
'Kaka mkubwa' Athumani Idd 'chuji' bado anagangaika kutafuta timu baada ya kutemwa na Yanga
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
TIMU mbalimbali za ligi kuu soka Tanzania bara
zinaendelea kufanya usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu mpya unaotarajia
kuanza kutimua vumbi septemba 20 mwaka huu.
Dirisha la usajili linatarajia kufungwa Agosti 27
mwaka huu kufuatia Shirikisho la soka Tanzania kusogeza mbele siku 10 kutoka
siku ya mwisho ambayo ilikuwa Agosti 17.
Usajili maana yake ni rahisi tu. Ni kuongeza nguvu
katika kikosi kilichotumika msimu uliopita. Inawezekana kubalisha wachezaji
wote, lakini huwa ni vigumu kutokea katika mchezo wa soka.
Timu inaweza kufanya usajili wa aina mbili.
Kuwapandisha wachezaji kutoka kikosi B au kutafuta wachezaji wapya nje ya timu
hiyo.
Kinachofanyika siku zote ni kupunguza wasiokufaa
na kuongeza wachezaji wapya watakaokuongezea nguvu zaidi katika mipango ya ligi.
Kama kusajili mara nyingi ni kuongeza nguvu, basi
watu wanaotakiwa kuhusika zaidi ni wakuu wa mabenchi ya ufundi kwasababu wao
ndio wanajua mapungufu ya vikosi.
Makocha ndio watu pekee wanaokaa na wachezaji kwa
muda mrefu, wanawafahamu kwa kila kitu,
wanatambua nidhamu na viwango vyao, hivyo wanapopendekeza fulani aachwe na fulani
aongezwa abaki, lazima waheshimiwe.

Nahodha wa zamani wa Simba na Taifa Stars Henry Joseph Shindika bado mambo hayajamnyokea baada ya kutemwa na Simba sc
Lakini kibongobongo, nao makocha wanakuwa na mambo
yao nyuma ya pazia. Wengine wanaweza kupendekeza kuachwa kwa mchezaji kwa
sababu binafsi. Tunajua baadhi ya makocha wanakuwa na mahusiano mabaya na
wachezaji nje ya uwanja, hivyo huamua kuwaondoa.
Ni kweli, lazima kocha awe na mchezaji anayemtii
ili wafanye kazi kwa mafanikio, lakini kuna wakati ‘udingi’ wa makocha unaleta
matatizo kwenye timu. Mfano makocha aina ya Luis Felipe Scolari aliyetimuliwa
na Brazil, kwa mtazamo wangu hawastahili katika soka la kisasa.
Naamini zaidi makocha vijana, makocha wa kisasa.
Makocha ambao wakati fulani wanaachana na migogoro binafsi na mchezaji na
kufanya kazi ya uwanjani, halafu mambo mengine baadaye.

Betram Mombeki (kushoto) alizinguana na Loga na kuachwa na Simba
Nawapenda makocha wanaowachukulia wachezaji kama ‘washikaji’
tu. Kosa likitokea wanakaa na kuzungumza na si kutumia ubabe wa cheo.
Oooh! Nilishasema ni hivi, basi inakuwa hivyo.
Hashauriki, haambiliki hata kama amekosea. Hawezi kuwaelewa vijana wake kwa
kuwasikiliza wanahitaji nini. Hawa ni makocha wa kizamani sana, mpira
umebadilika.
Ninaposema makocha wa kisasa simaanishi moja kwa
moja suala la umri. Kocha anaweza kuwa ‘Dingi’, lakini akajua namna ya kuishi
na vijana wake ambao ni wadogo kiumri na wana mambo mengi ndani na nje ya
uwanja.
Inafahamika kuwa nidhamu ya mazoezi, nidhamu ya
ndani na nje ya uwanja kwa baadhi ya wanasoka nchini Tanzania ni ndogo sana.
Ndio maana wachezaji wengi wanaachwa na timu zao.
Hata hivyo, timu kubwa za Simba na Yanga mara nyingi
zinawaharibia wachezaji kwa kuwachukua na kuwatelekeza hovyo. Hata namna
wanavyovunja mikataba ni uzamani mtupu. Mara wachezaji wasilipwe haki zao, kila
kukicha utasikia migogoro inatokea wanapoachana na wanandinga wake.

