Na Baraka Mpenja
Wapiga kwata wa klabu ya jeshi la kujenga taifa, JKT Mlale ya mkoani Ruvuma wako makini na usajili wa wachezaji ili kupata nafasi ya kupanda ligi kuu bara msimu wa 2014/2015 baada ya kushindwa kufanya hivyo msimu uliopita.
Katika pita pita za MATUKIO DUNIANI kutafuta habari kwa ajili ya wasomaji wake, kocha msaidizi wa klabu hiyo, Edgar Msabila amezungumza na mtandao huu na kusema kuwa wanaendelea kujipanga kwa ajili ya msimu mpya wa ligi daraja la kwanza, huku wakihaha kutafuta wachezaji vijana kuimarisha kikosi chao.
“Katika kikosi cha JKT Mlale tunawatumia wachezaji 17 vijana, hakuna timu yenye wachezaji vijana wengi kiasi hicho kuanzia ligi kuu na ligi daraja la kwanza, sisi tunajali sana soka la vijana kwani hao ndio wenye nguvu na wanafundishika vizuri zaidi ya wakongwe”. Alisema Msabila.
Kocha huyo aliyekiongoza kikosi hicho katika michuano ya kuadhimisha Jeshi la kujenga taifa jijini Dar es salaam, alisisitiza kuwa msimu uliopita walifanya jitihada kubwa sana, lakini safu ya ushambuliaji ilikuwa na matatizo zaidi.
“Ubutu wa safu ya ushambuliaji ulituangamiza msimu uliopita, lakini kwa sasa tupo katika mipango ya kunasa vifaa vipya, tayari kuna wachezaji tumefanya nao mazungumzo na muda si mrefu tutaweka wazi majina”. Alisema Msabila.
Msabila alisema klabu yao inataka kuwa nembo ya soka la Ruvuma kama walivyofanya Maji Maji FC “Wanalizombe” miaka ya nyuma, lakini pia medani ya kitaifa na kimataifa.
“Kwa mipango tuliyonayo, tunahitaji sapoti kubwa sana kutoka kwa wadau na mashabiki wa klabu hii, kwa pamoja tunaweza na tutafika mbali zaidi”. Alisema Msabila.
Kocha huyo alisema wachezaji wake wana hamu kubwa ya kucheza ligi kuu, na mara kwa mara anazungumza nao na kuwapa moyo kuwa msimu ujao ni wao.
“Nimekuwa nikisisitiza sana suala la nidhamu na kujitambua, nawapa moyo vijana wangu na wanaelewa sana, nina uhakika tutaweza kufanya vizuri na kupata nafasi kama walivyofanya wenzetu Mbeya City, Rhino Rangers na Ashant United. Unajua msimu uliopita tulikuwa wazuri, lakini tulikuwa na changamoto kubwa sana katika safu ya ushambuliaji”. Alisema Msabila.
0 comments:
Post a Comment