
LOUIS Van Gaal atawaomba wachezaji wake kumpa
zawadi ya kuondokea siku ya jumamosi ili awe kocha wa kwanza wa Uholanzi kushiriki kombe la dunia bila
kufungwa.
Kocha huyo wa Uholanzi atajiuzulu ili kujiunga na
klabu yake ya Manchester United mara baada ya kumalizika kwa mechi ya mshindi
wa tatu kesho dhidi ya wenyeji Brazil, mjini Brasilia.
Uholanzi walipoteza mechi ya nusu fainali dhidi ya
Argentina kwa mikwaju ya penati siku ya jumatano-lakini Van Gaal ana hamu ya
kuhakikisha timu yake inashinda ili kuweka rekodi ya timu hiyo kuondoka kombe
la dunia ikiwa imefungwa kwa penati tu.
“Itakuwa sehemu ya hotuba yangu nitakayotoa kwa
mara ya mwisho na naamini wachezaji wanataka kunipa zawadi kwa njia ya ushindi
ili tubaki kuwa timu ambayo haijafungwa,” Van Gaal amewaambia waandishi wa
habari kwenye mkutano wa kabla ya mechi leo ijumaa.
“Polepole, lakini kwa uhakika tunajua kuwa tunatakiwa
kushinda. Timu ya Uholanzi haijawahi kurudi nyumbani bila kufungwa, sasa ndio
nia yetu kwa sasa”.
“Kuna kitu tunatakiwa kufanya. Bado tunaweza
kuweka rekodi kwasababu Uholanzi ilipoteza mechi mwaka 1974 na 1978”.
Van Gaal ameumia kucheza mechi ya mshindi wa tatu baada
ya kupoteza kwa penati dhidi ya Argentina na amekiri Uholanzi inaendelea
kuimarika baada ya kushindwa kufika fainali.
“Ilikuwa huzuni kubwa sana, sana, sana na ndoto
ziliyeyuka. Haitaweza kurudia tena, lakini lengo lilikuwa ni kuwa wa kwanza”.
Aliongeza Van Gaal.

0 comments:
Post a Comment