
Makamu wa Rais wa Simba sc, Geofrey Nyange 'Kaburu'
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WEKUNDU wa Msimbazi Simba wameipongeza bodi ya
ligi kuu soka Tanzania na Shirikisho la soka Tanzania, TFF, kutoa ratiba mapema kwa mujibu wa kanuni.
Makamu wa Rais wa Simba sc, Geofrey Nyange ‘Kaburu’
amesema kuwa kanuni inasema ratiba itoke angalau mwezi mmoja kabla ya msimu
mpya wa ligi kuanza na wahusika wamefanya hivyo kwasababu ligi itaanza septemba
20 na ratiba imeanikwa hadharani jana Agosti 20.
“Niwapongeze waendeshaji wa ligi ambao ni bodi ya
ligi na TFF kwasababu wamekidhi matakwa ya kikanuni ambapo inatakiwa ratiba
kutoka angalau mwezi mmoja kabla ya ligi kuanza,” Alisema Kaburu. “Lakini sio
hilo tu, ratiba imezingatia mambo mengi sana. Imezingatia watazamaji kwa kuwapa
nafasi kuona mechi, kwasababu mechi za katikati ya wiki zinakosa watazamaji kwasababu
ya mashabiki kutingwa na kazi”.
“Pia ratiba hii ni ya mwendelezo, tunaona ligi
inaendelea mpaka desemba huko, hakuna mapumziko. Nadhani wameangalia wenzetu.
Hakika ni ratiba nzuri kwasababu imeangalia watazamaji, wadhamini na hata
wadhamini wa TV wataweza kusafirisha vifaa kwa amani”.
Simba itaanza kampeni ya kusaka ubingwa wa ligi
kuu septemba 21 mwaka huu dhidi ya Coastal Union uwanja wa Taifa jijini Dar es
salaam.
Baada ya mechi hiyo, septemba 27 wataikaribisha Polisi Morogoro katika dimba hilo la Taifa.
Kwasasa kikosi cha Simba kipo Kisiwani Unguja,
Zanzibar, chini ya kocha mkuu, Mzambia
Patrick Phiri kikiendelea kujiandaa na msimu mpya.
Kwa miaka mitatu sasa, Simba haijawa katika ubora
wake huku ikikumbwa na mabadiliko ya mara kwa mara katika benchi la ufundi.
Lakini chini ya Phiri mwenye historia ya kuwapa
ubingwa bila kufungwa mwaka 2009, Simba wanaamini wataingia kwenye ushindani
tofauti na misimu mitatu ya nyuma.
Msimu uliopita, Simba walishika nafasi ya nne
nyuma ya Mbeya City, Yanga na mabingwa Azam fc.
0 comments:
Post a Comment