Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Agosti 4, 2014, saa 2:17 usiku
BAADA ya mkutano mkuu wa klabu ya Simba
uliofanyika jana Agosti 3, 2014 kufikia maamuzi ya kuwafuta wanachama 72
uanachama wa klabu hiyo kwa kosa la kupeleka masuala ya mpira mahakamani,
Michael Richard Wambura ataunguruma kesho kuzungumzia hilo.
Katibu mkuu huyo wa zamani wa kilichokuwa chama
cha soka Tanzania, FAT ni miongoni mwa wanachama hao waliofukuzwa jana na
mkutano mkuu.
Wambura na Mtemi waliipeleka Simba mahakamani
mwaka 2010 kinyume na katiba ya Simba, TFF, CAF na TFF ambapo ni marufuku
kupeleka masuala ya mpira katika mahakama za kawaida za haki.
Wanachama wengine 70 walienda mahakama kuu
wakipinga kuenguliwa kwa Wambura katika uchaguzi wa juni 29 kwa madai kuwa
katiba ya Simba imekiukwa, hivyo wakaitaka mahakama kusimamisha uchaguzi.
Mahakama ilikubali kusikiliza shauri hilo na kesi
ipo mahakamani, lakini iligoma kusimamisha uchaguzi wa Simba uliofanyika juni
29 mwaka huu.
Akizungumza leo jijini Dar es salaam, Wambura
amasema kesho atapata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari, hivyo
itakuwa nafasi nzuri ya kuweka kila kitu wazi.
“Nimesoma kwenye vyombo vya habari leo asubuhi
kuwa jana kulikuwa na mkutano mkuu na ulikuwa unahusu wanachama 69 waliopeleka
kesi mahakamani, pamoja na mimi na mwenzangu tuliopeleka kesi mwaka 2010.” Alisema
Wambura.
“Mimi natafakari na nadhani kesho nitaongea na waandishi wa habari baada ya kuwasiliana na
watu mbalimbali, kujua wanasheria wanasemaje na katiba ya Simba inasemaje. Kesho
nitaeleza kwa kina kila kitu na maswali yote yatajibiwa.”
Jana makamu mwenyekiti wa Simba sc, Geofrey Nyange
‘Kaburu’ alisema wanachama wote waliofukuzwa walipewa barua kabla za kuwataka
wafike kwenye mkutano mkuu, lakini hakuna hata mmoja aliyehudhuria.
Lakini Wambura ameonekana kukana kupata barua hiyo
na kauli yake ni hii hapa: “Kama mimi nimesoma leo kwenye vyombo vya habari
kuwa kulikuwa na mkutano mkuu, unapata jibu kuwa nilipata barua au hapana. “Hivyo
vyote ni suala la ushahidi, kama kweli walinipa barua, ni nani alinipa, nani alisaini, zilikuwa barua
za nini”
“Cha muhimu kesho nitazungumza na waandishi wa
habari na itakuwa ni nafasi nzuri ya kueleza yote.”
0 comments:
Post a Comment