Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi (katikati) akiongea na wachezaji wake Hassan Mwasapili (kushoto) na Peter Richard (kushoto
Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976
MBEYA City fc wamejawa na hofu kuelekea katika
mchezo wa keshokutwa uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Nje kidogo ya jiji la Dar
es salaam dhidi ya `Wauza Mitumba` wa Ilala, Ashanti United kutokana na
mazingira ya wapinzania wao wanaotaka kukwepa kushuka daraja msimu huu.
Kocha mkuu wa klabu hiyo, Juma Mwambusi amesema kuwa
kikosi walichokuja nacho hakina majeruhi
hata mmoja na sasa wapo katika mikakati ya kutafuta ushindi.
“Tunajua kila mchezo uliobaki kwetu ni muhimu.
Mazingira ya uwanja wa ugenini na mazingira ya timu tunayokutana nayo yanaifanya
mechi hii iwe ngumu zaidi, lakini hatuwezi kukata tamaa, mapambano mpaka siku
ya mwisho”. Alisema Mwambusi.
Mwambusi aliongeza kuwa hawezi kuahidi kitu chochote
kwa mashabiki wao, lakini anawaomba wazidi kuwaunga mkono ili waweze kufanya
vizuri na kuangali mwisho wa ligi watakuwa nafasi gani.
“Ligi ya mwaka huu imekuwa na ushindani mkubwa,
angalia timu ya Yanga tunayofuatana nayo tunapishana pointi moja, ingawa wana
michezo mkononi. Azam fc yupo nafasi ya kwanza kwa pointi 53, kwakweli
kumkimbiza kunahitaji juhudi kubwa sana”. Alifafanua Mwambusi.
Kocha huyo aliongeza kuwa matokeo kwasasa hayatabiriki kirahisi kwasababu timu zote zinafungwa
bila kujali ukubwa na ukongwe wao.
“Inahitajika mikakati mingi ya uwanjani kama
unahitaji kupata matokeo mazuri. Tunahakikisha tunafikia malengo yetu
tuliyojiwekea kwani muda upo na mechi
zipo”. Alieleza Mwambusi.
Kocha mkuu wa Ashanti United, Abdallah Kibadeni (wa kwanza kulia) akiangalia moja ya mechi za klabu yake
Naye kocha mkuu wa Ashanti United, Abdallah Kibadeni
`King Mputa` ameuambia mtandao huu kuwa wameweka kambi yao Bamba Beach
kigamboni jijini Dar es salaam kwa lengo la kutuliza akili za wachezaji wao
kuelekea michezo mitatu ya mwisho.
“Tumebakiwa na mechi tatu, tupo hapa Bamba Beach,
eneo ni zuri na tulivu.
Tunajiandaa kuhakikisha tunashinda mechi tatu
zilizosalia ili kujinasua kwenye mstari wa kushuka daraja”. Alisema Kibadeni.
Kibadeni aliongeza kuwa yeye mwenyewe yuko makini
pamoja na wachezaji wake kujiandaa na mchezo wa jumamosi dhidi ya Mbeya City.
“Mbeya City wanahitaji ubingwa. Kwa umoja walionao
itakuwa ngumu kuwafunga. Lakini nasisi hatuna jinsi zaidi ya kupambana kusaka
pointi tatu muhimu kama kweli tunataka kubakia ligi kuu”. Alisema Kibadeni.
Kocha huyo alifafanua kuwa mechi za mwishoni mwa
ligi hazitabiriki kwasababu kila timu inajipanga kwa njia zake kutafuta
ushindi.
“Tupo Bamba Beach kwa karibu wiki ya tatu. Viongozi
wanatumia fedha zao kutugharamia. Lazima nasisi tujidhatiti uwanjani. Kikubwa
mashabiki wetu waendelee kutuunga mkono”. Alisema Kibadeni.
Mpaka sasa Ashanti United wapo nafasi ya 12
wakijikusanyia pointi 21 katika mechi 23 walizoshuka dimbani.
Juu yao wapo Mgambo JKT wenye pointi 22 baada ya
kucheza mechi 23.
Wauza mitumba hao wa Ilala wapo katika hatari ya
kushuka daraja kwasababu mpaka sasa wapo katika timu tatu za mwisho kwenye
msimamo wa ligi kuu.
Timu nyingine mbili za mwishoni ni Rhino Rangers ya
Tabora na JKT Oljoro ya Arusha.
Mechi zilizosalia kwa Ashanti ni dhidi ya Mbeya City
jumamosi ya wiki hii uwanja wa Azam Complex.
Pia atakuwa na mchezo dhidi ya Simba sc aprili 13
Uwanja wa Taifa, huku kipute cha mwisho kikitaraji kupigwa uwanja wa Sokoine
jijini Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons.
Kibadeni atakutana na Mbeya City yenye uchu wa
kutafuta ubingwa wake wa kwanza mwaka huu, kwasababu mpaka sasa wapo nafasi ya
tatu kwa kujikusanyia pointi 45 baada ya kucheza mechi 23, pointi moja nyuma ya
Yanga waliopo nafasi ya pili kwa pointi 46.
Mbeya City watakuwa wanahitaji matokeo mazuri ili
kuishikilia nafasi ya pili kwa muda, wakati wakisubiri matokeo ya jumapili
baina ya Yanga na JKT Ruvu, uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.


0 comments:
Post a Comment