
Na Mwandishi Wetu, Tanga
UONGOZI wa Klabu ya Coastal Union ya Tanga
umemfungia aliyekuwa beki wa kushoto Abdi Banda kucheza mpira wa
miguu ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya kukosa nidhamu
na kusaini mikataba katika vilabu viwili tofauti.
Adhabu hiyo itahusisha kutokucheza mechi
zozote ikiwemo zile za kirafiki kutokana na kukiuka makubaliano aliyoingia na
klabu hiyo ya Coastal Union wakati aliposajiliwa.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari
leo,Katibu wa Coastal Union,Kassim El Siagi alisema kuwa uongozi umeamua
kumpa adhabu hiyo kwa kukosa nidhamu pale aliposaini mkataba mwingine
na timu ya Simba SC ya Dar es Salaam wakati akijua tayari ana mkataba wa miaka
mitatu na timu ya Coastal Union.
El Siagi alisema kuwa mchezaji huyo alikuwa
amebakiza miaka miwili kucheza timu ya Coastal Union na hivi sasa yupo katika
mikataba miwili kwa timu mbili tofauti ambazo zinashiriki ligi moja.
“Ki ukweli hali hii
hatuweza kuivumilia ndio maana tumeamua kuchukua hatua hiyo kali ili iweze kuwa
fundisho kwa wachezaji wengine wenye tabia kama hii “Alisema Katibu El Siagi.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo mchezaji
huyo atakuwa amevunja sheria na kanuni za mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini
na kulitaka shirikisho la soka kutoa ushirikiano katika maamuzi hayo.
0 comments:
Post a Comment