Na Baraka Mpenja
MICHUANO ya klabu bingwa Afrika Mashariki na kati,
Kombe la Kagame, imefikia patamu mjini Kigali, Rwanda ambapo hatua ya robo
fainali inaanza kutimua vumbi leo hii.
Mechi ya kwanza itaanza majira ya 9:00 alasiri kwa
kuwakutanisha Polisi dhidi ya Atletico, zote za Rwanda.
Robo fainali ya pili itaanza majira ya saa 11:00
jioni ambapo timu mbili pinzani nchini Rwanda, Rayon Sport na wanajeshi wa APR
wataoneshana kazi.
Kibarua kingine kitaendelea kesho ambapo mechi
iliyotabiriwa kuwa ngumu zaidi katika hatua hii ya kombe la Kagame
itawakutanisha mabingwa wa Tanzania, Azam fc dhidi ya El Merreikh ya Sudan.
Kutokana na historia nzuri ya El Merreikh katika
soka la Afrika mashariki na kati, hakika Azam wametumbukia katika daraja zito,
lakini kama watajipanga vizuri wanaweza kuibuka na ushindi.
Meneja wa Azam fc, Jemedari Said alisema
wamejiandaa vizuri na wanafurahia kuchuana na timu ngumu ambayo itawapa kipimo
kizuri cha kujua maendeleo ya kikosi
chao.
“Sio pambano jepesi, El Merreik ni timu yenye
historia kubwa. Sisi kama Azam hatuwaogopi, tunawaheshimu, tutapambana kupata
ushindi ili kutinga nusu fainali na hatimaye fainali na kutwaa ubingwa”.
Alisema Jemedari.
Jemedari alisema katika mazoezi ya jana jioni,
wachezaji wote waliokuwa majeruhi, Waziri Salum ambaye hajacheza mechi yoyote,
Saint Prex Lionel, Shomari Salum Kapombe
wote walifanya mazoezi, na kwa mara ya kwanza kikosi kizima kilikuwa uwanjani
kujiandaa na mchezo huo.
Mechi nyingine ya kesho jumatano itawakutanisha
KCC ya Uganda dhidi ya Altabara ya Sudan Kusini.

0 comments:
Post a Comment