Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WEKUNDU wa Msimbazi Simba wanaendelea vyema na
maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara unaotarajia kuanza
kushika kasi septemba 30 mwaka huu.
Simba wamepiga kambi visiwani Zanzibar (Unguja) chini
ya kocha mkuu mpya, Mzambia, Patrick Phiri akisaidiwa na kocha msaidizi, kiungo
wa zamani wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’, Suleiman
Abdallah Matola ‘Veron’ na kocha wa makipa, Idd Pazzi ‘Father’.
Simba ilianza programu ya mazoezi mara moja kwa
siku hapo jana katika fukwe za bahari ya Hindi, lakini Phiri ameamua kuongeza
dozi ambapo leo atafanya mazoezi mara mbili, (asubuhi na jioni).
Lengo la Phiri ni kupata muda wa kutosha wa kusuka
kikosi chake akijua wazi kuwa msimu ujao atakumbana na changamoto kubwa ya
kusaka ubingwa wa Tanzania bara.
Pia kocha huyo alisisitiza suala la mechi za
kirafiki ili kukiona kikosi chake kwa mara ya kwanza na kujua nini cha kufanya
zaidi.
Kocha huyo aliyerejea nchini kwa mara ya tatu
kuifundisha Simba baada ya kutimuliwa kwa Mcroatia, Zdravko Logarusic ‘Loga’ aliahidi
mambo mazuri kwa Simba iliyoshinda kuwika kwa miaka mitatu mfululizo.

Hans Poppe
Wakati huo huo, mwenyekiti wa kamati ya usajili ya
Simba, Keptein wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans
Poppe yuko mjini Kigali, nchini Rwanda kufuatilia michuano ya kombe la Kagame
inayoendelea nchini humo.
Uwepo wa Poppe huko Kigali unatafsiriwa kuwa ni
kujaribu kuona vifaa vipya vya kuongeza Msimbazi ikizingatiwa Shirikisho la
soka Tanzania jana limetangaza kuongeza siku 10 zaidi za usajili mpaka Agosti
27 mwaka huu badala ya siku ya mwisho iliyokuwa jana Agosti 17.
Katika siku hizo zilizoongezwa mtu makini na
mwenye mapenzi makubwa na Simba sc, Hans Poppe anaweza kuibuka na vifaa vipya
hususani wakati huu Kombe la Kagame likifikia hatua ya robo fainali itakayoanza
kutimua vumbi leo hii.
Wakati hayo yakijiri Msimbazi, nao mahasimu wao, Dar
Young Africans wanatarajia kuondoka wiki hii jijini Dar es salaam kuelekea
kisiwani Pemba, Zanzibar ambapo wataweka kambi ya kujiandaa na ligi kuu Bara.
Yanga sc watakuwa huko chini ya kocha
anayesemekana kurudisha morali ya kila mchezaji kwasasa, Mbrazil, Marcio
Maximo.
Nao wagosi wa Kaya, Coastal Union wanatarajia
kutua Pemba kesho jumanne,.
Kwa maana hiyo, mashabiki wa Zanzibar watashuhudia
timu tatu za ligi kuu soka Tanzania bara zikijivua katika ardhi yao inayosifika
kwa uzalishaji wa zao la Karafuu.

0 comments:
Post a Comment