Thursday, July 11, 2013


ashanti7Vijana wa Ashanti wakiwa mazoezini siku za nyuma na mpaka sasa wanaendelea na jalamba la kufa mtu
……………………….
Na Baraka Mpenja 
“Kila kona ni kazi tu, ukicheka na nyani utavuna mabua, ni jalamba la kufa mtu” hii ni kauli inayozifaa timu nyingi za ligi kuu.
Timu mpya ya ligi kuu soka Tanzania bara msimu ujao, Ashanti United ya jijini Dar es salaam imetamba kufanya vizuri katika mikikimikiki ya ligi hiyo kutokana na maandalizi ya nguvu wanayofanya sasa.
Katibu mkuu wa Klabu hiyo, Abubakar Sellasi ameuambia mtandao wa MATUKIO DUNIANI kuwa kwa sasa wanajipanga kumaliza usajili mapema kabla ya tarehe za mwisho ili kupata nafasi nzuri ya kupima kikosi chao kabla ya kuanza kibarua cha ligi kuu yenye ushindani mkubwa.
“Tunatambua wazi kuwa ligi itakuwa ngumu sana kwetu, lakini ligi daraja la kwanza ni ngumu zaidi kwani kuna timu tatu tu zinazotakiwa kupanda, tulipambana sana, na nguvu ile tutaitumia katika msimu mpya wa ligi kuu uliotangazwa kuanza agosti 24 mwaka huu”. Alisema Sellasi.
Sellasi alisisitiza kuwa kwa sasa wanaendelea na mazoezi, huku wakiendelea na zoezi lao la kusaka vipaji vipya kwa malengo ya kuchanganya na wakongwe kidogo.
“Sisi tuko makini sana, na ndio maana tunawataka mashabiki wetu kutulia wakati huu wa mawindo, cha kuwaomba ni kutuunga mkono zaidi ili tufike mbali”. Alisema Sellasi.
Pia katibu huyo alisema jumanne ya wiki ijao katika dimba la Chamazi, Mbande, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam, watacheza mechi ya kirafiki dhidi ya wenyeji wa uwanja huo, wana lambalamba Azam FC.
“Wiki ijao siku ya jumanne tutapimana na Azam fc, ni nafasi ya kupima mazoezi yetu ambayo tumefanya kwa muda sasa, mechi hii ni kipimo kizuri sana kwani wapinzani wetu wamekuwa na uzoefu wa soka la ligi kuu na mashindano ya kimataifa. Pia wana wachezaji wa kimataifa”. Alisema Sellasi.
Sellasi alisema lengo lao ni kuwapa uzoefu vijana wao kwani kwa sasa ligi imekuwa ngumu zaidi na timu zote zinacheza soka safi.
Ashanti ni miongoni mwa timu tatu zilizopanda kucheza ligi kuu soka Tanzania bara msimu ujao, wakati nyingine ni Mbeya city ya jijini Mbeya na Maafande wa Rhino Rangers ya Tabora.
Timu zote tatu zimepata nafasi baada ya Africa Lyon, wanakishamapanda Toto Africa na Polisi Moro kuporomoka daraja msimu uliopita.

0 comments:

 
https://www.sexmutant.com/ https://www.sexindrag.com/ porn movies sex videos hd porno video