Nyota wa azam fc washindwa kushangilia goli leo
MABINGWA watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Azam fc wameendelea kuisoma namba ya Yanga baada ya kutoka suluhu (0-0) dhidi ya Tanzania Prisons katika mechi ya ligi kuu soka Tanzania bara iliyomalizika usiku huu uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Tangu waifunge Al Merreick mabao 2-0 ligi ya mabingwa Afrika mwishoni mwa wiki iliyopita, Azam fc hawajapata ushindi wala kufunga goli lolote.
Alhamisi ya wiki hii, februari 19, walitoka suluhu (0-0) dhidi ya Ruvu Shootings katika mechi ya ligi kuu iliyopigwa uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.
Kwa matokeo ya leo, Azam wamefikisha pointi 27, pointi nne nyuma ya Vinara Yanga.
Yanga wameifunga Mbeya City 3-1 uwanja wa Sokoine, jioni ya leo.
Sasa Azam wamecheza mechi 15, wameshinda 7, wametoa sare 6, wamepoteza 2. Wamefunga magoli 22 na kufungwa 12, tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa ni 10.
Katika mechi ya leo, mlinda mlango wa Prisons, Mohammed Yusuph amekuwa kikwazo kikubwa kwa Azam fc kupata pointi tatu muhimu.
Kwa dakika zote aliokoa michomo ya hatari ya washambuliaji wa Azam fc na kuipata pointi moja timu yake iliyopoteza kwa kufungwa mabao 3-0 dhidi ya Yanga, alhamisi wiki hii.
Prisons wamefikisha 12 mkiani mwa msimamo wa ligi kuu soka Tanzania.
0 comments:
Post a Comment