Na Baraka Mpenja
Mkakati wa kuwarudisha upya katika
soka la ushidani mabingwa wa zamani wa Tanzania mwaka 1986, Tukuyu stars
“Banyambala” unazidi kushika kasi huku mpango wa muda mfupi wa kuisajili timu
hiyo kucheza ligi daraja la tatu ngazi ya mkoa ukiwa umekamilika.
Akizungumza na mtandao huu kwa njia
ya simu kutoka wilayani Rungwe mkoani Mbeya, katibu mkuu wa chama cha soka
wilayani humo, Enzi Wiliam Seme, amesema sasa Banyambala wapo ligi daraja la
tatu jijini Mbeya .
Seme amesema katika michuano ya ligi
hiyo, wamefuzu hatua ya sita bora na sasa wakishika nafasi ya pili wakiwa na
Pointi 5 nyuma ya vinara wa ligi hiyo klabu ya Magereza Ruanda waliojikusanyia
pointi 6 kibindoni.
Katibu huyo alisema hapo jana
walionesha umwamba wao kwa kuwatungua Kimondo mbozi mabao 2-1 na kuzidi
kujiweka sawa kuingia ligi daraja la pili ngazi ya taifa.
“Unajua wakati tunazindua mkakati wa
kuifufua klabu yetu, tuliweka mipango ya muda mfupi na mrefu, mpango wa kwanza
ulikuwa kuisajili timu icheze ligi daraja la tatu, sasa tumekamilisha,
tunachohangaika sasa ni kusonga mbele zaidi katika ligi hiyo”. Alisema Seme.
Seme aliongeza kuwa hatua ambayo
inaendelea kwa sasa ni kubadilisha katiba ya klabu hiyo kutoka mfumo wa ridhaa
kwenda kampuni ili kukaribisha wadau wenye nia ya kununua hisa kufanya hivyo
mara moja.
“Tunataka timu yetu iwe bora na
kitalu cha kuzalisha wachezaji, hatua muhimu pia ni kuiongoza kisasa, ndio
maana tunafanya mchakato wa kuibadili katiba yetu ili kuwapa nafasi wenye fedha
zao kununua hisa na kuimarisha klabu yetu”. Aliongeza Seme.
Pia katibu huyo alisifu serikali ya
wilaya chini ya mkuu wa wilaya Chrispin
Meela, kuwa inahaha huku na huku kuhakikisha inapata wadhamini wa kuiwezesha
timu hiyo kurejea rasmi katika soka la Tanzania na kimataifa.
Seme alijigamba kuwa chini ya Meela
hakuna kinachoharibika, lazima watanzania wawaone kwa mara nyingine Tukuyu
stars wakitanda anga za soka la Tanzania.
Pia kiongozi huyo aliongeza kuwa
wanajipanga kufanya mkutano wa pamoja na wachezaji wa zamani wa klabu hiyo
wakiwemo Godwirn Aswile, Moses Mkandawile, Willy Martin na wengineo ili kuona
wamefikia wapi na mkakati wao wa kuisaidia klabu hiyo kurejea tena.
Tukuyu stars ni moja kati ya klabu
zilizokuwa na jina kubwa sana nchini Tanzania kutokana na umoja wa wakazi wa
Mbeya, wachezaji wake maarufu kama ‘Banyambala` pamoja na na viongozi wa
serikali ambao walihamasisha kuishangilia timu hiyo.
0 comments:
Post a Comment