Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976
SIMBA SC ya Dravko Logarusic imesafiri leo hii
kwenda mjini Bukoba, mkoani Kagera kuwafuata wenyeji wao, `Wanankulukumbi`
Kagera Sugar katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara utakaopigwa jumamosi
uwanja wa Kaitaba.
Simba isiyohitaji ubingwa msimu huu wala nafasi ya
pili, itacheza mchezo huo dhidi ya Kagera Sugar yenye malengo ya kushika nafasi
ya tatu au nne msimu huu.
Kocha Loga atawaingiza dimbani vijana wake akiwa na
kumbukumbu ya kupigwa mabao 2-1 na Azam fc mechi iliyopita, wakati Kagera
walitoka suluhu pacha ya bila kufungana na Ruvu Shooting uwanja huo huo
utakaotumika jumamosi.
Katika kikosi cha Simba kilichoondoka leo, baadhi ya
wachezaji wa kikosi cha kwanza wameachwa kwa madai ya kupumzishwa kusubiri
mechi ya mwisho ya aprili 19 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam dhidi ya
mahasimu wao wa jadi, Young Africans.
Kocha mkuu wa Kagera Sugar, Mganda Jackson Mayanja alikaririwa
katikati ya wiki akisema kuwa Simba haimtishi sana, lakini anamuogopa sana
mshambuliaji wake hatari, Mrundi, Amisi Tambwe.
Mayanja amepumua baada ya kusikia kuwa mshambuliaji
huyo pamoja ba beki matata, Joseph Owino wameachwa katika kikosi kilichosafiri
kuelekea mjini Bukoba.
Mbali na nyota hao wa kimataifa, wegine waliochwa ni
mshambuliaji Betram Mwamboke, Kiungo Abdulhalim Humud ‘Gaucho’ na beki wa kushoto Issa Rashid `Baba Ubaya”.
Sababu iliyoelezwa na benchi la ufundi la Simba sc,
kupitia kwa kocha msaidizi, Suleiman Matola `Veron` ni kuwa Simba ina wachezaji
wengi vijana ambao wanawaamini sana na watawapa matokeo mazuri jumamosi.
Pia alisema wameamua kuwapumzisha nyota hao ili
kuwaandaa kwa ajili ya mchezo muhimu dhidi ya Yanga.
Simba inajiwinda dhidi ya Yanga katika mchezo wa
mwisho aprili 19 siku ambayo pazia la ligi kuu soka Tanzania bara litafungwa.
Timu hizi mbili zina upinzani mkubwa, hivyo Simba
licha ya kuwa katika hali mbaya msimu huu watahitaji kushinda ili kulinda
heshima yao.
Mzunguko wa kwanza zilitoka sare ya mabao 3-3 ambapo
Yanga walifunga mabao yao kipindi cha kwanza na Simba kusawazisha yote kipindi
cha pili.
Wakati wachezaji hao wakiachwa, Simba bado wamesema
wanajiandaa vizuri kwa ajili ya mechi
zilizosalia kuhakikisha wanafanya vizuri.
Afisa habari wa klabu hiyo, Asha Muhaji alisema
kupoteza mechi mbili mfululizo haikuwa mipango yao bali soka wakati mwingine
linatoa matokeo kama hayo.
“Mashabiki wetu wana uchungu sana wa timu yao
kufungwa mara kwa mara, lakini ni upepo mbaya kwetu msimu huu. Kikubwa
tuendelee kuwa pamoja na kukubali matokeo yanayotokea uwanjani. Tutajipanga msimu
ujao kwa kuimarisha kikosi chetu”. Alisema Asha.
Wakati hayo yakijiri kwa upande wa Simba, duru za
habari kutoka ndani ya kikosi cha Kagera Sugar zinasema kuwa kikosi chao
kimejiandaa vizuri kuwakabili Simba.
Murage Kabange, Kocha msaidizi wa Kagera Sugar
aliuambia mtandao huu kuwa wanawaheshimu Simba licha ya kutokuwepo katika mbio
za ubingwa mwaka huu.
“Tunajiandaa kupambana sana. Malengo yetu ni
kuhakikisha tunawafunga na kujiweka mazingira mazuri ya kushika nafasi ya pili
au tatu. Mashabiki wajitokeze kwa wingi jumamosi kutuunga mkono”. Alisema
Kabange.
Mpaka sasa, Simba sc wapo nafasi ya nne baada ya
kucheza mechi 23 na kujikusanyia pointi 36 pekee.
Msimu umekuwa mgumu kwa Simba ambao waliwafukuza
Abdallah Kibadeni na Jamhuri Kiwhelo na kuwaleta Mcroatia, Dravko Logarusic na Mtanzania, Suleiman Matola
kwa lengo la kupata matokeo mazuri zaidi ya mzunguko wa kwanza.
Hata hivyo Logan na Matola wameshindwa kuwapa Simba
mafanikio msimu huu na kuifanya kuwa timu ya `tia maji tia maji`.
Kagera Sugar wenyewe wameshuka dimbani mara 22 na kujikusanyia pointi 33 katika nafasi ya
5 ya msimamo.
Wamebakiza kiporo kimoja dhidi ya Yanga aprili 9
mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Pia wamebakiza mechi dhidi ya Simba sc, Mgambo
JTK na Coastal Union.
Kwa upande wa Simba, mechi walizosaliwa nazo ni tatu
ambapo ataanza kesho kutwa dhidi ya Kagera Sugar , atakutana na Ashanti aprili
13, na atahitimisha msimu kwa kuivaa Yanga ya Mholanzi, Hans Van Der Pluijm aprili
19 mwaka huu, uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.


0 comments:
Post a Comment