
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Agosti 16, 2014, saa 7:40 mchana
TAARIFA za mchana huu zinaeleza kuwa aliyekuwa
kocha mkuu wa Simba sc, Mfaransa, Patrick Liewig amerejea nchini kwa mara ya
pili na kujiunga na Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa meneja wa kocha huyo, Abdulfatah
Salim Saleh, Mfaransa huyo amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuwanoa mabingwa hao
wa zamani wa Tanzania kwa mwaka 1999 na 2000.
Mtibwa Sugar ilivutiwa na utendaji wa Liewig akiwa
Simba kabla ya kufukuzwa mwaka juzi na nafasi yake kuchukuliwa na mzawa, Abdallah
Kibadeni ambaye naye alifukuzwa baada ya kuiongoza klabu hiyo kwa mzunguko
mmoja msimu wa 2012/2013.
Baada ya kutimuliwa na Simba, Liewig alikuwa
anatajwa kuwania na Coastal Union, lakini taarifa hizo hazikutimia kwa wakati
huo.
Hata hivyo haijaelezwa hatima ya kocha wa sasa wa
Mtibwa Sugar, Mzalendo Mecky Mexime ambaye ana mipango kabambe ya kuirudisha
timu hiyo katika soka la ushindani nchini.
Mtibwa Sugar ni moja ya klabu kongwe nchini
Tanzania na inaendeshwa kwa mfumo wa kampuni sawa na Kagera Sugar na Azam fc.
Kurejea kwa Liewig nchini kutaongeza uhondo wa
ligi kuu kwasababu idadi ya makocha wa kigeni imeongezeka.
Yanga wananolewa na Mbrazil, Marcio Maximo, wakati
Simba wao wamemuajiri Mzambia Patrick Phiri siku chache baada ya kumtimua
Mcroatia, Zdravko Logarusic maarufu kwa jina la Loga.
Mabingwa, Azam fc wananolewa na Mcameroon, Joseph
Marius Omog wakati Mtibwa wao wameamua kumchukua Mfaransa Liewig.

0 comments:
Post a Comment