Na Baraka Mpenja
Wekundu wa Msimbazi Simba wanatarajia kuoneshana ufundi wa kusakata kabumbu dhidi ya wakusanya mapato wa Uganda, klabu ya URA, katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam majira ya saa 10 alasiri, ikiwa ni mechi ya kimataifa ya kirafiki.
Mnyama ambaye ametokea ziarani mikoani amerejea jijini Dar es salaam kwa lengo la mechi hiyo ya kujipima ubavu na kujaribu wachezaji wapya waliowasajili kwa ajili ya msimu mpya wa ligi kuu Tanzania bara.
Akizungumza na MATUKIO DUNIANI leo hii, Afisa habari wa klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga, Mr. Liverpool amesema kuwa hali ya wachezaji ni nzuri, na hapo jana jioni walipasha moto misuli kwa ajili ya mechi ya leo.
“Wachezaji wote wapo salama, hakika mechi ya leo ni muhimu sana kwa Simba, ingawa haina kombe wala zawadi, lakini itatumika kama sehemu ya kujaribu wachezaji wapya”. Alisema Kamwaga.
Picha kwa Hisani ya www.globalpublisher.info
Kamwaga aliongeza kuwa mechi hii ya kimataifa ni ya kwanza kwa kocha wao mpya Abdallah King Kibadeni “King Mputa” kuiongoza Simba tangu alirithi mikoba ya Mfaransa Patrick Liewig, hivyo ni muhimu sana kwake kuangalia kikosi chake ikizingatiwa anacheza uwanja anaoufahamu.
“Ni jambo jema kwa kibadeni kujipima ubavu katika mechi hii ya kirafiki ya kimataifa, wote tunawajua URA, ni timu nzuri sana na inajua kushindana katika soka, hivyo King atapata changamoto nzuri kuelekea msimu mpya wa ligi kuu Tanzania bara.” Alisema Kamwaga.
Afisa habari huyo alisisitiza kuwa Simba inajenga kikosi chake kwa ajili ya msimu mpya wakiwa na malengo ya kurejesha taji lao walilopokonywa na watani wao wa jadi, hivyo mashabiki lazima wawe wavumilivu na waiunge mkono klabu yao.
Wakati Kamwaga akielezea maandalizi ya wekundu wa Msimbazi, leo hii pia kutakuwa na mkutano wa wanachama utakaofanyika jijini Dar es salaam kuanzia majira ya saa tatu asabuhi.

Mwenyekiti huyo alisema ajenda ya kwanza itakuwa ni kujadili taarifa ya ukaguzi wa fedha za klabu, na baada ya kujadiliwa kwa ajenda hiyo, watajadili ya pili ambayo ni mipango endelevu ya klabu hiyo.
Rage aliendelea kueleza kuwa ajenda ya tatu ni Taarifa ya klabu itakayosomwa na katibu mkuu Evodius Mtawala, baada ya hapo wanachama watachangia, huku hotuba ya mwenyekiti ikifuatia na hatimaye kufungwa kwa mkutano huo.
“Cha msingi ni kuwa wanachama watakaohusika katika mkutano huo ni wale hai tu waliolipa ada ya uanachama kupitia benki. Kama mtu anafikiri ni utani basi ajitokeze siku hiyo wakati si mwanachama hai”. Alisema Rage.
Rage aliwataka wanachama wa Simba kujiandaa na mkutano huo ambao utakuwa chachu ya mafanikio ya klabu yao ikiwemo kutwaa ubingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu ujao.
0 comments:
Post a Comment