
Kikosi cha Yanga sc msimu uliopita
Na Baraka Mpenja, Dar es laam
0712461976
LIGI kuu soka Tanzania bara inaanza kutimua vumbi
septemba 20 mwaka huu kwa timu 14 kuchuana vikali kuwania taji linaloshikiliwa
na mabingwa Azam fc.
Msimu ujao tutashuhudia timu tatu mpya
zilizofanikiwa kupanda ligi kuu ambazo ni Ndanda fc ya Mtwara, Stand United ya
Shinyanga na Polisi Morogoro.
Timu hizi zimechukua nafasi ya timu tatu
zilizoporomoka daraja msimu uliopita ambazo ni Ashanti United ya Ilala, jijini
Dar es salaam, Rhino Rangers ya Tabora na JKT Oljoro ya jijini Arusha.
Timu nyingine 11 zitaendelea kuwa zile zile ambazo
ni Azam fc, Yanga sc, Mbeya City fc, Simba sc, Kagera Sugar, Ruvu Shooting,
Mtibwa Sugar, JKT Ruvu, Coastal Union, Mgambo Shooting na Tanzania Prisons.
Msimu uliopita kulikuwa na mabadiliko katika
nafasi za juu. Azam walitwaa ubingwa, Yanga wakashika nafasi ya pili, Mbeya
City nafasi ya tatu na Simba nafasi ya nne.
Kama unafuatilia kwa umakini ligi kuu iliyoanzishwa
mwaka 1965 ikiitwa Ligi ya Taifa, baadaye Ligi Soka daraja la kwanza na
hatimaye kuitwa Ligi kuu mwaka 1997 utagundua kuwa Simba na Yanga ni klabu
zinazoongoza kutwaa ubingwa.
Tafsiri yake ni kwamba kocha anapoteuliwa kuiongoza
Yanga au Simba, anaaminika kuipa timu ubingwa na si vinginevyo. Utawala wa
Simba na Yanga umedumu kwa muda mrefu wamekuwa wakipokezana ubingwa kama vile
mbio za vijiti.
Watakujaje?: Moja ya kikosi cha Simba sc msimu uliopita
Licha ya hivyo, kuna timu ambazo miaka ya nyuma
ziliwahi kujitutumua na kubeba kombe, mfano Cosmopolitans FC (1967), Mseto Sports
(1975), Pan African FC (1982), Tukuyu Stars (1986), Coastall Union (1988),
Mtibwa Sugar (1999, 2002). Nyingine zitazitaja.
Ubingwa wa mwisho msimu wa 2013/2014 umetua
mikononi mwa timu changa ya Azam fc iliyoanza kushiriki ligi kuu msimu wa 2008/2009.
Katika kipindi cha miaka sita, Azam fc wameshindana na kutwaa ubingwa. Kitu
pekee kinachowasaidia wanalambalamba hao ni kuanzia pale walipoishia.
Tatizo la klabu nyingi za Tanzania hata Simba na
Yanga, ni kuanza upya mara kwa mara. Ni ngumu kuona timu inaanzia pale
ilipoishia. Kwa mfano timu inaweza kutwaa ubingwa msimu huu, msimu ujao
ikaondoka katika ushindani wa ubingwa na kushika nafasi ya tatu au nne.
Kwa mfano 2007/2008, Yanga na Simba zilikuwa
zinachuana vikali kusaka taji, lakini Azam ndio kwanza walikuwa wanacheza ligi
daraja la kwanza na kupanda ligi kuu msimu huo.

Kikosi cha mabingwa Azam fc msimu ulioipta
2008/2009 Simba na Yanga walikuwa vidume wa
kuwania taji na mwishoni wanajangwani wakatwaa kombe. 2009/2010 Simba wakiongozwa
na Mzambia Patrick Phiri walitwaa ubingwa bila kufungwa mechi yoyote na wapinzani
wao wakubwa walikuwa Yanga, Azam bado walikuwa wanahangaika kwa kutokea.
2010/2011 Yanga na Simba waliendelea kuchuana
vikali katika mbio za ubingwa na wanajangwani kutwaa taji, lakini msimu wa
2011/2012, Simba chini ya kocha Mserbia Milovan Cirvovic walitwaa kombe tena
kwa rekodi nzuri ya kuwatandika Yanga mabao 5-0.
Katika msimu huo Azam fc walishika nafasi ya pili
na ndio yalikuwa mafanikio makubwa kwa klabu hiyo. Ilipata nafasi ya kucheza
kombe la shirikisho barani Afrika ambapo ilifanya vizuri na kuishia raundi ya
tatu baada ya kuzitoa klabu za Al Nasir Juba ya Sudan kusini, Barrack YC ya
Liberia na kutolewa kwa mbinde na FAR Rabat ya Morocco.
Ukiangalia kwa umakini, katika msimu huu wa
2011/2012, Azam na Simba ndio walikuwa washindani wa ubingwa, Yanga walikaa
pembeni kidogo.
Msimu unaofuata, 2012/2013, Azam wakaanzia
walipoishia na kumaliza nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Yanga. Simba waliishia
nafasi ya tatu. Kwa maana hiyo, Azam ndio waliweza kuanzia walipoishia, wakati
Mnyama aliporomoka kutokana na kukosa mipango mizuri.

