
Na Baraka Mpenja
Uongozi mpya wa Chama cha kandanda
mkoani Ruvuma (FARU) umejipanga kuwekeza katika soka la vijana ili kuunga mkono
mpango wa shirikisho la soka Tanzania
TFF ulizinduliwa hivi karibu na Rais wake Leodigar Chila Tenga kwa lengo la
kuwekeza katika soka hilo kwa mwaka 2013-2016.
Mwenyekiti wa chama hicho Golden
Singaone, amesema viongozi wengi wa chama hicho ukimwondoa katibu mkuuu wake ni
wapya kabisa, hivyo wamekuja na mipango mingi ya kuboresha Mpira wa miguu
mkoani humo hususani soka la vijana.
Singaone alisema uongozi huo
umeyakuta mashindano pekee ya Coca Cola, lakini sasa wanafanya mipango ya kutafuta
udhamini ili kuwa na mashindano mengi zaidi kama sehemu ya kuwaweka pamoja vijana kwa muda mrefu.
“Mimi binafsi licha ya kuwa
mwenyekiti wa chama, pia ni mdau mkubwa wa soka la vijana na ndio maana kila
mwaka ninaendesha mashindano ya viaja ya `Singaone Cup, kwakweli tunajipanga
kufanya mambo ya maana sana”. Alisema
Singaone.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa TFF
imeonesha njia nzuri ya kuthamini soka la vijana ambalo kwa sasa ndio msingi wa
timu ya taifa iliyojaza makinda wengi, endapo juhudi hizi zitaendelezwa, taifa
litanufaika sana na aina ya wachezaji watakaopatikana.
“Kikubwa ni kutafuta fedha za kutosha
ili mambo yaende sawa, soka linahitaji uwekezaji na kama tutapata watu wa kutambua
umuhimu wa jambo hili, basi itasaidia sana kujenga misingi bora ya soka letu”.
Aliongeza Singaone.
Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa
licha ya kuanza mikakati hiyo, pia wana mikakati mizito ya kuisaidia klabu
maarufu mkoani humo na Tanzania nzima, Maji maji Fc “wanalizombe” ili wasajili wachezaji makini
na kupata makocha wa kiwango cha juu.
Kwa upande wake meneja wa Majimaji FC
Godfrey Ambrose Mvula maarufu kama “Makete” amesema wameandaa tukio maalumu
aprili 27 mwaka lililopewa jina la “Maji maji day” kwa lengo la kuwakutanisha wadau wa soka
mkoani Ruvuma ili kuhamasishana kuichangia timu hiyo kwa ajili ya ligi daraja
la kwanza msimu ujao.
“Siku hiyo ni muhimu sana kwetu wana
Ruvuma, tunafikiri kuwaalika baadhi ya wachezaji wa zamani na wasanii maarufu
wa mkoa wetu, Abdallah Kibaden, Madaraka Seleman `mzee wa kiminyio`, wasanii
kama Joseph Haule `Profesa Jay` na wengine wengi wanatarajiwa kualikwa siku hiyo ili kupamba
tamasha hilo kubwa”. Alisema Mvula.
Mvula alisema baada ya tukio hilo,
wanajipanga kufanya usajili wa wachezaji wapya ambao watachanganya damu, yaani
chipkizi na wazoefu ili waimarishe klabu hiyo.
Meneja huyo aliongeza kuwa wachezaji
wengi watawatoa katika mashindano ya Coca Cola mwaka huu huku wakifanya juhudi
ya kupata makocha wa kiwango cha juu ili waiunganishe timu hiyo.
Mvula alisisitiza kuwa
kinachowasumbua sana wana Lizombe ni ukata, sasa wanajitahidi kupanga mipango
ya kupata fedha wakisaidiwa na mkuu wa mkoa huo, Said Mwambungu anayewatafutia
wadhamini.
0 comments:
Post a Comment