
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MABINGWA wa zamani wa Tanzania kwa mwaka 1999 na
2000, Mtibwa Sugar wamekanusha taarifa zilizoenea mchana wa leo kuwa wameingia
mkataba wa mwaka mmoja na aliyewahi kuwa kocha wa Simba sc, Mfaransa Patrick
Liewig.
Leo mchana iliripotiwa kuwa Mtibwa imeamua
kumchukua Liewig baada ya kuvutiwa na kazi yake akiwa Simba, lakini alifukuzwa
mwaka juzi na mikoba yake kutua mikononi mwa mzalendo, Abdallah Kibadeni ‘King
Mputa’.
Mkurugenzi wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser amesema
taarifa hizo si za kweli, na wanachojua ni kwamba Mecky Mexime akisaidiwa na
Zuberi Katwila na Patrick Mwangata ndio makocha wa klabu hiyo.
“Taarifa hizo ndio nazisikia, hakuna kitu kama
hicho. Hutujawahi kuwa na mawasiliano na kocha huyo. Kocha wetu ni Mexime na
anaendelea vizuri na maandalizi ya ligi kuu msimu ujao. Kikosi chetu kipo Dar
es salaam kwasasa ”. Alisema Bayser.
Wakati huo huo, Mtibwa Sugar imetoka suluhu pacha
ya bila kufungana na JKT Ruvu katika mechi ya kirafiki iliyopigwa jioni ya leo uwanja
wa Bandari, Tandika, jijini Dar es salaam.
Mechi hiyo ilikuwa maalumu kwa makocha Mecky
Mexime wa Mtibwa na Fredy Felix Minziro wa JKT Ruvu kupimana ubavu.

0 comments:
Post a Comment