Jabir Aziz (kushoto) aliachwa na Azam fc baada ya mkataba wake kuisha mwishoni mwa msimu uliopita
Leo hii ukipita katika mazoezi ya JKT Ruvu,
unamkuta Athamani Idd ‘Chuji’, Henry Joseph, Jabir Aziz, Betrem Mombeki na wengineo
wakifanya majaribio ili wasajiliwe.
Ukienda Mwadui unawakuta Mohamed Banka, kwa mara
nyingine Chuji, mara Juma Jabu wanafanya majaribio. Kila timu ndogo ya ligi kuu
ukilinganisha na Simba, Azam na Yanga inasheheni nyota waliotemwa na klabu
hizo.
Swali linakuja? Inakuwaje ‘Chuji’, Joseph, Aziz wanafanya
majaribio JKT Ruvu kwa muda mrefu wakati ametoka kucheza Simba au Yanga kwa
kiwango cha juu?
Hivi unadhani Chuji ameshuka kiwango kiasi kwamba
JKT Ruvu au Mwadui fc wamuangalie kwa mwezi mmoja au zaidi?
Unadhani Henry Joseph kaisha kiasi kwamba hawezi
kupata timu zaidi ya Simba au Yanga? Hapana. Kuna kitu kinatafutwa zaidi.
Wachezaji wengi wa Tanzania hasa wanaotemwa na
timu kubwa wanasahau kuwa katika maisha kuna kupanda na kushuka. Inapotokea
unashuka, lazima uwe na nidhamu ya hali ya juu ili kurudi mchezoni.

Jembe: Amri Kiemba (kushoto) ni mfano wa kuigwa
Mfano mzuri ni jinsi ambavyo Amri Ramadhani Kiemba
‘Baba wawili’ alivyojitunza. Aliachwa na Simba, Yanga akajiunga na timu ndogo
kama Kagera Sugar na mpaka akaenda Miembeni Zanzibar, lakini akarudi kwa nguvu
kutokana na nidhamu ya mazoezi.
Mfano wa wachezaji kama hawa ni wachache sana. Leo
hii Fundi, Shaaban Kisiga ‘Malone’ anasajiliwa na Simba licha ya umri kwenda
kutokana na nidhamu ya mpira aliyonayo. Amekaa kwenye ‘game’ kwa muda mrefu.
Wachezaji wa Kibongo wanawika msimu mmoja au
miwili tu, mara unasikia kachuja. Anapoenda timu ndogo, anafanyiwa majaribio
kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Tatizo la wachezaji wanaocheza Simba na Yanga
wakienda JKT Ruvu au timu nyingine, wanataka kuishi maisha yale yale.
Kama Yanga
alikuwa anapata posho kila akikutana na kiongozi kama Yusuf Manji, Seif Magari
na wengine, anataka akikutana na mwenyekiti wa Ndanda fc amtoe kichache nje ya
malipo rasmi.
Eti!, bosi vipi nimepigika, nitoe kidogo bhaaasi? Kumbe
bosi mwenyewe hana hizo hela na anafanya mipango ya kumuingizia mshahara mwisho
wa mwezi na hata wakati fulani anachelewa kutokana na uwezo mdogo wa timu
kiuchumi.
Inapotekea mazingira haya,wachezaji wengi wanaanza
vurugu na utovu wa nidhamu na kuona maisha yamekuwa magumu katika klabu hizo.
Cha msingi ni kwamba, JKT Ruvu, Ndanda fc,
hapawezi kuwa sawa na Yanga, Azam, au Simba. Mchezaji akienda huko ajue kuna
vitu atakosa tu. Zile pesa zakutoana kishikaji kutoka kwa akina Hans Poppe,
Seif Magari, Davis Mosha huwa hazipo.
Jambo la muhimu ni kujua kuwa katika maisha kuna
kupanda na kushuka. Ukienda timu ndogo unapata nafasi kubwa ya kucheza, jenga
nidhamu nzuri ya mazoezi, utarudi katika kiwango chako na kurudishwa Simba au
Yanga kama shujaa.
Lakini kama tabia za utovu wa nidhamu zitaendelea,
makocha wa timu ndogo na viongozi wataendelea kuwafanyia majaribio kwa miezi
miwili na zaidi wakiwahofia kuharibu timu zao.

0 comments:
Post a Comment