
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Agosti 4, 2014, saa 3:07 usiku
TIMU mbili za Taifa za Tanzania, Taifa Stars na
Serengeti Boys zimerejea Dar es salaam kwa ndege ya Air Tanzania kutokea
Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Stars ilitokea Mjini Maputo na kuungana na wadogo
zao nchini Afrika kusini na kusafiri pamoja leo.
Kikosi cha Mart Nooij jana kilifungwa mabao 2-1 na Msumbiji katika
mchezo wa kuwania kupangwa hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali
za mataifa ya Afrika, Afcon 2015 nchini Morocco.
Mechi ya kwanza katika uwanja wa Taifa jijini Dar
es salaam, Stars ilitoka sare ya mabao 2-2 na Mambas na baada ya matokeo ya
jana ilitupwa nje ya mashindano kwa wastani wa mabao 4-3.
Kwa upande wa timu ya taifa ya vijana chini ya
miaka 17 Serengeti Boys yenyewe jumamosi Agosti 2 mwaka huu ilifungwa mabao 4-0
katika mchezo wa marudiano nchini Afrika kusini na kutupwa nje ya michuano ya
kuwania kufuzu fainali za Afrika kwa vijana.
Mechi ya kwanza uwanja wa Azam Complex, Chamazi
nje kidogo ya jiji la Dar es salaam, Serengeti walitoka suluhu ya bila kufungana
na Amajimbos, hivyo matokeo ya jana yamewafanya watolewa kwa wastani wa
mabao 4-0.

Afisa habari wa Shirikisho la soka Tanzania , TFF
aliyeambatana na Taifa Stars nchini Msumbiji na kambi ya siku mbili Afrika
kusini amesema kwamba timu zote zimewasili salama na kambi zote zimevunjwa
rasmi leo hii.
“Timu zote mbili zimerejea saa 9 alasiri kwa ndege
ya Air Tanzania zikitokea Johannesburg Afrika kusini. Timu zote zilikuwa kwenye
michuano ya Afrika, lakini kwa bahati mbaya zote zimetolewa na kambi zimevunjwa
rasmi leo kusubiri programu nyingine za walimu.” Alisema Wambura.
“Kw utaratibu wa mpira, timu inapoingia kwenye
mashindano, yanapokwisha au kuishia njiani, lazima benchi la ufundi likiongozwa
na kocha mkuu litengeneze ripoti na kuiwasilisha sekretarieti, halafu inapelekwa
kamati ya ufundi na kujadiliwa na baadaye inapelewa kamati tendaji na kuyafanyia
kazi mapendekezo.”
Hata hivyo beki wa kulia wa Stars, Shomary Kapombe
jana alimwaga machozi baada ya Stars kufungwa na baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa
Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es salaam alizungumza na waandishi wa
habari.
Kapombe alikiri kuumizwa na matokeo ya jana na
kuwataka watanzania kutokata tamaa na timu yao.
“Mchezaji kama mchezaji lazima uyapokee matokeo,
lakini unaangalia tumefungwaje. Mechi ya Msumbiji matokeo kweli tumefungwa, lakini
kuna vitu vinakatisha tamaa kama maamuzi ya refa.’ Alisema Kapombe.
“Katika mpira kuna changamoto, lakini napenda
kuwaambia Watanzania kwamba wayapokee matokeo. Haikuwa nia yetu kufanya hivyo,
tulienda kupigana ili kulinda matokeo, lakini tumefungwa, Watanzania wasife
moyo, yatatokea mashindano mengine
tutafanya vizuri”
“Nimejifunza kuwa Katika mashindano yoyote sasa
hivi mchezo wa nyumbani ni muhimu zaidi. Nimeona tulivyokosa ushindi nyumbani,
imetugharimu ugenini. Hili ni fundisho.”
0 comments:
Post a Comment