
Mbwana Samatta (kushoto) na Thomas Ulimwengu (kulia) wataionesha kazi Burundi iliyoitungua 3-0 Taifa Stars Aprili 26 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars inaendelea
kujinoa katika mazoezi yake ya mwisho mwisho mjini Bujumbura kuelekea kuchuana
na Burundi hapo kesho (septemba 7 mwaka huu).
Mechi hiyo ya kimataifa ya kirafiki ipo katika
kalenda ya Shirikisho la soka Duniani, FIFA.
Kikosi cha wa wachezaji 20 wa Stars tayari
kilishatua Bujumbura tangu jana na tayari kilishaanza kuzoea hali ya hewa nchini
humo, huku morali ya wanandinga wote ikiwa juu kabisa.
Stars itaongozwa na Watanzania wawili wanaokipiga
TP Mazembe ya DR Congo, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu kulipa kisasi cha
kufungwa mabao 3-0 na Burundi katika mchezo maalumu wa kirafiki uliofanyika
April 26 mwaka huu uwanja wa Taifa kuadhimisha miaka 50 ya Muungano.
Katika mechi hiyo kikosi cha Stars iliyosheheni
wachezaji waliotoka katika mpango maalumu wa maboresho ya Taifa Stars
uliofanywa na shirikisho la soka Tanzania, TFF, ilishindwa kuhimili
makali ya washambuliaji wa Burundi kama vile Didier Kavumbagu na Amiss Tambwe,
lakini kesho itaingia kikosi kamili gado.
Wachezaji waliopo Burundi chini ya kocha Mholanzi,
Mart Nooij ni makipa Mwadini Ali (Azam fc) na Deogratius Munishi ‘Dida’,
(Yanga).
Wachezaji wengine ni Shomari Kapombe (Azam fc),
Oscar Joshua (Yanga), Said Mourad (Azam fc), Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga),
Kelvin Yondani (Yanga), Joram Mgeveke (Simba).
Wengine ni Saimon Msuva (Yanga), Erasto Nyoni
(Azam fc), Himid Mao (Azam fc), Amri Kiemba (Simba), Haroun Chanongo (Simba),
Salum Abubakary ‘Sure Boy’ (Azam fc), Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya, Qatar),
Hamis Mcha ‘Vialli’ (Azam fc), Juma Luizio (Zesco United, Zambia), Mrisho Ngasa
(Yanga), Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu (wote TP Mazembe, DR Congo).

0 comments:
Post a Comment