
Na Baraka Mpenja
HATUA ya Robo fainali ya michuano ya klabu bingwa
Afrika Mashariki na kati, Kombe la Kagame, inaanza kutimua vumbi leo jumanne
mjini Kigali, Rwanda.
Robo fainali ya kwanza itaanza majira ya 9:00
alasiri kwa kuwakutanisha wanyarwanda wawili, Polisi na Atletico.
Mechi hii inatazamiwa kuwa na upinzani mkubwa
kutokana na viwango vya timu hizo ambazo
zinafamiana vizuri katika michuano ya ligi kuu nchini Rwanda.
Robo fainali ya pili itaanza majira ya saa 11:00
jioni ambapo timu mbili pinzani nchini Rwanda, Rayon Sport na APR zitachuana
vikali.
Baada ya kuwafahamu washindi watakaocheza nusu
fainali leo, robo fainali nyingine mbili zitapigwa kesho jumatano.
Mabingwa wa Tanzania Bara, Azam fc maarufu kama
Wana Lambalamba watashuka dimbani kukabiliana na El Merreikh ya Sudan.
Kutokana na historia nzuri ya El Merreikh katika
soka la Afrika mashariki na kati, hakika Azam wamekwaa kisiki ambacho
wanahitaji maarifa makubwa kukivuka.
Meneja wa Azam fc, Jemedari Said alisema
wamejiandaa vizuri na wanafurahia kuchuana na timu ngumu ambayo itawapa kipimo
kizuri cha kujua maendeleo ya kikosi chao.
“Sio pambano jepesi, El Merreik ni timu yenye
historia kubwa. Sisi kama Azam hatuwaogopi, tunawaheshimu, tutapambana kupata
ushindi ili kutinga nusu fainali na hatimaye fainali na kutwaa ubingwa”.
Alisema Jemedari.
Jemedari alisema wachezaji wote waliokuwa
majeruhi, Waziri Salum ambaye hajacheza mechi yoyote, Leonel Saint -Preux l,
Shomari Salum Kapombe wote walifanya mazoezi, na kwa mara ya kwanza
kikosi kizima kilikuwa uwanjani kujiandaa na mchezo huo.
Mechi nyingine ya kesho jumatano itawakutanisha
KCC ya Uganda dhidi ya Altabara ya Sudan Kusini.

0 comments:
Post a Comment