Wagonga nyundo: Mbeya city fc walileta changamoto nzuri msimu uliopita
Katika michuano ya kombe la shirikisho, safari
hiyo Azam waliteleza na kuishia raundi ya kwanza kwa kutolewa na Ferroviario ya
Msumbiji.
Msimu wa 2013/2014, Azam fc wakaendeleza pale
walipoishia katika michuano ya ligi kuu na wapinzani wao wakubwa wakawa Yanga
na Mbeya City na hatimaye kuweka rekodi ya kutwaa kwa mara ya kwanza taji la
ligi kuu.
Wapi Simba? Wao waliendelea kujikongoja na
kuharibu zaidi na hatimaye kushika nafasi ya nne na mafanikio makubwa yalikuwa
kubadilisha makocha tu kuanzia Milovan Cirvovic aliyewapa ubingwa 2011/2012,
Patrick Liew, Abdallah Kibadeni, Zdravko Logarusic na sasa Patrick Phiri.
Kimsingi, Azam fc wamekuwa washindani wazuri kwa
miaka mitatu mfululizo, wakati Simba na Yanga wanabadilishana. Kama Yanga wapo
safi msimu huu, Simba wanakuwa kwenye matatizo na hivyo hivyo kwa upande wa
pili.

Wakata Miwa: Kagera Sugar msimu uliopita walijitahidi kupambana, lakini walishindwa kuvuka mafanikio ya Abdallah Kibadeni
Ninachojaribu kueleza ni kwamba timu za Tanzania
zinashindwa kuanzia pale zilipoishia katika michuano mbalimbali. Ndio maana
unaweza kushangaa Mbeya City fc waliomaliza nafasi ya tatu msimu uliopita
wakashuka nafasi za chini zaidi. Sio lazima iwe hivyo, wanaweza kupanda pia
kutokana na maandalizi yao.
Kitu kizuri zaidi katika mpira ni kuanzia
ulipoishia na unaweza kufanya hivyo kama una watu sahihi katika maeneo sahihi.
Yaani una benchi nzuri la ufundi, wachezaji wazuri na utawala bora.
Uongozi katika klabu za Tanzania ni tatizo.
Migogoro mingi inatokea bila sababu hasa kwa klabu za Simba na Yanga sc.
Wakati tunasubiri kuanza ligi kuu, niwakumbushe
wageni Stand United, Ndanda fc na Polisi Morogoro kuwa wadau wana hamu ya kuona
wanaleta ushindani wa kweli ili kuepuka ligi ya timu mbili au tatu kusaka
ubingwa.

Vipi msimu ujao?: Ruvu Shooting walijikakamua msimu uliopita
Inafahamika wazi kuwa kama timu imepanda katika
misingi imara, yaani wakati inatafuta njia ya kucheza ligi kuu ilijipanga
kuandaa timu badala ya kulazimisha kupanda kimagumashi, basi itaendelea kubakia
ligi kuu.
Lakini kama ujanja ujanja ulitumia, sitoi nafasi
ya timu hizo kuendelea kufanya vizuri zaidi ya kurudi ligi daraja la kwanza kwa
mara nyingine tena.
Mbali na hilo, nazishauri klabu kufanya maandalizi
mazuri ambayo yalianza wakati wa kucheza ligi daraja la kwanza na sasa ni
kuongeza nguvu ikiwa ni pamoja na kusajili wachezaji wengine. Kama vikosi
viliandaliwa vizuri kutoka ligi daraja la kwanza, kucheza ligi kuu ni kuongeza
nguvu tu.
Lakini viongozi nao watambue mipaka yao. Wasipende
kufanya kazi zisizowahusu. Katibu mkuu unaingiliaje mambo ya ufundi?
Na ninyi makocha bakini katika misingi ya taaluma
zenu. Msikubali kuonewa na kupangiwa mambo ya ajabu nje ya kazi yenu. Huko ni
kudhalilisha na kutoheshimu taaluma zenu.
Tunajua sasa hivi njaa imepungua kwa timu za ligi
kuu. Kuna ‘Mihela’ kutoka kwa wadhamini Vodacom, Azam TV na baadhi ya timu zina
mikataba na makampuni kama vile Binslum na TBL.
Tumieni hela hizo kiusahihi ili kuandaa timu za
kushindana. Naamini mtafanya makubwa kama mipango itakuwa mizuri.
Asubuhi njema!

0 comments:
Post a Comment