
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MSAFARA wa kwanza wa magwiji wa Real Madrid, ‘Real
Madrid Legends’ utatua nchini Tanzania kesho, ukitarajiwa kuongozwa na
mwanasoka bora wa zamani wa dunia na Ulaya, Mreno, Luis Filipe Madeira Figo.
Magwiji hao watashuka dimbani jumamosi Agosti 23
dhidi ya kikosi maalumu cha nyota wa zamani wa Tanzania ‘Tanzania All Stars’
ndani ya uwanja wa kisasa wa Taifa, jijini Dar es salaam.
Figo ataongozana na nyota wengine wawili waliotamba
na Real Madrid miaka ya nyuma, Muingereza Michael Owen na Christian Karembeu.
Figo aliyestaafu soka mwaka 2009, alishinda tuzo
mbili mfululizo mwaka 2000 ambazo mwanasoka bora wa Ulya na Dunia na katika
enzi zake za kucheza soka alikuwa mchezaji hatari kupita maelezo na sasa
anakuja kukumbushia ufundi wake katika ardhi ya Rais Jakaya Kikwete.
Mbali na Figo, mwanasoka mwingine bora wa zamani
wa dunia, Zinedine Zidane na Mbrazil Ronaldo de Lima wanatarajia kutua nchini
Ijumaa na kundi kubwa la magwiji hao.

Mkurugenzi wa makampuni ya Tanzania Sisi ni
Nyumbani (TSN) (waandaaji wa ziara hiyo), Farough Baghozah amekaririwa akisema
mapokezi makubwa kwa ajili ya magwiji hao yameandaliwa na watawasili kwa
mafungu, lakini kundi kubwa litaingia nchini Agosti 22.
Baghozah alisema magwiji hao watapokelewa kwa
maandamano kutoka uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA)
jijini Dar es salaam na kupelekwa hoteli ya Ladger Plaza, Bahari Beach.
Tayari kikosi cha ‘Tanzania All Stars’ kimeanza
mazoezi katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam chini ya kocha maarufu, Charles
Boniface Mkwasa ‘Master’akisaidiwa na Fredy Felix Minziro na Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’.
Mlinda mlango na nahodha wa kikosi hicho, Mohamed
Mwamweja ametoa wito wa Watanzania kujitokeza kwa wingi kuwaona nyota wao wa
zamani kwasababu wamejipanga vizuri.
Mwamweja alikiri
kuwa wamekaa muda mrefu bila kucheza mpira, lakini mazoezi hayo yamewaongezea
nguvu ya kucheza mechi hiyo.
Kipa huyo anayetarajia kuanza katika kikosi cha
kwanza alisema watajifunza mengi kutoka kwa magwiji hao, lakini nao watajifunza
vitu fulani kutoka kwa wachezaji wa Tanzania.
Wachezaji wanaoendelea kujifua kwa ajili ya
kukumbushia enzi zao na magwiji wa Real Madrid ni:
Makipa waliowahi kutamba nchini Tanzania, Mohamed
Mwameja na Peter Manyika.
Watakaosuka safu ya ulinzi ni mabeki Shadrack John
Nsajigwa Mwandemele, Boniface Pawasa, John Mwansasu, Mecky Mexime,
Abubakar Kombo, George Masatu na Habib Kondo,
Viungo ni: Suleiman Abdallah Matola ‘Veron’,
Shaaban Ramadhani, Salvatory Edward, Sabri Ramadhani ‘China’, Yussuf Macho
Musso, Abdul Mashine, Abdul Maneno, Mao Mkami, Steven Nyenge, Akida Makunda na
Mtwa Kihwelo.
Washambuliaji:
Monja Liseki, Iddi Moshi, Dua Said, Emmanuel Gabriel Mwakyusa, Said Maulid
‘SMG’, Thomas Kipese, Nasor Mwinyi ‘Bwanga’, Edibilly Lunyamila, Mohamed
Hussein ‘Mmachinga’, Clement Kahbuka,
Madaraka
Suleiman ‘Mzee wa Kiminyio’ na Akida Makunda.
0 comments:
Post a Comment