani.
“Sikuwa na taarifa kama hayo yalitokea, lakini uongozi tutakaa Kikao na baada ya kufuatilia kila kitu tutatoa taarifa kamili, lakini uamuzi wa kuhamishia mechi zetu Taifa hatuupi kipaumbele” Amesema kiongozi huyo.
Februari 15 katika mkutano wa waandishi wa habari na makocha wa Azam FC na Al Merreikh kwenye ofisi za TFF Karume, Meneja wa Azam, Jemedari Said Mzumari aliulizwa na mmoja viongozi wa Waarabu hao sababu za kuchezea mechi hiyo Chamazi na sio Taifa na akajibu:.
“Chamazi ndio uwanja wetu wa Nyumbani, FIFA na CAF wameturuhusu kuutumia kwa michezo yote ya kimataifa baada ya kuridhishwa na ubora wake, isitoshe Taifa sio kwetu tunataka kutumia Home advantage (Faida ya kucheza nyumbani)” alisema Jemedal Said.

Kwa upande wa mashabiki wakizungumzia mazingira waliyokutana nayo jana katika heka heka za kuingia kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kubeba watu Elfu 7000, baadhi walionesha kusikitishwa na na kitendo cha kufungiwa milango na kurudi nyumbani bila kuona mtanange huo.
“Mimi nimefika hapa kama dakika ya 10 baada ya mpira kuanza, nimenunua tiketi lakini nilipokwenda kuingia nikakuta milango imefungwa wakisema eti Uwanja Umejaa, Sasa najiuliza kivipi Uwanja utajaa wakati nje watu wengi tu tumebaki tukiwa na tiketi zetu” Amesema Salim Mbaruku mpenzi wa Soka Tanzania.
“Jana (Juzi) walisema kuwa tuje mapema Uwanja unachukua watu 7000 tu, sawa nimekuja mapema hapa nimechukua tiketi yangu nikarudi nyumbani kuweka sawa mambo yangu, nimerudi muda huu nakuta milango imefungwa eti Uwanja umejaa wakati nje kunawatu wanatiketi tena wengi” Amesema Fikiri Juma Shabiki w Soka.
“Nimeshindwa kwenda Morogoro ili niwaone Al Merreikh lakini nimefika hapa tunakatazwa kuingia kwasababu uwanja umejaa, Labda niwaambie Uongozi wa Azam kuwa huu uwanja ni mdogo sana Watu 7000 katika soka ni mashabiki wachache sana, kama kutakuwepo na mechi kubwa kama hii bora wawe wanahamishia Taifa ili kutoa nafasi kwa mashabiki wengi watazame mpira” Amesema Charles Edward shabiki wa Simba.


0 comments:
Post a Comment