Rais
Mstaafu Benjamin Mkapa akipongezwa na Mhadhama Polycarp Kardinali Pengo
jana wakati misa ya jubilei ya miaka 75 ya kuzaliwa kwake. Picha na
Fidelis Felix.
Dar es Salaam. Rais Mstaafu,
Benjamin Mkapa jana aliadhimisha miaka 75 ya kuzaliwa kwake kwa kufanya
Ibada ya Misa iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam,
Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo.
Katika ibada hiyo ya shukrani
iliyofanyika Kanisa Katoliki la Maria Imakulata, Upanga jijini Dar es
Salaam, Mkapa aliwataka Watanzania kumshukuru Mungu kwa kila jambo.
“Tunamshukuru Mungu kwa majaliwa
aliyoipatia nchi yetu ya Tanzania na tunamwomba azidi kuijalia umoja
katika yote tunayofanya na tunayokusudia kuyafanya,” alisema Mkapa.
Mkapa pia aliwashukuru waumini
wenzake katika kanisa hilo, huku akifichua siri kwamba, Kadinali Pengo
alimtaka ahamie Kanisa la Mtakatifu Joseph wakati alipokuwa rais, lakini
hakukubali.
Kwa upande wake, Kardinali Pengo aliwataka Watanzania kuwa na tabia ya kumshukuru Mungu kwa kila jambo.
“Alichofanya Rais Mstaafu Mkapa
ni cha kuigwa. Tunatakiwa kutambua kuwa hatuishi kwa nguvu zetu bali kwa
uwezo wa Mungu hivyo ni lazima tumshukuru kama alivyofanya mwenzetu,”
alisema Kardinali Pengo.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria
ibada hiyo ni pamoja na Mawaziri Wakuu Wastaafu, Edward Lowassa na
Cleopa Msuya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa
Bunge), William Lukuvi na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Wengine
ni waziri wa zamani, Profesa Philemon Sarungi, Askofu Mkuu wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa pamoja wakuu wa
zamani wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Majenerali, Robert
Mboma na George Waitara.
CHANZO: MWANANCHI


0 comments:
Post a Comment